Monday, December 31, 2018

ASKOFU KANISA KATOLIKI ZANZIBAR AITAKA JAMII KUWALEA WATOTO KATIKA MAADILI MEMA

Na Masanja Mabula -PEMBA

 ASKOFU wa kanisa katoliki Zanzibar Agustino Shao ameitaka jamii kuwalea watoto katika maadili mema , na kuhakikisha wanawalinda na vikundi viovu ili kuwafanya wawe nashuhuda wa ukweli.

Amesema ni jukumu la kila mzazi na mlezi kuhakikisha mtoto wake anaishi kwa hofu ya mungu kwa kufuata mafundisho ya dini.

 Askofu shao, ameyasema hayo wakati akizungumza na watoto wa haki na amani katika maadhimisho ya kumbukumbu ya watoto mashahidi iliyofanyika kitaifa  katika kanisa kuu wete pemba.

Amesema wazazi wanajukumu la kumtayarisha mtoto kuweza kutambua leo yake paamoja na kesho yake, pamoja na kuwapatia elimu ambayo ndio mkombozi wao.

“Kila mzazi analojukumu la kuhakikisha mtoto wake anapata malezi bora ambayo yatamsaidia kuishi kwa hofu ya Mungu na kujiepusha na makundi maovu ”alifahamisha.

 Aidha amelaani tabia ya baadhi ya wazazi ya kuwakosesha haki ya elimu watoto wa kike , na kusema wote wanahaki ya kupata elimu.
Amesema mipango ya Mungu iko juu kuliko ya mwanadamu , na kuitaka jamii kumtegemea Mungu katika kazi zao za kila siku.

Kwa upande wao walezi wa watoto wa haki na amani akiwemo Frola Vicent John kutoka Pemba na Jenister Mvula kutoka Unguja wamesema changamoto kubwa inayowakabili ni wazazi kutokuwa na mwamko wa kuwaruhusu watoto kushiriki utume.

Wamesema pamoja na juhudi wanazochukuwa kuwafuatilia watoto, lakini bado baadhi ya wazazi wanaonekana kuwa ni kikwazo katika kuwahimiza watoto kushiriki mafundisho.

“Tunapa changamoto kutoka kwa wazazi kwani baadhi yao wanakwamisha  mipango yetu kwa kutowahimiza watoto wao kushiriki mafundisho “alisema Frola.

Watoto wa haki na amani Judith Damian Modest na Mikael Costa Gerevas wameitaka kuwalinda watoto dhidi ya matendo ya udhalilishaji ili waishi kwa amani na upendo.

Mikael ameiomba serikali kuwachukulia hatua wanahusika na vitendo vya kuwabaka watoto wadogo, ili kuwalinda na kuwafaanya watoto waishi kwa amani na upendo kutoka kwa wazazi wao.

Maadhimisho hayo ya kumbukumbu ya watoto mashahidi , zaidi ya watoto mia moja na ishirini kutoka Unguja na Pemba wameshiriki.

No comments:

Post a Comment