NA MWAMVUA MWINYI,
PWANI
MKUU wa mkoa wa Pwani,
mhandisi Evarist Ndikilo amewaagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa
halmashauri kuhakikisha wanajenga madarasa 122 na matundu ya vyoo ili wanafunzi
4,731 waliobaki kujiunga kidato cha kwanza waweze kuanza masomo ,ifikapo
January 30 mwaka 2019.
Aidha amewaelekeza
,kufuatilia shule za msingi kumi zilizofanya vibaya kimkoa na kuhakikisha
wanachukua hatua mahsusi .
Pamoja na hayo, Ndikilo
amekemea walimu wavivu na kuwataka wafanye kazi kwa molari ili kuinua ufaulu na
taaluma kwa wanafunzi.
Akitoa maagizo katika
kikao cha kamati ya uchaguzi wa wanafunzi waliofaulu kidato cha kwanza mkoani
hapo, alieleza wanafunzi 4,731 hawatapata nafasi hivyo watasubiri hadi ujenzi
ukamilike awamu ya II.
Alisema, endapo halmashauri
zingekamilisha wajibu wake wa kujenga majengo ya madarasa hali hiyo
isingetokea.
Mkuu huyo wa mkoa alitaja
takwimu kihalmashauri ambapo wanafunzi 487 halmashauri ya Bagamoyo hawana
nafasi, Chalinze 103, Kibaha Vijijini 285,Kibaha Mjini 711 na Kibiti 537 .
Ndikilo alitaja
halmashauri ya Kisarawe wanafunzi 324,Mkuranga 1,071 na Rufiji 213 .
“Halmashauri zote
zilizobakiza wanafunzi zijipange, mjiwekee mkakati kuondoa tatizo hili ili
watoto waweze kwenda shule “Watumieni wadau wa elimu na wawekezaji kushirikiana
kwenye hili “alisisitiza Ndikilo.
Ofisa elimu mkoani Pwani,
Abdul Maulid, aliahidi kutekeleza maagizo waliyopewa na mkuu huyo wa mkoa kwani
zipo wilaya ambazo zinaendelea na zoezi la kukamilisha ujenzi huo.
Alisema, kwa mwaka 2018
mkoa wa Pwani umepanda na kushika nafasi ya 11 kitaifa ukilinganisha na 2017
ambapo ilishika nafasi ya 19 kitaifa.
No comments:
Post a Comment