Serikali imetumia zaidi ya shilingi
bilioni 19 kukarabati shule kongwe 17 nchini lengo likiwa ni kuboresha
mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika shule hizo za kitaifa ambapo
jukumu la uratibu wa ukarabati wa shule hizo 17 ilipewa Mamlaka ya Elimu Tanzania
(TEA).
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa
Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako wakati wa makabidhiano ya
Miradi ya ukarabati wa shule hizo 17 yaliyofanyika katika shule ya sekondari ya
wavulana Sengerema, wilayani Sengerema Mkoani Mwanza ambapo amesema ukarabati
huo umefanywa kwa kutumia fedha za Serikali.
Prof. Ndalichako amesema ukarabati wa
shule hizo 17 zilizosimamiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania ni utekelezaji wa
mpango kabambe wa serikali wa kukarabati shule zote 89 kongwe za serikali
ambapo amesema mpaka sasa tayari shule kongwe 46 zimeshakamilika.
Alisema serikali inaendelea na
utekelezaji awamu ya tatu ya mpango huu ambapo shule nyingine 17 zitakarabatiwa
mwaka huu wa fedha.
Akizungumzia ukarabati huo Waziri
Ndalichako alisema kama uamuzi wa uboreshaji wa mazingira ya kufundishia na
kujifunzia katika shule kongwe usingefanyika mapema kungeweza kutokea majanga
kwani hali ya miundombinu ilikuwa katika hali mbaya hasa katika mifumo ya
umeme, maji safi na taka na mapaa mengi yalikuwa yameoza kabisa.
Nawaambia watanzania kwamba tulikuwa
na hatari ya kupata majanga makubwa kama shule hizi zisingefanyiwa ukarabati
huu mkubwa kwani sehemu nyingine hali ilikuwa mbaya zingeweza kudondoka na
katika baadhi ya shule mabati ambayo yalikuwa yameezekwa ni yale ambayo kiafya
hayaruhusiwi amesema Waziri Ndalichako.
Alisema ukarabati huo mkubwa katika
shule kongwe umewezekana kufanyika kutokana na mwelekeo wa Serikali wa Awamu ya
Tano ya kuhakikisha kwamba huduma kwa wananachi zinaboresha na dhamira ya
serikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli ya kuhakikisha kwamba fedha za umma zinaelekezwa kwa ajili ya
maendeleo.
'Fedha zilizotumika katika uboreshaji
huu ni matunda ya kodi za watanzania, narudia tena ni fedha za umma ambazo
zimetolewa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba watoto wa kitanzania ambao wana
safari ya kupata elimu wanapata katika mazingira bora" alisisitiza
Ndalichako.
Ndalichako amepongeza Uongozi wa
Wilaya, shule na mshauri muelekezi ambao ni Chuo Kikuu cha Sayansi na
Teknolojia Mbeya kwa usimamizi mzuri wa mradi huo pamoja na kusimamia vizuri
matumizi ya fedha za mradi huo ambapo alisema hali na ubora wa majengo
inavyoonekana inaakisi thamani ya fedha zilizotolewa.
Hata hivyo amewaasa wanafunzi kujenga
utamaduni wa kutunza majengo na vifaa na viongozi wa shule hizo kuhakikisha pia
pamoja na kutunza wanajenga utamaduni wa kufanya ukarabati mdogondogo kila
wakati.
Prof. Ndalichako alisema serikali
inaendelea kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji ambapo alitolea
mfano katika mwaka wa fedha ulioisha wa 2018/19 serikali kupitia Mradi wa Lipa
kulingana na Matokeo EP4R ilitenga na kutoa fedha ambazo ziliwezesha kujengwa
kwa madarasa 1,208, mabweni 222, matundu ya vyuo 2,141 na nyumba za walimu 99
pamoja na kutatua changamoto ya huduma ya maji safi ambapo katika baadhi ya
shule visima vilichimbwa.
Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Emanueli
Kipole amemshukuru waziri kwa uboreshaji wa sekta ya elimu katika wilaya hiyo
kwani mambo makubwa yanafanyika katika kuhakikisha utoaji wa elimu unaboreshwa
ukiondoa ukarabati wa shule sekondari ya wavulana Sengerema.
Ameeleza baadhi ya miradi ambayo
tayari imeshapatiwa fedha ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya shule
kiasi cha milioni 254, milion 410 kwa ajili ya ukarabati wa chuo cha wananchi
ambacho kilikuwa kimechakaa na sasa inajengwa ofisi ya uthibiti ubora wa shule
kwa zaidi ya shilingi milioni 152 ambazo zimetolewa na wizara.
Mwenyeiki wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu
Tanzania Prof. Maurice Mbago amemshukuru waziri na serikali kwa kuiamini Bodi
ya Mamlaka hiyo kwa kuwapa kazi yakusimamia ukarabati wa shule kongwe 17 kati
ya 89 na kutoa ufadhili wa asilimia 100 jambo ambalo linaonyesha ilivyodhamiria
kuboresha elimu hususan mazaingira ya kufundishia na kujifunzia.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Elimu Tanzania(TEA) Bahati Geuzye alimweleza waziri kuwa TEA iliingilia
makubaliana ya kiutendaji na Halmashauri za maeneo husika juu ya usimamizi wa
kazi kwa kusaidiaana na wataalam elekezi katika kusimamia ili matokeo ya kazi
yaweze kutokea kwa wakati.
Waziri ndalichako katika kukabidhiwa
mradi huo pia alitembelea Shulle ya Sekondari ya Wasichana Bwiru iliyoko katika
Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza ambayo imekarabatiwa katika mradi huo ambapo
ametumia nafasi hiyo kuiagiza Mamlaka ya Elimu Tanzania kuwajengea Bweni moja
katika shule.
Mbunge wa Jimbo hilo Mh. Angelina Mabula alimpongeza na
Kumshukuru Waziri wa Elimu kwa jitihada kubwa zinazoedelea katika kuboresha
mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji katika Wilaya hiyo na kuahidi
kushirikiana kuhahakikisha shule hiyo inafanya vizuri zaidi katika mitihani ya
kitaifa.
Shule 17 zilizokarabatiwa kwa uratibu
wa TEA ni pamoja na Shule ya sekondari ya Dodoma, Mwenge sekondari singida,
Sekondari ya Wasichana Ruvu, Kilakala Sekondari na Shule ya Sekondari Ilboru.
No comments:
Post a Comment