Friday, December 14, 2018

VULU AKABIDHI VIFAA VYA MIL. 4.5. WANACCM WAPEWA SEMINA ELEKEZI

Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Pwani, Zainabu Vulu, akikabidhi mifuko 60 ya saruji kwa Diwani wa Utete, Hawa Mchopa 
.....................................

Na Omary Mngindo, Kibiti
 
MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani Zaynab Matiti Vulu, amefanya ziara katika majimbo ya Kibiti na Rufuji mkoani hapa, ambapo amekabidhi vifaa mbalimbali vilivyogharimu sh. Milioni 4.5

Katika ziara hiyo iliyoanza juzi, Vulu akiwa Jimbo la Kibiti alipokelewa na Mbunge wa Jimbo hilo Ally Ungando, aliyeambatana na Diwani mwenyeji Hamidu Ungando na viongozi mbalimbali ambapo baada ya mapokezi alifika shule ya msingi Zimbwini na kukabidhi bati 20 yenye thamani ya sh. Laki 540.

Akizungumza shuleni hapo, Vulu alianza kuwashukuru wananchi hao kwa mwamko wa kujitolea katika kujiletea maendeleo, serikali, wabunge, madiwani pamoja na wadau mbalimbali wanaoendelea kujitoa katika sekta mbalimbali.

"Nami nikiwa mdau wa maendeleo nakabidhi mabati 20 yenye thamani ya shilingi 540,000, pia nitakwenda kukabidhi mapazia maalumu ya kuzunguka kitanda cha mama anayejifungua, pamoja na gharama za mabomba na ufundi zinagharimu sh. milioni mbili hamsini na nane elfu," alisema Vulu. 

Akizungumza baada ya kupokea mabati hayo, Diwani Ungando alimshukuru Vulu kwa msaada huo, huku akisema kuwa umefika wakati mwafaka kwani tayari darasa lililoongezwa limeshakamilika na kwamba kilichobaki na kupauliwa kisha kupigwa bati. 

Viongozi wengine ngazi ya Kata walioongozana na Vulu ni pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Khatibu Chaurembo, Amina Mapande, Moza Kiluya, Zaynab Chitanda diwani Ungando ambao kwa umoja wao wameahidi bati 25.

Vulu akiwa Jimbo la Rufiji amekabidhi mifuko 60 ya saruji isiyogawanyika katika miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa shule ya msingi katika Kitongoji cha Kiwili Kata ya Utete ambapo alishiriki zoezi la ufyatuaji wa tofari. 

Mbali ya mifuko hiyo pia amenunua lori za mchanga ambazo zote gharama yake vimegharimu milioni 2,442,000 ambapo akiwa katika Kitongoji hicho akishirikiana na viongozi wa chama pamoja na wananchi walishirikiana na kusafisha eneo kisha kufyatua tofari.

Hawa Mchopa diwani Kata ya Utete alimshukuru mbunge huyo huku akisema amekuwa bega kwa bega na wananchi wake katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo. 
  
Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Pwani, Zainabu Vulu, akibeba moja ya tofali katika eneo linalotarajiwa kujengwa shule ya msingi.

 
Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Pwani, Zainabu Vulu, akilima eneo la ujenzi kabla ya kuanza kufyatua tofali kwaajili ya ujenzi wa shule ya msingi.

No comments:

Post a Comment