Friday, July 26, 2019

KAMPUNI ZA BIMA ZATAKIWA KUPANUA WIGO WA HUDUMA.

Kamishna wa Sera kutoka wizara ya fedha na mipango, Mgonya Benedicto, akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango katika ufunguzi wa mkutano wa nne wa mwaka wa washauri na madalali wa bima nchini uliofanyika leo tarehe 26 julai 2019, mjini Bagamoyo.

Serikali imezitaka kampuni za bima nchini kuongezaa idadi ya wananchi wanaotumia bima hasa wakulima na wafugaji ili kufikia lengo la serikali la kufikisha asilimia 50 ya watu wazima wanaopata huduma ya bima ifikapo mwaka 2029.


Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philipo Mpango wakati wa ufunguzi wa mkutano wa nne wa mwaka wa washauri na madalali wa bima nchini uliofanyika leo tarehe 26 julai 2019, mjini Bagamoyo.


Katika hutuba iliyosomwa kwa niaba yake na Kamishna wa Sera kutoka wizara ya fedha na mipango, Mgonya Benedicto, Dkt. Mpango amesema ushirikiano kati ya serikali na Kampuni za bima utaleta tija ili kuimarisha sekta ya bima hapa nchini.


Alisema watanzania wengi uchumi wao unategemea kilimo, hivyo ni vyema sasa kampuni za bima zikafikiria kupanua wigo wa huduma ya bima ili iweze kuwafukia wakulima na wafugaji ili nao wafaidike na bima za mazao na mifugo.


Aliongeza kwa kusema kuwa, sekta ya bima hapa nchini imekuwa na mchango mdogo kwenye pato la taifa na kwamba ili kuongeza mchango wa sekta hiyo mipango imara na madhubuti inahitajika ikiwa ni pamoja na mageuzi katika mazingira ya udhibiti na usimamizi wa sekta, ushirikiano wa kimkakati na taasisi zingine na utashi wa kufanya mabadiliko.


Aidha, alisema serikali inapenda kuona mamlaka ya bima na kampuni za bima zinajiandaa kutoa mchango katika uchumi wa viwanda ili kwenda sambamba na juhudi za serikali za kufikia kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.


Dkt. Mpango aliwahakikishia washauri na madalali wa bima kuwa, serikali ya awamu ya tano imeweka kipaumbele katika sekta ya fedha hasa bima.


Alitumia nafasi hiyo kuitaka Mamlaka ya Usimamizi wa bima Tanzania (TIRA) kutekeleza sheria ya bima ya mwaka 2019 na marekebisho yake ili kuhakikisha taifa linanufaika na uwepo wa sekta ya bima hapa nchini.


Aliongeza kuwa, Mamlaka ya Usimamizi wa bima Tanzania (TIRA) na wadau wengine wanapaswa kuweka mazingira wezeshi ili kuhakikisha kwamba upatikanaji wa bidhaa na huduma za bima na kuimarishwa ili kuwafikia watanzania wengi zaidi.


Dkt. Mpango alimalizia kwa kuwataka Mamlaka ya Usimamizi wa bima Tanzania (TIRA) na wadau wote wa bima waweke juhudi katika katika kutoa elimu kwa umma ili kujenga uelewa kwa wananchi.


Kwa upande wake Kamishna wa bima Tanzania, Dkt. Musa Juma amesema miongoni mwa mikakati ya kukuza uelewa kwa jamii kuhusu umuhimu wa huduma ya bima ni kutumia vyombo vya habari ili wananch wengi waweze kuhamasika na kujiunga na bima.


Alisema watu wengi hawaelewi umuhimu wa bima hali inayopelekea kuona haiwahusu jambo ambalo linapaswa kurekebshwa kwa kutoa elimu.


Dkt. Juma alisema Mamlaka ya bima inajipanga kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa bima ili kufanikisha malengo ya kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa huduma ya bima.


Nae Rais wa Chama cha Washauri na Madalali wa Bima (TIBA), Amir Kiwanda, amesema kuna changamoto kubwa ya kuwafikia wananchi wa vijijini hasa wakulima na wafugaji kwakuwa wengi wao hawapatikani sehemu moja na kwamba hawana vyama vya kuwaunganisha.


Alisema mkutano huo unatoa fursa kwa washiriki kuwasilisha changamoto mbalimbali zinazikaabili sekta ya bima ili kuwe na azimio la pamoja kutokana na mapendekezo ya wadau.


Kauli mbiu ya mwaka huu ni "Bima jumuishi kwa ukuaji wa Uchumi na kupunguza Umasikini"
  Kamishna wa bima Tanzania, Dkt. Musa Juma, akizungumza katika mkutano wa nne wa mwaka wa washauri na madalali wa bima nchini uliofanyika leo tarehe 26 julai 2019, mjini Bagamoyo.
 
Rais wa Chama cha Washauri na Madalali wa Bima (TIBA), Amir Kiwanda, akizungumza katika mkutano wa nne wa mwaka wa washauri na madalali wa bima nchini uliofanyika leo tarehe 26 julai 2019, mjini Bagamoyo.
 
Kamishna wa Sera kutoka wizara ya fedha na mipango, Mgonya Benedicto, akifurahia jambo na Kamishna wa bima Tanzania, Dkt. Musa Juma, katika mkutano wa nne wa mwaka wa washauri na madalali wa bima nchini uliofanyika leo tarehe 26 julai 2019, mjini Bagamoyo.
 
Washiriki wa mkutano wa nne wa mwaka wa washauri na madalali wa bima nchini uliofanyika leo tarehe 26 julai 2019, mjini Bagamoyo wakisikiliza mada zilizokuwa zikiwasilishwa katika mkutano huo.


 Washiriki wa mkutano wa nne wa mwaka wa washauri na madalali wa bima nchini uliofanyika leo tarehe 26 julai 2019, mjini Bagamoyo wakisikiliza mada zilizokuwa zikiwasilishwa katika mkutano huo.
 
Kamishna wa Sera kutoka wizara ya fedha na mipango, Mgonya Benedicto, akiwa katika picha ya pamoja na viongozi na wajumbe wa Chama cha Washauri na Madalali wa Bima (TIBA), katika mkutano wa nne wa mwaka wa washauri na madalali wa bima nchini uliofanyika leo tarehe 26 julai 2019, mjini Bagamoyo.

No comments:

Post a Comment