Wananchi wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuchunguza afya zao kama wanamaambukizi ya Homa ya Ini kutokana na tabia ya ugonjwa huo kukaa mwilini kwa miaka 20 hadi 30 bila kugundulika.
Hayo ymeelezwa leo Jijini Dar es Salaam kwenye upimaji bure wa Homa ya Ini uliofanyika katika Hospitali ya Aga Khan ambapo Daktari Bingwa wa Mfumo wa Chakula na Ini kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili John Rwegasha amesema upimaji huo unaendana na kupatiwa chanjo kwa ambae hajaupata na walioambukizwa kupatiwa matibabu.
“Watanzania wengi hawana chanjo ya Ini kutokana na chanjo hiyo kuanza kutolewa mwaka 2002 kwa watoto wanaozaliwa hivyo waliozaliwa kabla ya hapo wako hatarini kupata maambukizi ya Homa ya Ini kutokana na miili yao kutokuwa na kinga”Amesema Dkt. Rwegasha.
Aidha amesema kuwa virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Ini vipo vya aina tano na vinapoingia katika mwili wa binadamu huenda moja kwa moja kushambulia Ini na kadri linavyoendelea kuathirika husababisha kupata magonjwa nyemelezi.
Dkt. Rwegasha ameongeza kuwa uambukizwaji wa virusi hivyo unatofautiana ambapo kirusi A na E vinambukiza kwa njia ya unywaji wa maji machafu yaliochanganyika na kinyesi na dalili zake ni kuumwa tumbo na kuharisha, virusi B na C vikiambukiza kwa njia ya damu, ngono, isiyo salama, kushirikiana vitu vya ncha kali na unyevuunyevu wa kushikana huku kirusi D kuambukiza kupitia mama mjamzito kwenda kwa mtoto.
Aidha amesema katika kutokomeza ugonjwa huo ni jukumu la kila mmoja kuchukua hatua ambapo kupitia Shirika la Takwimu la Taifa NBS takwimu zinaonyesha kuwa watu 4 kati ya 100 wanamaambukizi ya Homa ya Ini huku watu walioko katika makundi hatarishi kuwa hatarini zaidi.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Saratani kutoka Hospitali ya Aga Khan Harrison Chuwa amesema katika hospitali hiyo kwa mwaka hupata wagonjwa 4 wenye saratani ya Ini ambao hutokana na kutopata matibabu ya haraka ya Homa ya Ini na hufariki baada ya miezi 18.
Sambamba na hayo amesema saratani ya Ini ni hatari na inashika namba mbili Duniani kwa kuua na inachangiwa na Homa ya Ini hivyo wananchi wajitokeze kwa wingi kupima na kupatiwa chanjo na kama wanamaambukizi wapatiwe matibabu ili kuepuka kupata homa ya Ini inayosababisha saratani ya Ini ambayo huua kama usipoiwahi.
Naye Daktari Bingwa wa Mfumo wa Chakula na Ini kutoka Hosptali ya Aga khan Casmir Wambura amesema takwimu za kidunia zinaonyesha kuwa asilimia 10 tu ya watu wenye Homa ya Ini wanaojijua hivyo kuna haja ya elimu zaidi kuendelea kutolewa kwa Jamii.