Sunday, July 28, 2019

WAUGUZI BAGAMOYO WAADHIMISHA SIKU YA WAUGUZI KWA KUCHANGIA UJENZI WA ZAHANATI.

Muuguzi mkuu wilaya ya Bagamoyo, Bi Rehema Kingu, akizungumza katika sherehe za siku ya wauguzi zilizofanyika kiwilaya katika kijiji cha Mwavi kata ya Fukayosi wilayani humo.
 
Muuguzi mkuu wilaya ya Bagamoyo, Bi Rehema Kingu, akizungumza katika sherehe za siku ya wauguzi zilizofanyika kiwilaya katika kijiji cha Mwavi kata ya Fukayosi wilayani humo,  kushoto ni Mgeni rasmi katika sherehe hizo, Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa.
............................ 

Wauguzi wilayani Bagamoyo wameadhimisha siku ya wauguzi kiwilaya, kwa kuchangia ujenzi wa Zahanati katika kijiji cha mwavi kilichopo kata ya Fukayosi wilayani humo.


Akizungumza wakati wa maadhimsho hayo mbele ya mgeni rasmi Mbunge wa jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa, Muuguzi mkuu wilaya ya Bagamoyo, Bi Rehema Kingu, alisema wamefikia hatua ya kufanya maadhimisho hayo kijijini hapo ili kuunga mkono juhudi za wananchi ambao walianza kujitolea kujenga zahanati katika kijiji hicho.


Alisema katika jamii imejengeka dhana kwamba wauguzi ni watu wenye tabia ya ukali na hivyo kuonekana hawapo karibu na jamii ambao ndio wagonjwa watarajiwa wanaotakiwa kuwauguzwa.


Aliongeza kuwa, ili kuondoa dhana hiyo, wauguzi wilayani Bagamoyo wameamua kuchangia vifaa mbalimbali vya ujenzi ili kuunga mkono juhudi hizo za wananchi na kutengeneza mahusiani mema kati ya wauguzi na wananchi.


Alisema katika hatua hiyo waliweza kuwasiliana na wadau mbalimbali ili kufanikisha malengo hayo na kwamba wapo walioitikia wito huo hali inayoleta faraja ili kuwaondolea adha wananchi wa kijiji hicho kutembea umbali mrefu kufuata zahanati.


Alisema wauguzi ni watu wenye huruma ambao hufanya kazi zao kwa kuzingatia miko na maadili ya kazi yao na kwamba ikitokea muuguzi anakuwa mkali kwa mgonjwa ni katika hali kumsaidia usalama wake wakati wa kutibiwa.


Aliendelea kusema kuwa, ili wauguzi wawe na furaha katika kazi yao wanawajibika kuhakikisha mgonjwa anakuwa salama ikiwa ni pamoja na kupunguza vifo vya kina mama na watoto.


Alisema katika wilaya ya Bagamoyo wauguzi wamejipanga na kuchukua ahadi ya kudhibiti madhara na vifo vya kina mama na watoto na hilo ndio lengo la muuguzi wakati wa kutekeleza majukumu yake.


Aidha, ameiomba jamii na wadau mbalimbali kuunga mkono juhudi za wauguzi ili kupunguza vifo vya kina mama na watoto na kwamba utekelezaji wa azma hiyo wadau wana mchango mkubwa wa kusaidia kutatua baadhi ya changamoto zilizopo huku kina mama wakitakiwa kufuata maelekezo ya kitaalamu wakati wa ujauzito na kujifungua.


Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Mbunge wa jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa amesema anawashukuru wauguzi kwa kufanya maadhimisho yao katika kijiji cha Mwavi yakiwa na lengo la kuchangia ujenzi wa Zahanati.


Alisema katika jimbo la Bagamoyo bado kuna baadhi ya vijiji vina changamoto ya kupata huduma ya afya ikiwemo kijiji cha Mwavi na vitongoji vyake, na kwamba juhudi za ujenzi wa Zahanati katika kijiji hicho zinapaswa kuungwa mkono na kila mwananchi anaeguswa.


Dkt. Kawambwa alisema kitendo walichikifanya wauguzi wa Bagamoyo kina akisi dhana ya muuguzi katika jamii na kwamba hali hiyo inaleta faraja kwa viongozi na wananchi kwa ujumla.


Aliongeza kwa kusema kuwa, wakazi wa kijiji cha Mwavi na vitongoji vyake watajivunia kuwa na wauguzi kwani daima watakumbuka mchango wa wauguzi katika kijiji cha Mwavi, kata ya Fukayosi na Bagamoyo kwa ujumla.


Katika ujenzi huo wa Zahanati Mbunge wa jimbo la Bagamoyo katika hatua za awali aliweza kuchangia shilingi milioni moja na laki tano, 1,500,000 kutoka mfuko wa jimbo ili kufanikisha kazi hiyo.


Aidha, katika harambee hiyo iliyoongozwa na wauguzi wa wilaya ya Bagamoyo, Mbunge huyo alichangia fedha shilingi laki tatu.


Jumla michango yenye thamani ya shilingi milioni saba na laki nne 7,400,000 imekusanywa katika harambee iliyosimamiwa na wauguzi wa wilaya ya Bagamoyo, kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali huku wauguzi wenyewe wakitoa Saruji mifuko 40 yenye thamani ya shilingi 520,000.


Awali akisoma risala mbele ya mgeni rasmi, Muuguzi Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Bi, Rehema Kingu, alisema miongoni mwa changamoto wanazokabiliwa nazo ni pamoja na upungufu wa wauguzi, kutolipwa fedha za likizo, pamoja na kutopandishwa vyeo kwa wakati.


Maadhimisho ya wauguzi duniani hufanyika kila mwaka ambapo Kauli mbiu ya mwaka huu katika siku ya wauguzi ni "Wauguzi sauti inayoongoza, Afya kwa wote".

 Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Mbunge wa jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa, akipata chai pamoja na wauguzi wa wilaya ya Bagamoyo kabla ya kuaza rasmi sherehe hizo zilizofanyika kijiji cha Mwavi kata ya Fukayosi wilayani humo.
 Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa (kushoto) akisikiliza ratiba ya sherehe hiyo, katikati ni Muuguzi Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Bi Rehema Kingu, na kushoto ni Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Wauguzi Tanzania, wilaya ya Bagamoyo, Bi Sikujua Mturo.
 
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa (kushoto) akipokea risala kutoka kwa Muuguzi Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Bi Rehema Kingu.
 
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa, akizungumza katika sherehe hizo.

Sehemu ya wauguzi wa wilaya ya Bagamoyo wakiwa katika sherehe hizo zilizofanyika kijiji cha Mwavi kata ya Fukayosi wilayani humo.

Baadhi ya kina mama wa kijiji cha Mwavi waliojitokeza kwenye sherehe hizo
 
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa, (kulia) akimkabidhi cheti Mratibu wa masoko kutoka kampuni ya Hill Group, Patrick Luambano, kama ishara ya kutambua mchango wa kampuni yao katika kuchangia ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Mwavi.
 Wauguzi wa wilaya ya Bagamoyo kwa pamoja wakikabidhi Saruji mifuko 40 kwa uongozi wa kijiji cha Mwavi ikiwa ni mchango wao katika ujenzi wa Zahanati ya kijiji hicho kilichopo kata ya Fukayosi wilayani humo.


 Muonekano wa jengo la Zahanati ya kijiji cha Mwavi, picha ya juu ni muonekano wa nyuma na picha ya chini ni muonekano wa mbele, Wauguzi wilayani Bagamoyo wameadhimisha siku ya wauguzi katika jengo hilo, lengo ni kuhamasisha wadau mbalimbali kuchangia ujenzi huo ili jengo hilo likamilike na wananchi wa kijiji hicho wapate huduma ya afya jirani na makazi yao.

Picha ya pamoja, mgeni rasmi, Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa, viongozi wa kijiji na kata, viongozi wa wauguzi pamoja na wauguzi kwa ujumla, mara baada ya kumaliza maadhimisho hayo, wakiwa mbele ya jengo la Zahanati linaloendelea kujengwa.

No comments:

Post a Comment