NA MWAMVUA MWINYI,
KISARAWE
MBUNGE wa viti maalum
mkoani Pwani, Zainab Vullu ametoa msaada wa mapazia mazito yanayotumika
kusaidia kuweka usiri kwa akinamama wanaokwenda kujifungua katika wodi ya uzazi
hospital ya wilaya ya Kisarawe.
Msaada huo unaelezwa
kuwaondolea kero waliyokuwa wakiipata akinamama hao kipindi cha nyuma ambapo
walikuwa wakikataa kujifungua hospitalini hapo kwa kuhofia kukosa faragha
wakati wa kujifungua.
Mbali ya msaada huo pia
ametoa mifuko 80 ya saruji kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya
,zahanati na shule vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya sh.milioni mbili.
Akitoa msaada huo ,Zainab
alieleza kipindi cha nyuma akinamama wanaojifungua walikuwa wanakaa sehemu
ambayo haijazibwa jambo ambalo limemsukuma kujitolea mapazia hayo.
“Faragha inaanza tangu
pale anapoanza kutafutwa mtoto hadi anapozaliwa lazima usiri uwepo,” alifafanua
Zainab.
Nae mkuu wa wilaya ya
Kisarawe ,Jokate Mwegelo alimshukuru mbunge huyo na kudai suala la ukosefu wa
mapazia hayo ilikuwa ni changamoto kwa akinamama wanaojifungua.
Mwenyekiti wa halmashauri
hiyo, Hamis Dikupatile alisema, serikali imekuwa ikijitahidi kuboresha
mazingira ya kutolea huduma lakini bado jitihada zinapaswa kufanywa na kila
mmoja.
Mganga mkuu wa halmashauri
ya Kisarawe, Jonathan Budenu alibainisha kutokana na changamoto hiyo
baadhi ya akinamama walikuwa wakikataa kujifungulia hapo kutokana na hali hiyo.
No comments:
Post a Comment