Na
Omary Mngindo, Rufiji
WAKAZI
wa Kijiji cha Mloka Kata ya Mwaseni Wilaya ya Rufiji Mkoa wa Pwani, wamemuomba
Waziri wa Maliasili na Utalii Hamisi Kigwangala, kufungua Ofisi ndogo kijijini
hapo ili kuwadhibiti tembo wanaozagaa.
Diwani
wa Kata hiyo Saidina Malenda ambaye pia ndio Mwenyekiti wa halmashauri ya
Rufiji, ameyasema hayo kijijini hapo alipozungumza na BAGAMOYO KWANZA BLOG,
ambapo alisema kuwa mara kadhaa tembo wamekuwa wakionekana mtaani, hali
inayoleta taharuki kubwa kwa wananchi.
Alieleza
kwamba tembo hao ambao hawajaleta madhara kwa binadamu, huingia kijijini hapo
wakitokea bonde la Hifadhi ya Selou, huku ikielezwa sababu kubwa inatokana na
kutopata chakula cha kutosha wawapo kwenye hifadhi hiyo ndipo wanalazimika
kufika kijijini hapo.
"Kwa
siku tembo anakula kilo 300, kutokana na upungufu wa chakula wanakuja mpaka
huku, ofisi ya Kata tuna mikakati ya kukabiliana na hali hiyo, tumenunua mabomu
tunawafukuza wanapokuja, tunamuomba Waziri Hamisi Kigwangwala atufungulie ofisi
ndogo itakayokuwa na askari," alisema Malenda.
Kwa
upande wake Imani Matimbwa alisema kuwa hawaoni sababu ya kwenda katika hifadhi
ya Selou kutokana na tembo kuonekana kijijini hapo kila wakati, sanjali na
wanyama wemgine wadogowadogo ambao huzagaa pasipokuwa na hofu yeyote.
"Ukienda
katika hifadhi ya Selou wanalazimika kutumia zaidi ya shilingi 30,000, sasa
shida hiyo ya nini wakati wanyama wenyewe tunawaona hapahapa kijijini, sisi
hatuna shida kama hiyo," alisema mkazi huyo.
Nae
Fatuma Ally alisema kuwa kutokana na adha hiyo inayohusisha wizara za maliasili
na kilimo, ni vyema kwa Mawaziri wote wawilo wakafika kwa pamoja kuangalia ni
namna gani wanavyoweza kutusaidia kuondokana na adha hiyo.
"Tuna
shida kubwa ya kupambana na wanyama hao, kwani mashambani shida mtaani
matatizo, wanapokuja kijijini watoto kwa kutowatambua utawaona wanawafukuzia
kwa nyuma jambo ambalo ni la hatari," alisema Fatima.
No comments:
Post a Comment