Friday, July 12, 2019

WAJASIRIAMALI PWANI WATAKIWA KUBUNI BIDHAA MPYA.



Mbunge wa viti maalum mkoa wa Pwani, Subira Hamisi Mgalu, akiangalia bidhaa zinazotengenezwa na wajasiriamali wilayani Bagamoyo wakati alipokuwa akikagua vikundi vilivyokopeshwa na Halamashauri hiyo, kushoto mwenye miwani ni Diwani wa kata ya Magomeni Bagamoyo, Bi Mwanaharusi Jarufu.
...............................

Na Selestian James.

Mbunge wa viti maalum mkoa wa Pwani, Subira Hamisi Mgalu, amewataka wajasiriamali mkoani humo kubuni Bidhaa mpya ili kukabiliana na ushindani katika masoko ya bidhaa za wajariamali.


Mgalu ameyasema hayo katika Halmashauri ya Bagamoyo wilayani humo, alipokuwa akikagua vikundi vilivyokopeshwa na Halmashauri hiyo ili kujiridhisha kama mjumbe wa mikopo kuona kama fedha hizo zimefika kwa walengwa na kufanyiwa kazi zilizokusudiwa.


Alisema wajasiriamali wengi wanalalamika bidhaa zao kukosa soko hali inayopelekea kukata tamaa ya kuendelea kuzalisha kwakuwa mitaji haikuwi kutokana na mauzo hafifu.


Aliwasihi kubuni bidhaa za aina mbalimbali na hasa kutumia fursa ya vitu ambavyo havipatikani katika eneo husika, vitu vinavyoendana na utamaduni wa watu wa eneo husika, kuangalia bidha ambayo haipo katika eneo husika itengenezwe pamoja na kuzingatia ubora wa bidha.


Alisema katika kipindi hiki ambacho mifuko ya plastic imepigwa marufuku na wananchi kutumia mifuko mbadala ni kipindi cha kutumia fursa ya kubuni mifuko mbadala inayoendana na mazingira na utamaduni wa watu wa Pwani ili kukidhi mahitaji ya wateja na kupanua wigo wa ubunifu katika ujariamali.


Akitolea mfano, Mgalu, alisema watu wa Pwani wanaasili ya kutumia vikapo hivyo wajasiriamali watengeneze vikapo kwa wingi ili kwenda sambamba na mahitaji, na kwamba wasipotumia fursa hiyo watu wa pwani watanunua vikapo kutoka mikoa mingine jambo ambalo litawafanya washindwe kuingia kwenye ushindani wa bidhaa.


Subira Mgalu ambae pia ni Naibu Waziri wa Nishati amewataka wananchi wilayani Bagamoyo kujitokeza kuchukua fomu za kuunganishwa umeme ili kutumia fursa ya punguzo la bei katika kuunganishwa umeme ambao kwa sasa ni shilingi elfu ishirini na saba tu 27,000.


Awali akisoma taarifa, Afisa Maendeleo ya Jamii anaeshughulikia mfuko wa vijana wilaya ya Bagamoyo, Halima Shabani, alisema Halmashauri ya Bagamoyo imetoa zaidi ya milioni 92 kwa vikundi vya wanawake na milioni 70 zimetolewa kwa vijana katika kipindi cha mwaka wa fedha wa mwaka 2018/2019 na hivyo kufanya jumla fedha zilizotolewa mwaka huu ni zaidi ya milioni 162.


Aidha, alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2015/2016 milioni 53 zimetolewa kwa vikundi vya vijana na milioni 59 kwa vikundi vya wanawake ambapo mwaka wa fedha 2016/2017 jumla ya milioni 136 zimetolewa kwa vikundi vya vijana na vikundi vya wanawake milioni 134, huku mwaka wa fedha 2017/2018 shilingi milioni 131 kwa vikundi vya wanawake na milioni 114 kwa vikundi vya vijana.


Akiwa katika ziara hiyo, Mbunge wa viti maalum mkoa wa Pwani, Subira Mgalu  alifanikiwa kukagua vikundi vya kata za Magomeni, Nianjema, na Kiromo ambapo alijiridhisha kuwa vikundi vyote vilifikiwa na fedha.


Kwa upande wao viongozi wa vikundi hivyo vilivyokopeshwa wameishukuru serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Magufuli kwa kuwajali wanawake na vijana katika kujikwamua kiuchumi.


Aidha, walisema kwa sasa hawana sababu ya kuingia kwenye vikundi vya mitaani ambavyo wanaweza kutapeliwa na badala yake wanapata mikopo kwa fedha za serikali ambazo hazina riba.
  
Mbunge wa viti maalum mkoa wa Pwani, Subira Hamisi Mgalu, akiangalia bidhaa zinazotengenezwa na wajasiriamali wilayani Bagamoyo wakati alipokuwa akikagua vikundi vilivyokopeshwa na Halamashauri hiyo,
  
Mbunge wa viti maalum mkoa wa Pwani, Subira Hamisi Mgalu, akiangalia bidhaa zinazotengenezwa na wajasiriamali wilayani Bagamoyo wakati alipokuwa akikagua vikundi vilivyokopeshwa na Halamashauri hiyo, kushoto mwenye miwani ni Diwani wa kata ya Magomeni Bagamoyo, Bi Mwanaharusi Jarufu.
 
Mbunge wa viti maalum mkoa wa Pwani, Subira Hamisi Mgalu, akiwa katika picha pamoja na vikundi vya wajasiriamali Halmashauri ya Bagamoyo.

Picha zote Na Selestian James.

No comments:

Post a Comment