Na Selemani Magali; Daresalaam
ADHA ya
kubangua korosho kwa kukoka moto sasa huenda ikabaki historia baada ya mamlaka
ya Ufundi Stadi (VETA) Songea kubuni mashine
ndogo ya kubangulia korosho yenye uwezo wa kubangua debe tatu
kwa siku, huku ikiwa na uwezo wa kutenganisha ubora wa bidhaa hiyo.
Mwalimu
kutoka VETA Songea, Susack Mbulu, amesema hayo katika banda la VETA,
lililopo katika maonesho ya 43 ya biashara ya Kimataifa
(DITF), yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere
barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam.
Amesema mashine hiyo inatumia nguvu za
binadamu na itawasaidia wazalishaji wadogo kuondokana
na mfumo wa kukoka moto na kukaanga korosho na
kisha kuanza kuzipasua kwa mkono, badala yake sasa watatumia
mashine hiyo.
"Ukitumia mashine hii, unaweza kutenganisha korosho
kwa ubora, yaani kama ni daraja la kwanza hadi la tatu. Na iwapo mtumiaji
wa mashine hii ataanza kubangua bila kukausha korosho
hizo vyema zitavunjika na iwapo zitakauka hazitovunjika bali
zitatoka sawa," amesema.
Ameongeza
kuwa mashine hiyo inauwezo wa kuanza kubangua korosho
ndogondogo ama zilizo kubwa kwa kuwa ina meno ya aina mbili ambayo kwa
pamoja yanaweza kubangua zao hilo na kumrahisishia mkulima mdogo.
Hata hivyo,
Mbulu ameushukuru uongozi wa VETA makao makuu kwa
ushirikiano wao na kuwezesha kutekeleza wazo
hilo, ambalo linaunga mkono dhana ya serikali ya
kufikia uchumi wa kati ambao ni wa
viwanda.
Amesema
katika kufikia uchumi wa viwanda VETA inaunga
mkono jitihada hizo ambapo wataweza kuwafikia na
kuwasaidia wajasiriamali wadogo. Lakini pia kusaidia korosho
kuingia sokoni katika hali ya ubora.
"Lengo letu ni kuhakikisha mashine hii inafikia
kiwango cha kutumia umeme au mota ambayo itafikisha hatua ya
kubangua hata gunia moja kwa siku la
korosho," amesema.
Aidha
amewashauri wafanyabiashara wa korosho kuwasiliana na VETA
ili kuweza kupata mashine hiyo na kuahidi kuwa
wanaweza kuifikisha serikali katika uchumi wa
viwanda.
No comments:
Post a Comment