Thursday, December 6, 2018

HATUNA CHA KUMLIPA JPM -WAKULIMA WA KOROSHO KIBAHA

WAKULIMA wa zao la korosho wilayani Kibaha mkoani Pwani .
........................................................
NA MWAMVUA MWINYI, KIBAHA 

WAKULIMA wa zao la korosho wilayani Kibaha mkoani Pwani ,wamesema maamuzi ya serikali chini ya Rais Dk John Magufuli kununua korosho ni mkombozi kwao. 

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mwenyekiti wa umoja wa vyama vya ushirika wa zao la korosho wilaya ya Kibaha (UVUKI) Adhu Mkomambo alisema ,hatua hiyo itasaidia kuondoa ubabaishaji wa malipo uliokuwepo kipindi cha nyuma. 

Alifafanua,  maamuzi hayo ni faida kubwa kwa wakulima kwani bei elekezi ni nzuri ya shilingi 3,300 kwa daraja la kwanza ambapo wafanyabiashara walisema watanunua kwa shilingi 2,700 hali ambayo ilikuwa ni mbaya.

“Manufaa ya maamuzi haya ni kunufaisha wakulima ambao wamekuwa wakitaabika kwa muda mrefu ambapo wafanyabiashara walikuwa wanaangalia maslahi yao binafsi,” 
“Hatuna cha kumlipa mh Rais, ila tunamuombea azidi kutetea wanyonge “alisema Mkomambo.

Nae mwenyekiti wa chama cha ushirika Kongowe Amcos Deo Joseph alisema, maamuzi hayo yataondoa usumbufu mkubwa waliokuwa wanapata wakulima katika malipo Mara wanapopeleka korosho kwenye minada.

Mzee Mwinshehe ambaye ni mwenyekiti wa chama cha ushirika Misugusugu Amcos alieleza, wakulima tegemeo lao ni korosho hivyo kuwalipa fedha ndogo ni kuwakwamisha kimaisha kwani wanategemea zao hilo kusomesha na shughuli nyingine za maendeleo na bei elekezi itapunguza gharama za pembejeo.

No comments:

Post a Comment