Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde akizungumza na Viongozi, Watumishi wa Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro na wakazi wa Marangu wakati wa hafla fupi ya kuwaaga vijana watakaopanda Mlima Kilimanjaro ikiwa ni ishara ya kumbukizi ya miaka 20 ya Kifo cha Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere.
....................................
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulia
Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde (Mb) amewataka vijana kuenzi mchango
wa Baba wa Taifa, Mwl. Julius Kambarage Nyerere kwa kuwa wazalendo na wenye
mshikamano katika kujenga Taifa.
Mhe. Mavunde amesema hayo wakati wa hafla fupi ya
kuwaaga vijana kutoka Mkoa wa Songwe, Arusha, Tanga, Kaskazini Unguja na Kusini
Unguja kabla ya kupanda Mlima Kilimanjaro ikiwa ni ishara ya kumbukizi ya miaka
20 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwl. Nyerere iliyofanyika Mkoani Kilimanjaro
katika Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA).
Alisema kuwa vijana wanapaswa kuwa wazalendo kwa
kuiga kivitendo yale yote yaliyotendwa na waasisi wa taifa hili, Mwl. Julius K.
Nyerere na Hayati Mzee Abeid Karume kwa kuendelea kudumisha upendo, amani na
mshikamo kwa mustakabali wa Taifa.
“Vijana waliowengi kipindi hiki wameweka pembeni
uzalendo wa kulipenda taifa lao hali ambayo inatubidi tujitahmini na kuenzi
falsafa walizokuwa nazo waasisi wetu ambao waliweka maslahi ya Taifa mbele
wakati wote,” alisema Mavunde.
Akitolea mfano wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, namna ambavyo amekuwa mstari wa
mbele katika kuwatumikia wananchi kwa kutekeleza masuala mbalimbali ya kitaifa
wakati wote ili nchi isonge mbele kimaendeleo.
Pia alitumia nafasi hiyo kuwapongeza vijana
waliopanda mlima huo awamu ya kwanza na awamu hii ya pili kwa kuonesha ushujaa
na uzalendo kwa Taifa lao ikiwemo kuwa mabalozi wazuri katika kutangaza sekta
ya utalii.
Aidha, Naibu Waziri Mavunde alitoa wito kwa vijana
kuacha kukaa kwenye vijiwe na kujihusisha kwenye mambo yasio na tija, bali
wajishughulishe kwenye miradi mbalimbali itakayo wawezesha kiuchumi na kusaidia
kukua kimaendeleo, kwa kuwa waasisi wa taifa walikuwa wachapakazi, waadilifu na
wabunifu ambao ni mfano mzuri wa kuigwa.
“Hakuna nchi yoyote dunia ambayo inaweza kuendelea
pasipo kuhusisha nguvu kubwa ya vijana katika maendeleo ya taifa,” alieleza
Mavunde
Aliongeza kuwa ili kufikia malengo kwenye uchumi wa
viwanda ni lazima vijana wazingatie uzalendo, utaifa na bidii katika kazi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Mhe.
Kippi Warioba alisema kuwa kitendo cha vijana hao kushiriki katika kupanda
Mlima huo ni jambo muhimu kwa taifa na inaashiria namna gani vijana wameanza
kutambua historia ya waasisi wa taifa lao.
Naye, Kiongozi wa Vijana hao waliopanda Mlima
Kilimanjaro Bw. Augustine Gusha aliunga mkono maelezo yaliyotolewa na Naibu
Waziri na alitumia nafasi hiyo kuwasihi vijana kudumisha amani ya nchi wakati
wote.
Katika Mbio za Mwenge wa Uhuru Mwaka 2019, Ofisi ya
Waziri Mkuu kupitia Idara ya Maendeleo ya Vijana inaratibu shughuli ya kupanda
Mlima Kilimanjaro kwa Vijana 100 kwa ajili ya kumbukizi ya Miaka 20 ya Kifo cha
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Awamu ya kwanza vijana
walipanda mlima huo tarehe 26 Machi, 2019 na awamu ya pili 26 Julai, 2019.
Awamu ya Tatu itakuwa mwezi Oktoba.
Mkuu wa
Wilaya ya Moshi, Mhe. Kippi Warioba akielezea jambo kwa vijana 8 walioshiriki
katika shughuli hiyo ya kupanda Mlima Kilimanjaro ikiwa ni kuadhimisha
kumbukizi ya miaka 20 ya Kifo cha Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere.
Kushoto ni Mkurugenzi wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo kutoka Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar, Bi. Mwanaidi Ali.
Baadhi ya
Watumishi wa Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro wakimsikiliza Naibu Waziri,
Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe. Anthony Mavunde (hayupo
pichani) wakati wa hafla ya kuwaaga vijana hao.
Sehemu ya
Vijana wanaotarajiwa kupanda Mlima Kilimanjaro kwa awamu ya pili wakimsikiliza
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe. Anthony Mavunde
(hayupo pichani) kabla ya kuanza safari ya kupanda Mlima huo, Julai 26, 2019.
Naibu
Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe. Anthony Mavunde
akiwaaga Vijana hao nane (8) kutoka Mkoa wa Songwe, Arusha, Tanga, Kaskazini
Unguja na Kusini Unguja alipowasindikiza vijana hao waliokuwa wakipanda Mlima
huo. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Moshi Mhe. Kippi Warioba.
No comments:
Post a Comment