Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George
Mkuchika (Mb), akizungumza na washiriki wa mjadala kwenye maadhimisho ya Siku
ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa, kabla ya kumkaribisha Jaji Mkuu Mstaafu
wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman kufungua rasmi mjadala huo jijini
Dodoma.
....................................
Viongozi, watumishi na wataalam mbalimbali nchini,
wametakiwa kujiepusha na mgongano wa maslahi kwa kutotumia nyadhifa zao au
ofisi zao kujinufaisha wao wenyewe, kuwanufaisha ndugu zao au jamaa zao na watu
wengine ili waweze kutekeleza wajibu wao ipasavyo katika ujenzi wa uchumi imara
wa taifa.
Wito huo umetolewa na Jaji Mkuu Mstaafu wa
Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman wakati akifungua mjadala kwenye
maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa, jijini Dodoma.
Mhe. Othman amesema, mgongano ya maslahi ni lazima
udhibitiwe kwa nguvu zote kwani unailetea sifa mbaya serikali, taasisi, idara
na sekta binafsi ambazo mgongano wa maslahi unajitokeza, na kuongeza kuwa
unamletea pia sifa mbaya ya kiutendaji kiongozi au mtumishi kwenye fani au
taaluma aliyobobea.
Mhe. Othman ameainisha njia za kuweza kuepukana na
mgongano wa maslahi, njia hizo ni kujiuzulu au kujitoa endapo kiongozi anaona
kuna maslahi binafsi kwenye jambo atakalolitolea maamuzi kwa ajili ya kulinda
maslahi ya umma.
Mhe. Othman amesisitiza kuwa, ni jukumu la
mtendaji mwenyewe kutamka mapema, kukiri kwa hiari na kwa uwazi kwamba ana
mgongano wa maslahi kwenye suala atakaloenda kulitolea maamuzi badala ya
kungoja kuambiwa ajiuzulu na kushutumiwa kuwa na mgongano wa maslahi kwenye
suala aliloshiriki kutoa maamuzi.
Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika amesema,
moja kati ya mambo ambayo ofisi yake inapambana nayo ni kuhakikisha inaondoa
uwezekano wa kuwepo kwa mgongano wa maslahi katika taasisi za umma.
Mhe. Mkuchika amefafanua kuwa, kiongozi au
mtumishi yeyote katika sekta ya umma hatakiwi kufanya biashara na taasisi yake
kwasababu kuna uwezekano mkubwa wa kupendelea kampuni yake kuipatia zabuni na
kuiongezea malipo ili aweze kujinufaisha na hatimaye kuitia hasara serikali.
Aidha, Mhe. Mkuchika ametoa wito kwa washiriki wa
mjadala kuhakikisha wanatoa maoni na mapendekezo ambayo yataondoa changamoto ya
mgongano wa maslahi katika sekta ya umma.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa
(Mb) amesema, viongozi na watumishi ambao wanasimamia maadili wanapaswa
kuyaisha yale wanayoyasema, na ni muhimu pia ni wajibu wao kuonyesha njia katika
uzingatiaji wa maadili ili wanapohubiri maadili mema wawe na ushawishi kwa
umma.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa ameongeza kuwa, vitendo vya
mmomonyoko wa maadili vinatakiwa kukemewa bila kusita wala kuonewa haya kuanzia
kwenye ngazi ya familia ili kujenga taifa lenye uadilifu.
Mada zilizojadiliwa katika mjadala huo ni pamoja
na, Mgongano wa masilahi katika utumishi wa umma, Ulinzi wa haki za binadamu na
mgongano wa maslahi na matumizi mabaya ya madaraka yanayopelekea mgongano wa
maslahi na uwepo wa rushwa nchini.
No comments:
Post a Comment