Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani
Jafo(kushoto) akimkabdihi cheti cha kuhitimu na kufaulu mafunzo ya Uongozi Mkuu
wa Mkoa wa Ruvuma Mhe.Christina Mndeme wakati
wa kufunga mafunzo ya Uongozi.
....................................
Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo ameinyooshea kidole Halmashauri ya Wilaya
ya Nyasa kwa hali inayoendelea ya kusuasua kwa Ujenzi wa Vituo vya Afya.
Kutokana na hali hiyo Waziri Jafo amemuagiza Naibu
Katibu Mkuu anayeshugulikia Afya Bi. Zainabu Chaula kufuatilia Halmashauri hiyo
na kufahamu kwa kina sababu zilizopekea kushindwa kutekeleza ujenzi wa Vituo
vya Afya kama walivyoelekezwa.
Waziri Jafo ameyasema hayo wakati wa kufunga
mafunzo ya Uongozi kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala yaliyofanyika
kwa siku Tano katika Ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma.
Mhe. Jafo alisema Fedha za Ujenzi wa Vituo
zina miongozo na taratibu zake na kuna muda maalumu wa utekelezaji wa miradi
hiyo sasa inakuwaje Halmashauri imekwishapata Fedha halafu hakuna utekekezaji
nini kinakwamisha ilihali fedha ipo tayari kwenye akaunti ya Halmashauri husika
“Pale Nyasa kuna tatizo na nataka kufahamu kwa
kina sababu zilizosababisha kukwama kwa ujenzi wa kituo cha Afya Timu ya
Wataalamu iende huko mara moja ili tuweze kuchukua hatua stahili na kituo cha
Afya kijengwa wananchi wapate huduma za Afya”
Aliongeza kuwa Wakuu wa Mikoa mambo haya
yanatendeka katika maeneo yenu ya utawala ukiwa kama
msimamizi wa shughuli zote za Serikali mnapaswa kufahamu na kuchukua hatua za
stahiki na kuhakikisha malengo ya Wizara yanafikiwa.
‘Tusikubali mtu au kundi la watu likarudisha nyuma
jitihada zetu za kumletea mtanzania maendeleo, Serikali imetoa fedha nyingi sana kwa ajili ya mwananchi
tuzilinde fedha hizo na tusimamje miradi itekelezwe kwa kiwango’ alisema Jafo.
Awali akifunga mafunzo hayo Waziri Jafo
aliwapongeza viongozi hao kwa ukomavu wa kiuongozi waliouonyesha wakati wote wa
Mafunzo na kuwataka kufanyia kazi elimu waliyoipata na kuleta
mabadiliko chanya na ya haraka katika jamii wanayoiongoza.
Aidha aliwataka kuongeza Wakuu hao wa Mikoa na
Makatibu Tawala kuongeza umakini katika usimamizi wa miradi ya maendeleo
inayotekelezwa katika maeneo yao
ili thamani ya fedha iweze kuonekana.
Akitoa taarifa ya awali Mtendaji Mkuu wa Taasisi
ya Uongozi Prof. Joseph Semboja alisema kuwa viongozi hao wameonyesha kuelewa
vizuri mada zote walizofundishwa na wametoa ushirikiano wa hali ya juu
wakati wakati wote wa mafunzo hayo.
Somo kubwa walilopewa viongozi wetu ni namna ya
kuwa kiongozi wa kimkakati, kusimamia rasilimali watu na kuitumia
ipasavyo na namna nzuri ya kujijengea sifa binafsi alisema Pro. Semboja.
Makundi muhimu ya viongozi wa Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa yamekwishapata mafunzo haya kwani yalianza kutolewa kwa
Wakurugenzi wa halmashauri zote Nchini, Wakuu wa Wilaya na kwa kumalizia na
Makatibu Tawala Mikoa pamoja na Wakuu wa Mikoa.
No comments:
Post a Comment