Wednesday, July 31, 2019

NDALICHAKO ASAIDIA SHULE YA NYAMPAKU, RUFIJI.

Na Omary Mngindo, Muhoro

WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi Profesa Joyce Ndalichako, kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania TEA, ameipatia shule ya Msingi ya Kijiji cha Nyampaku sh. Mil. 60, kujenga vyumba vitatu vya madarasa shuleni hapo.


Shule hiyo iliyoko ndani ya Kata ya Muhoro wilaya ya Rufiji Mkoa wa Pwani, awali ilikuwa inakabiliwa na upungufu wa vyumba vya madarasa, hali iliyowalazimu wanafunzi kuingia darasani kwa zamu.


Akizungumza na Majira shuleni hapo, Mwalimu Mkuu Abdallah Simba alisema kuwa, mafanikio hayo yametokana na yeye kumwelezea Waziri Ndalichako, kuhusiana na changamoto hiyo, ambapo alimuunganisha na Mkurugenzi wa TEA ambaye ameiwezesha shule kupata kiasi hicho cha fedha.


"Waziri Ndalichako alifika nikamwelezea changamoto ya vyumba vya madarasa, akaniunganisha na Mkurugenzi wa TEA aliyetusaidia shilingi milioni 60 tulizojenga vyumba vitatu, tumekarabati darasa moja, tumechimba vyoo sanjali na kisima cha maji," alisema Mwalimu Simba.


Aliongeza kuwa awali shuleni hapo hali ilikuwa mbaya kutokana na kukabiliwa na changaamoto hiyo, ambayo baada ya kumwelezea Waziri huyo na kupatiwa fedha hizo walizojenga vyumba vitatu, kukarabati darasa moja, kujenga vyoo vya walimu sanjali na kuchimba kisima cha maji.


Mwalimu Mkuu Msaidizi Ziada Salumu alisema kuwa kwa sasa shule yao imeboreshwa, wanafunzi wanafurahia masomo ukilinganisha na hapo awali ambapo walikuwa wanaingia darasani kwa zamu kutokana na upungufu wa vyumba.


"Tunaiahukiru sana serikali yetu ya awamu ya tano kwa kutupatia fedha hizo ambazo zinetumika kikamilifu katika uboreshaji wa shule yetu, sasa hivi wanafunzi hawaji shule na maji, tunayo ya kutosha," aliasema Ziada.


Nae Selemani Omary alielezea furaha yake iliyotokana na mazingira yaliyopo hivi sasa shuleni hapo ikilinganishwa na hapo awali, huku akimshukuri Waziri Ndalichako.

No comments:

Post a Comment