Kwa mara ya kwanza tangu avishwe cheo
cha Kamishna Mhifadhi wa Misitu na Mhe. Dkt Hamisi Kigwangalla, Waziri wa
Maliasili na Utalii na hatimaye kula Kiapo cha Utii na uadilifu mbele ya Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli Julai 9, 2019, Kamishna Prof. Dos Santos Silayo amewasili makao
Makuu ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), jana, Julai 12 jijini Dar
es salaam na kupokelewa na Viongozi Waandamizi na watumishi wa TFS.
Akizungumza na watumishi wake mara
baada ya kuwasili ofisini hapo, Kamishna Prof. Silayo alisema mabadiliko
yanayotokea katika sekta ya maliasili yamepelekea pia kubadili mfumo wa
usimamizi na utendaji wetu toka ule wa Kiraia kwenda Jeshi Usu.
Hatua hiyo ikapelekea kuvishwa cheo
cha Kamishna Mhifadhi wa Misitu na Mhe Dkt. Hamisi Kigwangalla, Waziri wa
Maliasili na Utalii na kula Kiapo cha Utii mbele ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama
Dkt. John Pombe Magufuli siku ya tarehe 9 Julai 2019.
“Mabadiliko hayo yanalenga kujenga
uwezo wa taasisi, uwezo wa watumishi ikiwa ni pamoja na kuwajengea ari,
uzalendo, weledi na ujasiri katika kusimamia rasilimali za misitu na nyuki,”
alisema Kamishna Prof. Silayo.
Kamishna Prof. Silayo alisema uwezo
wa watumishi wa TFS utaenda sambamba na weledi katika matumizi ya mbinu na
vifaa vya kisasa vinavyoweza kumudu mabadiliko ya changamoto za uhifadhi
kuanzia usalama wao pamoja na usalama wa mali zenyewe unaotokana na kuongezeka
kwa mbinu za kihalifu kila wakati.
Aidha Prof. Silayo alitoa shukurani
kwa Mheshimiwa Rais na viongozi wote wa wizara ya Maliasili na Utalii kwa hatua
hiyo waliyofikia ambayo anaamini itasaidia kukuwa kwa sekta ya misitu nchini na
kuongeza ushirikiano na wadau wengine hususani wananchi katika kusimamia misitu
yetu.
Akiongea kwa njia ya simu Naibu
Kamishna wa Huduma Saidizi, Emmanuel Wilfred alisema mabadiliko hayo
yamepelekea kubadili mfumo wa usimamizi na utendaji wa TFS toka ule wa Kiraia
kwenda Jeshi Usu na hivyo kulazimu watumishi wote kwenda kwenye mafunzo.
“Tunaendelea kutoa mafunzo kwa
watumishi wachache waliobaki na kwa wale waliokwishakwenda kwenye mafunzo
tunakamilisha taratibu ili Kamishna aweze kuwatunuku vyeo vyao, lakini niwatake
wafanyakazi wote kuenda sambamba na mabadiliko kwa kasi hitajika,” alisema
Kamishna Msaidizi huyo.
Rosemary Sabida mmoja wa watumishi wa
TFS anasema mabadiliko hayo yataisaidia TFS kukabiliana na changamoto
mbalimbali za uhifadhi nchini.
Jumla ya Makamishna wanne, Kamishna
wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Dkt Allan Kijazi, Kamishna
wa Uhifadhi wa Misitu toka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof Dos
Santos Silayo na Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori
Tanzania (TAWA) Dkt. James V. Wakibara pamoja na Kamishna wa Uhifadhi wa
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Freddy Manongi walivishwa vyeo vya
kijeshi Julai 9, 2019 katika sherehe za Uzinduzi wa Hifadhi ya Taifa ya Burigi
– Chato zilizofanyika wilayani Chato mkoani Geita.
No comments:
Post a Comment