Saturday, December 15, 2018

WANA CCM MSOGA WAPIGWA MSASA

Na Omary Mngindo, Msoga

WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Msoga, Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, wamepatiwa semina elekezi iliyoandaliwa na uongozi wao, ikiendeshwa na chama hicho ngazi ya Wilaya

Semina hiyo iliyofanyika Kijiji cha Mboga, inaendeshwa na Katibu wa chama hicho Wilaya Kamote Kombo, Katibu Mwenezi Fransis Bolizozo, Kufulu Rashidi Katibu Kata ya Kiwangwa wakiongozwa na viongozi wa Kata chini ya Diwani wao Jamdani Mwinyikondo na viongozi mbalimbali.

Akitoa mada katika semina hiyo, Bolizozo alisema kuwa lengo la semina ni kuwakumbusha wanachama hao kutambua majukumu yao, huku wakitambua kwamba wanaelekea kwenye chaguzi ngazi za Vijiji, Vitongoji na Mitaa zinazotaraji kufanyika mapema mwakani. 

"Chama ngazi ya wilaya kimeamua kuandaa semina elekeza inayolenga kukumbushana majukumu yetu katika utendaji wa kazi zetu, tukumbuke tunaelekea katika chaguzi kuanzia mwakani tutambue majukumu yetu," alisema Bolizozo.

Kamote aliwaasa Wana-CCM hao kuendelea kuwatumikia wananchi, huku aliwajibu Wenyeviti kama wanakutana na wananchi wenye matatizo katika maeneo yao,  huku aliwahimiza kuwa na ratiba za kukutana na kutatua kero zinazowakabili wananchi. 

"Ni jambo jema kwa Wenyeviti kuwa na utaratibu wa kuwa na vikao katika maeneo yenu kwa lengo la kusikiliza kero zinazowakabili watu mnaowaongoza katika ngazi zenu, " alisema Kamote.

Diwani Mwinyikondo alisema kuwa viongozi ngazi hiyo wameweka mikakati maalumu inayolenga kuunda mkono juhudi za Rais Dkt. Joho Magufuli kuhakikisha wanyonge wanapewa kipaumbele katika kutatuliwa changamoto zinazowakabili. 

Mwenyekiti wa chama hicho ngazi ya Kata Idd Tungo aliwashukuru watendaji wa ngazi mbalimbali kwa kuwa karibu na chama hicho katika kuhakikisha wanasaidiana katika kupambana na changamoto zinazowakabili wananchi. 

No comments:

Post a Comment