Saturday, July 27, 2019

Anne Makinda awaasa madiwani wanawake kuwajibika

Na Mwandishi wetu - Mwanza
Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda, amewataka  wabunge na Mdiwani wa vitimaalum nchini kusimamia kikamilifu rasilimali za umma ili ziwanufaishe wananchi wote.
Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda, akitoa ufafanuzi wa jambo katika semina ya kujenga uwezo viongozi wanawake wa serikali za Mitaa (WASEMI).

Akizungumza Jijini Mwanza katika semina ya kujenga uwezo kwa viongozi wanawake wa serikali za Mitaa (WASEMI) iliyoandaliwa na shirika la TGNP Mtandao, Makinda alisema kwamba, mchango wa wabunge na madiwani wa viti maalum umekuwa hauonekani vizuri au kutambuliwa na jamii kutokana na wao wenyewe kuwa na hofu au kutokujiamini kitu ambacho kimechangia kuwarudisha nyuma na kushindwa kuendelea mbele.

“tatizo letu sisi viongozi Wanawake, tunajenga hofu, tunaogopa sana kujitokeza na kuwajibika vizuri kwa wananchi, eti kwa sababu ni viti maalum. Sisi tulianzia pia viti maalum , lakini tulipata nafasi ya kwenda jimboni kwasababu tulijiamini, tuliwajibika kikamilifu na tulihangakikisha uwezo wetu unaonekana na kila mmoja. Jitokeze, kwa wananchi, watumikie kwa uadilifu na watakuona na kutambua mchango wako” alisema Makinda

Makinda amewaasa wanawake viongozi wa serikali za Mitaa, kuhakikisha wanasimamia ubora wa huduma za jamii kwenye halmashauri zao na kuhakikisha kila kinachofanyika kwenye halmashauri wanakielewa vizuri na kutoa taarifa kwa wananchi wote.
Awali akizungumza Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake viongozi wa serikali za Mitaa (WASEMI), ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmshauri ya Wilaya ya Morogoro Bi. Kibena Kingo, alisema kwamba WASEMI itahakikisha wenyeviti  wa halmshauri wanawake wanaonesha mfano bora wa utendaji uliotukuka kwenye halmashauri zao hasa kutokomeza rushwa, ubadhirifu  wa mali za umma na kuhakikisha kila senti iliyopangwa kwajaili ya kuboresha maisha ya wananchi inatumika vizuri.

“Niwaombe ndugu zangu, viongozi wanawake wa halmshauri pamoja na madiwani, sisi wanawake tumeaiminiwa tukapewa nafasi, tusimamie vizuri rasilimali za halmshauri zetu, tujenga mtandao wa kutokomeza Ukatili wa Kijinsia, tutenge bajeti nzuri inayozingatia usawa wa kijinsia na kuboresha maisha ya wananchi wote bila ubaguzi” alisema Bi. Kingo

Mkutano huu ambao umeandaliwa kwa ushirikiano wa TGNP Mtandao na WASEMI ulihudhuriwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Serikali za Mitaa ALAT Gulamhafeez Mukadam, na Naibu waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi Bi. Anjelina Mabula ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ilemela jijini Mwanza. 

Tanzani ina Halmshauri 185, ambapo kati ya hizo, wanawake wanaoongoza Halmshauri ni watano pekee ambazo ni halmashauri za Biharamulo, Hai, Mwanga, Morogoro na Gairo. Ambao wamekubaliana kuhakikisha wanaweka hitoria ya kuwa halmashauri za mfano kwa maendeleo na zenye kuzingatia usawa wa kijinsia katika Nyanja za uongozi na mipango.
Mwenyekiti wa Umoja wa Serikali za Mitaa ALAT Gulamhafeez Mukadamika akitoa neno katika semina iliyofanyika jijini Mwanza ya kuwajengea uwezo viongozi wanawake wa serikali za mitaa.

Naibu waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi Bi. Anjelina Mabula ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ilemela jijini Mwanza akiongea na washiriki wa semina hiyo.

No comments:

Post a Comment