Na Selestian James.
Wanachama wa
klabu ya yanga wilayani Bagamoyo wameadhimisha wiki ya wananchi kwa kufanya
usafi maeneo mbalimbali ya mji wa Bagamoyo.
Shughuli hiyo
ya usafi imewajumuisha watu wa kada mbalimbali ambao ni wanachama wa yanga
wakiongozwa na Diwani wa kata ya Nianjema
iliyopo katika halmashauri ya wilaya Bagamoyo, Abdul Mzee Pyallah ambaye
pia ni katibu wa hamasa ya kuchangia Yanga Bagamoyo.
Miongoni mwa
sehemu walizofika kufanya usafi ni pamoja na Hospitali ya wilaya ya Bagamoyo.
Shughuli hiyo
yenye kauli mbiu "funga kazi kusanya kijiji" ni miongoni mwa hatua
muhimu za maadhimisho ya wiki ya wananchi
ambayo ilizinduliwa visiwani Zanzibar na itafikia
kilele mwanzoni mwa mwezi ujao katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam.
Sambamba na
hilo Diwani Pyallah pia amezungumzia uwepo wao tena hospitalini hapo siku ya
tarehe tatu ni kwa ajili ya kutembelea
wodi ya watoto na kutoa zawadi mbalimbali kwa wagonjwa.
Aidha,
alisema watatembelea kituo cha watoto waishio
katika mazingira magumu kilichopo katika kata ya Nianjema, na ziara hiyo
itamalizikia katika gereza la Kigongoni kwa ajili ya kuwaona wafungwa gerezani
humo.
Miongoni mwa
shughuli walizoweza kufanya ni pamoja na kuchangia damu kwa wagonjwa pamoja na
kushiriki na wananchi katika shughuli za kijamii ikiwa vitendo vinavyoakisi
makusudio ya wiki ya wananchi.
Kwa upande wao
madaktari waliokuwepo katika tukio hilo wameeleza kufurahishwa na hatua hiyo na
kuwapongeza huku wakiwaomba kuendeleza utamaduni huo.
Aidha,
waliowaomba pia kusaidia kifaa maalum cha kupimia upumuaji wa watoto kwani ni
moja ya vifaa vinavyohitajika sana katika utendaji kazi wa hospitalini hapo.
Wanachama wa Yanga Bagamoyo wakishiriki katika usafi wa mazingira katika hospitali ya wilaya Bagamoyo, ikiwa ni katika kuadhimisha wiki ya wananchi.
Diwani wa kata ya Nianjema
iliyopo katika halmashauri ya wilaya Bagamoyo, Abdul Mzee, akishiriki usafi wa mazingira pamoja na wananchama wengine wa Yanga ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya wananchi.
PICHA ZOTE NA SELESTIAN JAMES.
No comments:
Post a Comment