Waziri
wa Nishati Dkt. Medard Kalemani akizungumza na wananchi wa kijiji cha
Nyarugondo wilayani Karagwe, Mkoa wa Kagera (hawapo pichani), wakati wa hafla
ya kuwasha rasmi umeme kijijini hapo.
....................................
Na Veronica Simba – Kagera
Waziri wa Nishati Dkt. Medard
Kalemani amewasha rasmi umeme katika kijiji cha Nyakabwera wilayani Kyerwa na
Nyarugondo wilayani Karagwe, Mkoa wa Kagera, tukio lililoibua furaha kwa wakazi
wa vijiji hivyo.
Akiwa amefuatana na viongozi na
wataalamu mbalimbali wa serikali na vyama vya siasa; Waziri aliwasha umeme
katika maeneo hayo na kuzungumza na wananchi, akiwa katika ziara ya kazi, jana,
Julai 18, 2019.
“Nampongeza Rais wetu Dkt. John Pombe
Magufuli; anafanya kazi kubwa. Katika sekta ya nishati, amedhamiria kufikisha
umeme katika vijiji vyote nchini,” Waziri Kalemani aliwaambia wananchi.
Kabla hajawasha rasmi umeme katika
vijiji hivyo, Waziri alitoa hamasa kwa wananchi wa maeneo husika ambao
hawajaunganishiwa umeme, kuchangamkia fursa hiyo kwa kujitokeza kwa wingi
kulipia gharama inayohitajika ambayo ni shilingi 27,000 ili wote wawe na umeme.
Vilevile, aliwataka kulinda
miundombinu ya umeme iliyopo katika maeneo yao ili kuiwezesha serikali
kuendelea kuwapatia huduma hiyo kwa ufanisi.
Alisema atakayebainika kuhujumu
miundombinu hiyo, atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Pia, aliwashauri viongozi wa taasisi
za umma pamoja na miradi mbalimbali ya kijamii kama vile mitambo ya maji,
shule, vituo vya afya, masoko, nyumba za ibada na kadhalika, kutenga fedha za
kulipia huduma ya kuunganishiwa umeme ili nishati hiyo ipelekwe katika maeneo
hayo muhimu.
“Sambamba na hilo, viongozi ainisheni
maeneo ambayo mmepanga kujenga miradi ya maendeleo na taasisi za umma ili
mkandarasi ayapelekee umeme, ili muda wa kujenga utakapofika, kuwepo na nishati
hiyo tayari,” alielekeza.
Aidha, Waziri alihamasisha matumizi
ya vifaa vya Umeme Tayari (UMETA) katika kuunganisha umeme ili kuepuka gharama
kubwa za kutandaza mfumo wa nyaya za umeme kwenye majengo. Aligawa vifaa hivyo
bure katika vijiji vyote viwili na kumtaka mkandarasi anayetekeleza mradi wa
umeme vijijini katika maeneo hayo kutowauzia wananchi vifaa hivyo hadi pale
vilivyotolewa bure na serikali vitakapoisha.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti,
viongozi mbalimbali wa serikali na vyama vya siasa katika maeneo hayo,
waliishukuru serikali kwa jitihada zake za kuwafikishia wananchi maendeleo
kupitia uunganishaji umeme.
Waliomba maeneo yaliyosalia
yafikishiwe huduma hiyo mapema ili wananchi wote wanufaike kwa kuanzisha
biashara ndogondogo kwa ajili ya kuinua maisha yao kiuchumi.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard
Kalemani (katikati), akikata utepe kabla ya kuwasha rasmi umeme katika nyumba
ya Bwana na Bibi Josam Paulo ikiwa ni ishara ya uwashaji rasmi wa umeme katika
kijiji cha Nyarugondo wilayani Karagwe, Mkoa wa Kagera, Julai 18, 2019. Wa
kwanza kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Dkt. Tito Mwinuka na wa wa
kwanza kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga.
Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Rashid
Mwaimu (kushoto) akimweleza Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (kulia),
hali ya upatikanaji wa umeme wilayani humo. Waziri alifika ofisini kwa Mkuu wa
Wilaya Julai 18, 2019 akiwa katika ziara ya kazi.
Waziri wa Nishati Dkt. Medard
Kalemani akielekea kuwasha umeme katika makazi ya baadhi ya wananchi wa kijiji
cha Nyarugondo wilayani Karagwe, Mkoa wa Kagera akiwa katika ziara ya kazi,
Julai 18, 2019.
Sehemu ya umati wa wananchi wa kijiji
cha Nyakabwera wilayani Kyerwa, Mkoa wa Kagera, wakimsalimu Waziri wa Nishati
Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) kwa kuinua mikono, alipofika kuwawashia
rasmi umeme na kuzungumza nao, akiwa katika ziara ya kazi Julai 18, 2019.
No comments:
Post a Comment