Sunday, December 9, 2018

WAZIRI MKUU AFURAHISHWA NA UWEKEZAJI WA VIWANDA CHALINZE


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa afurahishwa na uwekezaji wa viwanda katika halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, kwa kutembelea na kukagua viwanda vikubwa viwili katika ziara aliyoifanya Jana katika halmashauri hiyo.

Mheshimiwa Majaliwa ametembelea kiwanda cha kuzalisha vigae cha Twyford kilichoko katika kitongoji cha Pingo katika mamlaka ya mji mdogo wa Chalinze na kujionea shughuli za uzalishaji katika kiwanda hicho,ambacho ni kiwanda kinachozalisha vigae bora katika afrika mashariki na kinauza ndani na nje ya nchi.

Aidha Waziri Mkuu alitembelea pia kiwanda cha kutengeneza bidhaa zinazotokana na matunda cha Sayona Fruits Ltd kilichopo katika kijiji cha Mboga, kiwanda ambacho kinamilikiwa na mwenyekiti wa wamiliki wa viwanda Tanzania Subashi Patel, ni kiwanda kikubwa katika afrika mashariki chenye mitambo ya kisasa na kinachonunua matunda kwa wingi kama malighafi ya kuendesha kiwanda hicho.

Mheshimiwa Majaliwa alikagua na kuona uzalishaji wa vinywaji mbalimbali na kuona jinsi watanzania wanavyonufaika na ajira kiwandani hapo.

Mheshimiwa Majaliwa katika hotuba yake kiwandani hapo alimpongeza mwekezaji wa kiwanda hicho Subashi Pateli kwa uwekezaji wenye tija unaotoa huduma za jamii, kuzalisha ajira kwa watanzania lakini pia kutoa kodi ya serikali kuu na halmashauri ya wilaya kwa maendeleo ya nchi na kuwataka wawekezaji wengine wawekeze kwa tija ili kutekeleza kwa vitendo Ilani ya Chama cha Mapinduzi kama ilivyonadiwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli.

" Katika kipengele cha viwanda kama kilivyotajwa kwenye Ilani kazi yetu ni kuweka vema kwani kimetekelezwa na muda wa uchaguzi utakapofika ni kuwauliza watanzania mnataka tufanye kitu gani kingine ." Waziri Mkuu alisema.

Majaliwa aliendelea kutoa wito kwa wanachalinze kulima matunda ambayo soko lake sasa linapatikana hapa kiwandani na kuwahamasisha kuleta matunda hayo kwani soko ni la uhakika na pasipo matunda uzalishaji haupo, akawataka wananchi kwa ujumla kuwalinda wawekezaji kwa udi na uvumba ili waweze kuzalisha kwa tija na kwa amani na utulivu kwani pasipo amani hakuna uzalishaji utakaofanyika hivyo aliwataka wananchi kwa ujumla kuwalinda wawekezaji popote pale nchini Tanzania ili uzalishaji ukafanyike kwa amani na wawekezaji wasikate tamaa kwa kutokuwa na amani katika maeneo waliyowekeza

Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo kwa niaba ya wananchi wa mkoa wa Pwani alitoa wito kwa wawekezaji wanaotaka kuja kuwekeza mkoani Pwani wanakaribishwa Pwani ni salama,mazingira ni rafiki kwa uwekezaji na amani ni ya kutosha," Tunayo ardhi ya kutosha kwa uwekezaji wa aina yoyote karibuni Pwani ya Viwanda." Ndikilo alisema.
 

No comments:

Post a Comment