MWANDISHI WETU
Tanzania, kupitia Wizara ya Viwanda na Bishara na Bohari Kuu
ya Dawa (MSD), imeandaa mkakati malumu wa uzalishaji wa dawa, kwa ajili ya
kuhudumia nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano wa Mradi wa
Uzalishaji Dawa na Vifaa Tiba kwa Ubia wa Sekta ya Umma na Sekta Binafsi jana,
Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa alisema mchakato huo unaanza
wakati Tanzania ikijiandaa kuwa mwenyeji wa mkutano wa SADC, hatua inayoaksi
juhudi za Serikali katika kujenga uchumi imara.
Alisema hatua ya ujenzi wa viwanda vitatu vya kutengeneza
dawa na vitendanishi nchini itasaidia kunusuru sehemu ya Sh Trilioni 1.2
zinazokwenda nje ya nchi kwa ajili ya ununuzi wa dawa zinazosambazwa nchini na
katika nchi za SADC chini ya MSD.
“Kimsingi, wakati Tanzania inakwenda kuwa mwenyeji na
kushika uenyekiti wa SADC kuanzia Agosti mwkaa huu, tunahitaji pia kuifanya iwe
mzalishaji wa dawa na vitendanishi kwa ajili ya nchi zote 16 wanachama, Afrika
Mashariki na Afrika.
“Kwa hiyo tumeweka mazingira rafiki kwa ajili ya uwekezaji
mkubwa katika sekta hii ya uzalishaji wa dawa na vitendanishi. Serikali pia
inaendelea kupitia sheria ambazo ni kero kwa uwekezaji, ambazo tutazipeleka
katika bunge lijalo kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu alisema tayari
andiko maalumu kw ajaili ya kuanzisha viwanda vya dawa kwenye maeneo matatu
nchini limeshakamilika na sasa wanafanya jitihada za kukaribisha wawekezaji.
Alisema katika wazo hilo jipya la kuanzisha viwanda vya dawa
kwa kushirikisha sekta binafsi, ujenzi wa viwanda hivyo vya za hospitali
umegawanywa katika maeneo matatu, ambayo ni Mwanza ambapo kutajengwa kiwanda
cha bidhaa za pamba, Mbeya kwa ajili ya kiwanda cha maji-tiba na Pwani kwa
ajili ya kiwanda cha bidhaa mchanganyiko.
“Kwa sasa MSD ndiyo
inayosambaza dawa katika nchi za SADC, lakini asilimia 85 ya dawa zote
zinanunuliwa nje ya nchi. Afrika Kusini ndiyo inayoonekana kinara katika nchi
hizi kwa mauzo ya dawa, lakini bado ina uhitaji mkubwa kwa sababu inaweza
kuhudumia asilimia 25 tu ya watu kwake kwa bidhaa za ndani.
“Kwa hiyo wakati tukielekea katika utani ujao wa SADC, moja
ya mambo muhimu ni kuhamaisha uwekezaji wa viwanda hivi vya dawa, ili fedha
inayokwenda nje, ambayo kwa sasa inafikia Sh Trilioni 1.2 kwa mwaka ibaki
katika nchi hizi,” alisema.
Alisema uwekezaji katika viwanda hivyo nchini utasaidia
kupungua gharama za usafirishaji na uhifadhi wa dawa ambazo huchukua hadi miezi
tisa kufika nchini, pia utaongeza ajira na kupanua wigo wa teknolojia.
Kamishna wa Ushirikishaji wa Seta ya Umma na Sekta Binafsi
(PPP), Dk John Mboya alisema maandiko ya uwekezaji huo utakaogharimu zaidi ya
Sh Trilioni 1.1 tayari yameshakamilika, ambapo unatarajiwa kuzalisha zaidi ya
ajira rasmi 800.
“Sheria ya PPP pia imeweka wazi kwamba uwekezaji wowote
lazima ushirikishe wazawa, kwa hiyo mwekezaji yeyote atakayejitokeza kama
akipatikana kutoka nje, atalazimika kushirikisha pia wazawa,” alisema.
Akitoa ufafanuzi, Meneja wa Mradi huo wa Uwekezaji katika
Viwanda vya Dawa kwa ubia na PPP, Fred Pondamali alisema hatua ya kupata
wawekezaji hadi kusaini mikataba rasmi inatarajiwa kuchukua muda wa miezi sita,
hivyo wawekezaji wanatarajiwa kuingia rasmi kwenye ujenzi kuanzia Juni 2020.
“Miradi hii inashindanishwa na watakaoshinda ni wale wenye
uwezo wa kifedha na teknolojia. Kwa hiyo utaratibu wa kuwashindanisha hadi
kuwakabidhi washindi maeneo ya uwekezaji utachukua muda mrefi kidogo,” alisema.
Alisema katika uwekezaji huo, kiwanda cha bidhaa za
hospitali zinazotokana na pamba kinachotarajiwa kujengwa Mwanza kitazalisha
bidhaa za aina tatu, cha bidhaa za maji-tiba huko Mbeya kitazalisha bidhaa za
aina 10 na cha dawa mseto huko Pwani kitazalisha bidhaa za aina 223.
No comments:
Post a Comment