Na
Omary Mngindo, Chalinze.
WATUMISHI
wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Chalinze (CHALIWASA) wilaya ya
Bagamoyo Mkoa wa Pwani, wametakiwa kuwatuliza wateja na kuwapa lugha nzuri,
hasa pale wanapokuja kwenye ofisi wakiwa na jazba.
Kauli
ya Mhandisi Raymond imefuatia malalamiko kutoka kwa Abdallah Kipolelo,
aliyelalamikia kuwepo kwa baadhi ya viongozi wa CHALIWASA kutokuwa na lugha
nzuri, mara baada ya kupokea taarifa za utendaji wa kazi kutoka kwa wateja.
Hayo
yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo Mhandisi Honest Raymond,
alipozungumza na watumishi katika kikao cha kukumbushana majukimu ya kazi, huku
suala la nidhamu likisisitizwa katika kikao hicho.
"Sisi
tunafundishwa namna ya kuwahudumia wateja, wao hawana somo kama hilo hivyo
unapokutana na mteja anakuwa mkali, wewe jukumu lako ni kumtuliza, kwani wakati
mwingine anaweza kufikia hatua ya kukupiga ngumi," alisema Mhandisi
Raymond.
Kwa
upande wake Kipolelo alisema kuwa kuna wakati mtumishi anapokea simu ya upole
kutoka kwa mteja akimjulisha kuwepo kwa uvujaji maji eneo alilopo, lakini
utakuta kiongozi anapiga simu kwa ukali, hatua aliyodai kama ya udhalilishaji.
"Mteja
anakupigia simu kwa upole akikuelezea kuwepo kwa tatizo eneo moja, wakati
huohuo unapigiwa simu kwa lugha ya ukali kutoka kwa kiongozi, wee Kipolelo uko
wapi, nenda eneo fulani kuna tatizo, lugha ambayo ni ya udhalilishaji,"
alisema Kipolelo.
Akitoa
mada katika kikao hicho, Elizabeth Eusebius ambaye ni Ofisa Maendeleo ya Jamii
aliwaambia watumishi hao kuwa wameamua kutoa mafunzo hayo kwa lengo la kuongeza
ufanisi wa utendaji kazi wa taasisi.
"Tumekuwa
tukijikita katika utoaji wa elimu kwa watumiaji wa maji, kwetu tumejisahau
warsha tunayopeana leo inalenga kufahamishana masuala mbalimbali ili wote
tukafanyekazi za Mamlaka," alisema Elizabeth.
No comments:
Post a Comment