Tuesday, July 2, 2019

RIPOTI YA CAG, HALMASHAURI YA BAGAMOYO YAPATA HATI SAFI.

Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo imefanikiwa kwa mara nyingine tena kupata hati safi (Unqualified Audit Opinion) kwa Mwaka wa fedha 2017/2018, ikiwa ni mara ya tatu mfululizo kwa Halmashauri ya Bagamoyo kupata hati safi.


Hayo yamesemwa jana Julai 01,2019 na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali Mkoa wa Pwani Bi. Mwajuma Mohamedi alipokuwa anawasilisha taarifa ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani wa halmashauri ya Bagamoyo.


Bi. Mwajuma amelieleza baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kuwa, kwa mujibu wa Katiba ya mwaka 1977 (Rev 2005) ibara ya 143 na sheria ya ukaguzi wa umma namba 11 ya 2918 kifungu cha 10 (1) ni jukumu la la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kufanya ukaguzi wa taarifa za mapato na matumizi ya fedha za umma Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Idara na mashirika ya umma.


Aliongeza kuwa, baada ya ukaguzi huo anatakiwa kutoa matokeo ya ukaguzi na mapendekezo kutokana na ukaguzi huo na hatua zinazotakiwa kuchukuliwa na menejimenti zilizopo kwa mujibu wa sheria.


Zaidi Bi. Mwajuma alisema, "Katika ukaguzi uliofanyika kwa mwaka wa fedha 2017/2018, Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo imepata hati safi na kufanya halmashauri hiyo kuendelea kupata hati safi kwa miaka mitatu mfululizo, kwani kwa Mwaka 2017/2018, mwaka 2016/2017 na mwaka 2015/2016 Bagamoyo imepata hati safi ya Mkaguzi na mdhibiti Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG)”.


Nae Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Bi. Theresia Mbando akizungumza katika mkutano huo maalum wa baraza la Madiwani amesema, ni jambo la kujivunia kwa Halmashauri na Mkoa wa Pwani kwa Bagamoyo kupata hati safi kwa miaka mitatu mfululizo, na kusisitiza kwamba maelekezo na mapendekezo yaliyotolewa na Mkaaguzi na mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) katika ripoti yake iliyowasilishwa katika mkutano huo, yafanyiwe kazi ili kuondoa kasoro ndogondogo zilizoonekana kipindi ukaguzi ulipofanyika, ili Halmashauri iendelee kupata hati safi miaka ijayo.


Bi. Theresia Mmbando pia ametumia nafasi hiyo, kuwaasa Madiwani na Wataalam wa Halamshauri kuhakikisha wanasimamia vyema ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri na kuongeza ubunifu katika kuanzisha vyanzo vipya vya mapato kwa kutilia mkazo uandishi wa maandiko ya miradi ya kimkakati inayofadhiliwa na Serikali kuu kwa sasa, itakayoisaidia Halmashauri kuongeza mapato yake ya ndani.





Akifunga Mkutano huo wa Baraza la madiwani, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Mhe. Said Ngatipura amesema, watahakikisha wanasimamia mapendekezo yote yaliyotolewa kwenye ripoti ya Mkaguzi na mdhibiti Mkuu wa Serikali na kusimamia ukusanyaji wa mapato ili kuhakikisha Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo inaendelea kufanya vizuri.
 
 Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali Mkoa wa Pwani Bi. Mwajuma Mohamedi akifuatilia Kikao maalum cha Baraza la madiwani wa Halmashauri ya Bagamoyo kwaajili ya kupokea taarifa ya mkaguzi wa hesabu za serikali.
  Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Bi. Theresia Mbando akizungumza katika mkutano huo.
 
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Mhe. Said Ngatipura akifunga mkutano huo.

No comments:

Post a Comment