Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akielezea kuhusu taaluma ya Uhasibu kuwa
nia muhimu katika maendeleo ya Viwanda na kutimiza ndoto ya
Serikali ya kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 wakati wa kuhitimisha
mkutano wa mwaka wa Wahasibu na kugawa tuzo ya taarifa bora ya fedha kwa washindi wa mwaka 2017, katika Kituo
cha Uhasibu na Ukaguzi eneo la Bunju, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
..........................................
Na, Peter Haule. WFM, Dar es Salaam
Wizara
ya Fedha na Mipango Fungu Hamsini (Vote 50) linalohusika na masuala ya utawala,
na Fungu ishirini na tatu (Vote 23) la Mhasibu Mkuu wa Serikali yamepata tuzo ya mshindi kwa nafasi ya pili na tatu katika utoaji wa Taarifa
bora ya fedha kwa mwaka 2017 katika kundi la Wizara na Idara za Serikali
inayoandaliwa na Bodi ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA).
Tuzo hizo zimetolewa kwa washindi na Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, katika Kituo cha Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu
kilichopo Bunju, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam baada ya kumalizika kwa
Mkutano wa mwaka wa Wahasibu nchini uliofanyika katika eneo hilo.
Dkt.
Kijaji alisema kuwa, taaluma ya Uhasibu inamchango mkubwa katika kukuza uchumi
wa viwanda na kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025 kwa kuwa Wahasibu na Wakaguzi
wa Hesabu wanahusika moja kwa moja katika suala la utawala na uongozi kupitia
mipango, kudhibiti matumizi ya fedha za Serikali na pia kuweka mazingira bora
ya uwekezaji kuelekea katika maendeleo ya uchumi wa viwanda hivyo kuwa na
tija katika agenda hiyo ya Taifa.
“Ni
wazi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe Rais Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli, inafanya kazi kwa bidii kuhakikisha Tanzania inakua na uchumi
wa kati ifikapo 2025, jambo hili haliwezi kufikiwa na Serikali pekee bali kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali ambao wanaweza kutumia taaluma yao na
kuishauri Serikali kwa njia mbalimbali, ikiwemo mijadala inayotokana na
mikutano ya mwaka ya wahasibu na wakaguzi wa hesabu”, alieleza Dkt. Kijaji.
Alisema
kuwa, ni vema Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu kuhakikisha wanaandaa taarifa
sahihi na kwa wakati kuhusu maendeleo ya viwanda ili wawekezaji wasipotoshwe
kuhusu uhalisia wa maendeleo ya Sekta hiyo, kwa kuwa taarifa za fedha
huwasaidia walipa kodi, wawekezaji na wadau wengine kufanya maamuzi.
Aidha
alisema kuw,a Serikali inaendelea kupambana na wararushwa na watumiaji wabaya
wa fedha za umma, kwa kuwa bado wapo Wahasibu ambao sio waaminifu ambao
wanacheza na hesabu kupitia taaluma hiyo kupotosha ukweli, alisema kipindi cha
kufanya mambo hayo kimepita na yeyote anayeendelea na tabia hiyo awe na uhakika
hatabaki salama kama hata badilika.
Alibainisha
kuwa suala la maadili ni muhimu sana
kwa wahasibu kwa kuwa wao wanaweza kufanya Serikali ikapata mapato au kupoteza
na kufanya ndoto za kuwa na uchumi wa viwanda kufikiwa au la
Hata
hivyo kufikiwa kwa uchumi wa Viwanda kunategemea uimara wa Sekta ya Umma na
Binafsi kwa kuwa wote wanajukumu la msingi la kufikia maendeleo hayo kwa kuwa
na taarifa za soko, taarifa za kihasibu na kutafuta suluhisho kwa masoko ya
fedha.
Naibu
Waziri huyo amefurahishwa na kuongezeka kila mwaka kwa idadi ya washiriki
katika ushindani wa taarifa bora ya fedha kutoka Sekta binafsi na umma, hasa
Mamlaka ya Serikali za Mitaa na Taasisi za Serikali, kwa kuwa ni hatua kubwa
kuelekea katika uwajibikaji na uwazi katika Sekta ya umma na kuongeza imani ya
wananchi katika utendaji wa sekta hiyo.
Naibu
Waziri Kijaji, amewapongeza washindi wote kwa juhudi walizozifanya na kuwataka
waendelee kufanya hivyo kwa manufaa yao
na Taifa kwa ujumla. Aidha amewapongeza wahasibu kwa kuamua kukaa pamoja na
kujadili taaluma ya uhasibu katika maendeleo ya Sekta mbalimbali ikiwemo ya
viwanda ambayo ni ajenda ya kipaumbele kwa Serikali ya awamu ya tano.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA), CPA. Pius Maneno, alisema kuwa tuzo zinazotolewa na NBAA zinalengo la kuhamasisha uwajibikaji na kuandaa taarifa ya fedha
zilizo na viwango vya kitaifa na kimataifa.
Alisema
kuwa washindi wa tuzo hizo wanapatikana
kupitia mchakato uliosheheni weledi wa hali ya juu kutoka kwa wabobezi wa
taaluma ya uhasibu nchini ambao wanaangalia vigezo kadhaa vikiwemo taasisi
kusajiliwa nchini, kuwasilisha hesabu kwa wakati na pia kufikisha kiwango cha
ubora wa taarifa kuanzia asilimia 75.
Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Fungu
50, Bw. Christopher Nkupama na Mhasibu Mkuu wa Serikali Msaidizi Fungu
23, Bw. Aziz Kifile, walisema kuwa tuzo hizo walizopata zinawapa morali ya
kufanyakazi kwa umahili zaidi na kuwapongeza watumishi walioko katika idara
hizo kwa kufanyakazi kubwa na bila kuchoka kuhakikisha kuwa wanazingatia
kanuni na taratibu za uhasibu wanapotekeleza majukumu yao.
Mshindi
wa Jumla katika tuzo hizo kwa taarifa
bora ya fedha kwa mwaka 2017 ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Tanga
Cement Plc na kwa upande wa Wizara na Idara za Serikali ni Tume ya
Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya
Washiriki
wa Tuzo hizo ni pamoja na
Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Wakala wa Serikali, Wizara na Idara za Serikali
na Sekta Binafsi.
Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akimkabidhi tuzo ya
taarifa bora ya fedha kwa mwaka 2017 Mhasibu Mkuu wa Serikali
Msaidizi Fungu 23, Bw. Aziz Kifile, katika Kituo cha Uhasibu na Ukaguzi eneo la Bunju, nje kidogo ya
Jiji la Dar es Salaam.
Mhasibu
Mkuu wa Serikali, CPA. Francis Mwakapalila (katikati), Mhasibu Mkuu wa
Fungu 50 Bw. Christopher Nkupama (wa pili kushoto), Mhasibu Mkuu wa Serikali
Msaidizi Fungu 23, Bw. Aziz Kifile, na maafisa wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha na Mipango wakiwa na
furaha baada ya kupokea tuzo ya taarifa bora ya fedha kwa mwaka 2017
iliyotolewa na Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA) eneo la Bunju, Nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Washindi
wa wa makundi mbalimbali ya Tuzo ya taarifa bora ya fedha kwa mwaka 2017 zinazotolewa na Bodi ya
Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA) wakiwa katika picha ya pamoja na Meza kuu baada ya
kukabidhiwa tuzo hizo eneo la Bunju,
nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
(Picha na Peter Haule- Wizara ya Fedha na Mipango)
No comments:
Post a Comment