Thursday, July 4, 2019

TFS BAGAMOYO YAKAMATA MKAA KWENYE BASI LA ABIRIA.

 Askari wa usalama barabarani wilayani Bagamoyo, (CPL) Machiwa, akizungumza jambo na Yusuf Haruna, ambae ni Mkuu wa kikosi cha doria kutoka Wakala wa Huduma za misitu wilaya ya Bagamoyo (mwenye kapelo)
Askari wa usalama barabarani wilayani Bagamoyo, (CPL) Machiwa, akizungumza na maafisa wa TFS, Dreva wa basi hilo na Kondakta pamoja na Abiria mara baada ya basi hilo kukamatwa likiwa linasafirisha mkaa kinyume na sheria, kushoto ni Afisa misitu kutoka wakala huduma za misitu Michael Makala,
Mkuu wa Usalama barabarani wilaya ya Bagamoyo, (DTO) Mkaguzi Msaidizi wa Polisi (AIP), Azizi Zuberi (katikati) akitoa maelekezo kwa askari wake wa usalama barabarani (CPL) Machiwa (kulia) kuhusu hatua za kuchukua badaa ya basi la abiria kukamatwa kwa kosa la kubeba mkaa, wanaosikiliza kulia ni Afisa misitu kutoka wakala huduma za misitu Michael Makala, na kushoto ni Yusuf Haruna, ambae ni Mkuu wa kikosi cha doria kutoka Wakala wa Huduma za misitu wilaya ya Bagamoyo.
 
 Muonekano wa mkaa ulivyopakiwa kwenye basi la abiria.
 Abiria wakiwa wamedowaa baada ya basi walilopanda kukamatwa Bagamoyo kwa kosa la kubeba Mkaa,
Askari wa usalama barabarani wilayani Bagamoyo, (CPL) Machiwa, akizungumza na abiria kuwataka watulie huku taratibu za kisheria zikiendelea kuchukuliwa kwa dereva na kondakta wa basi hilo.
  
Afisa misitu kutoka wakala huduma za misitu Michael Makala, akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukamata basi la abiria likiwa limebeba mkaa.

Tukio hilo limetokea kituo cha ukaguzi wa mazao ya misitu kilichopo Sanzale wilayani Bagamoyo.
...............................  


Wakala wa huduma za misitu nchini (TFS) wilaya ya Bagamoyo wamekamata Basi la Abiria lenye namba T 612 DFU likiwa limebeba mkaa gunia 18 kinyume na sheria.


Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukamata basi hilo, Afisa misitu kutoka wakala huduma za misitu Michael Makala, amesema mkaa huo umesafirishwa kinyume na sheria ya usafirishaji wa mazao ya misitu hapa nchini.


Ameongeza kuwa, usafirishaji wa mkaa huo kwenye basi la abiria umekiuka sheria kwakuwa hakuna vibali vya kusafirisha mkaa wala risiti ya kulipia ushuru.


Aliongeza kuwa, mara kadhaa wamekuwa wakikamata mabasi yakipakia mkaa kwenye buti la gari jambo ni hatari pia hata kwa usalama wa abiria na gari.
Makala alitumia nafasi hiyo kuwaonya madereva wa mabasi kuacha tabia ya kusafirisha mazao ya misitu bila ya kufuata sheria.


Alisema utoroshaji wa mazao ya misitu unachangia kuikosesha serikali mapato na kufanya uharibifu wa misitu kwakuwa uvunaji na usafirishaji vyote vinatakiwa kuzingatia sheria.


Alisema TFS wilaya ya Bagamoyo wamejipanga kufanya doria kila aina ya usafiri ili kubaini utoroshaji wa mazao ya misitu na kuwaonya wale wote wenye tabia ya kubeba mazao ya misitu bila ya kufuata sheria waache mara moja ili kuepuka usumbufu na hasara.


Nae Mkuu wa Usalama barabarani wilaya ya Bagamoyo, (DTO) Mkaguzi Msaidizi wa Polisi (AIP), Azizi Zuberi amesema usafirishaji wa mkaa kwenye basi la abiria ni miongoni mwa makosa hatarishi katika makosa ya usalama barabarani.


Alisema mara kadhaa mkaa unakuwa hauzimiki vizuri kutoka kwenye tanuri lake hivyo kubeba mkaa kwenye basi la abiria kunaweza kusababisha mlipuko wa moto na kuhatarisha usalama wa abiria.


Alitumia nafasi kuwataka madereva kuacha tabia ya kupakia mkaa kwani ndani ya mabasi na kwamba atakaekamatwa atachukuliwa hatua za kisheria.


Zuberi alisema atahakikisha katika eneo lake la kazi (wilaya ya kipolisi Bagamoyo) hakuna basi la abiria ambalo litapita likiwa limebeba mkaa.


Alisema askari wa usalama barabarani wilaya ya Bagamoyo wamejipanga kushghulikia madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani.


Kwa upande wao abiria wa basi hilo wamewapongeza Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) Wilaya ya Bagamoyo kwa kukagua mabasi yanayobeba mkaa na kuyakamata kwani kwa kufanya hivyo watachunga nidhamu ya kazi.


Aidha, wamesema ukiukwaji wa sheria za barabarani kunapelekea ajali na usumbufu kwa abiria ambao wangependa kufika safari zao kwa muda maalum.

No comments:

Post a Comment