Naibu wa Waziri wa Nishati, Subira
Mgalu amewataka wakandarasi ambao wanadhani hawatakamilisha ama kuchelewesha
kazi ya usambazaji wa umeme vijijini kutokana na changamoto mbalimbali , ni
vyema kazi hizo wakapatiwa wakandarasi wenye uwezo ili miradi hiyo ikamilike
kwa wkati.
Akizungumzia kazi ya kusambaza umeme
vijijini katika maeneo aliyotembelea, Julai 16,2019, Mgalu alisema kuwa kuna
baadhi ya wakandarasi wamekuwa hawaendani na kasi inayotakiwa katika kutekeleza
mradi huo, na kwamba wamekuwa na sababu nyingi za kujitetea licha ya awali
kuonyesha kuwa na uwezo wa kufanya kazi hizo.
Aliweka bayana kuwa kasi ndogo ya
utekelezaji mradi huo ikilinganishwa na kipindi kilichowekwa kuukamilisha,
inaonyesha wazi kabisa kuwa wakandarasi hao hawatamaliza kazi hiyo kwa wakati
uliopangwa na hivyo kurudisha nyuma juhudi za serikali katika kutimiza malengo
yake ya kuwapatia umeme wananchi wote .
“Kuna wakandarasi ambao walianza
vizuri lakini sasa wanasuasua kutokana na changamoto mbalimbali, usikumbatie
kazi igawe kwa wenye uwezo, usisubiri jumba bovu likuangukie, Serikali wala
Wizara ya Nishati hatutakubali kurudishwa nyuma, ukishindwa ama kuchelewesha
sheria itachukuwa mkondo wake kwa kuwa fedha nyingi zimetengwa kwa ajili ya
kuwapatia wananchi umeme,”alisisitiza Mgalu.
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri Mgalu
aliwasha umeme katika baadhi ya nyumba za kijiji cha Itundaukulu pamoja na
Zahati ya kijiji hicho, pia katika shule ya msingi ya Simbo pamoja na kuwasha
umeme katika baadhi ya nyumba katika Kijiji cha Simbo wilayani Uyui, mkoani Tabora.
Aidha alikemea tabia ya baadhi ya
wakandarasi wanaondoka katika eneo la mradi mara baada ya kijiji husika
kuwashwa umeme, badala ya kubaki na kuendelea na kazi ya kuwaunganishia
wananchi wengine waliokwisha lipitia huduma hiyo, jambo ambalo limekuwa
likilalamikiwa sana na wananchi.
Aliwagiza viongozi wa Serikali za
mitaa na vijiji kuwa walinzi wa wakandarasi hao, na wahakikishe kazi ya
uunganishwaji wa wananchi inaendelea, na endapo mkandarasi atalazimika kuondoka
eneo la mradi, basi kuwepo na sababu maalum na watoe taarifa kwa uongozi wa
Vijiji.
“Nasikitishwa sana na baadhi ya
wakandarasi, wakiona umeme umeshawashwa katika kijiji na wao wanaondoka eneo
hilo, nawaeleza ukweli wakadarasi timizeni wajibu wenu kulingana na makubalino
ya mikataba na kutekeleza maagizo mbalimbali mnayopewa, tabia hii
hatutaivumilia, fanyeni kazi kwa mujibu wa mikataba muwatendee haki watanzania
na taifa kwa ujumla,” alisisitiza Mgalu.
Aidha amefafanua kuwa bei ya
kuwaunganishia wananchi umeme vijijini ni shilingi 27,000 tu, bei hii itandelea
kutumika hata pale Mradi wa REA utapokamilika na kazi hiyo wakapewa Shirika la
Umeme nchini (TANESCO) kuendelea na kazi hiyo, hivyo wanachi wote waendee
kuunganishwa lengo ni kuwafikia wananchi wote.
“Hapo awali ilikuwa ,mara baada ya
mradi wa REA kukamilika katika eneo husika kazi ya uunganishaji wananchi
inakabidhiwa kwa Tanesco, na bei ya kulipia gharama hiyo ilikuwa ni zaidi ya
170,000/=, sasa serikali imesema hapana bei ibaki ileile shilingi 27,000 kwa
wananchi wote wa vijijini,” alisema Mgalu.
Vilevile aliwatoa hofu wananchi kuwa,
mara baada ya mradi wa REA kukamilika, serikali imeanzisha mradi mwingine wa
ujazilizi ambao utakuwa ukiendelea na kazi ya kusambaza umeme kwa wananchi
ambao hawakuweza kufukiwa na REA, na mradi huyo utahusisha mikoa mbalimbali.
Naibu waziri wa Nishati, Subira Mgalu
akimkabidhi kifaa cha Umeme tayari (UMETA) kijana mwenye ulemavu wa Ngozi,
Mateso Juma, katika kijiji cha Ifucha Manispaa ya Tabora Mjini.
Serikali imeelekeza kuwa, UMETA licha
ya kugaiwa bure kwa wateja 250 wa mwanzo wanaounganishwa na Umeme wa REA,
kipaumbele kiwe ni kuwapa walemavu, wajane na wazee wasiojiweza na wenye zaidi
ya miaka 60.
Naibu waziri wa Nishati, Subira Mgalu, akiangalia Askrim na soda vikiwa baridi kutokana na kuhifadhiwa kwenye friji, hiyo ni baada ya kuwasha umeme katika vijiji vya mkoa wa Tabora.
No comments:
Post a Comment