WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali
imeanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania kwa lengo la kuwasaidia
wakulima wapate mitaji ili waongeze tija.
Pia amewataka wakuu wa wilaya za Kilosa na Mvomero
mkoani Morogoro wahahakikishe wanawahamasisha wananchi katika maeneo yao kuchangamkia fursa ya
kilimo cha miwa.
Waziri Mkuu aliyasema hayo jana jioni (Ijumaa,
Desemba 7, 2018) alipotembelea shama la miwa Mkulazi na MbIgiri mkoani Morogoro
alipokuwa njiani kwenda jijini Dodoma.
Alisema lengo la kuanzishwa shamba la mwa la
Mkulazi ni katika jitihada za Serikali za kuhakikisha mahitaji ya
sukari nchini yanafikikia katika kiwango kinachohitajika.
Waziri Mkuu alisema Serikali imepanga kuzalisha
sukari itakayotosheleza mahitaji na njia pekee ni kuboresha kilimo
cha miwa, kujenga viwanda vitakavyozalisha sukari ya kutosha.
Alisema shamba hilo linaendeshwa kwa ubia kati ya
NSSF na Jeshi la Magereza, hivyo, aliiagiza Menejimenti mpya ya Mkulazi
kuhakikisha shamba hilo
linasimamiwa kikamilifu.
Waziri Mkuu pia, alimuagiza Kamishna Jenerali wa
Magereza, Phaustine Kasike apeleke wataalamu wengi wa kilimo katika shamba hilo ili wasaidie
kusimamia kitaalamu.
“Nataka shamba hili lisimamiwe kitaalamu,
uzalishaji uwe wa kitaalamu na liwe mfano na mashamba mengine, tusishindwe na
watu binafsi,” alisema.
Kuhusu suala la maji hususan kipindi cha mvua
ambayo huaribu shamba, Waziri Mkuu aliwataka watafute namna nzuri ya
kuyahifadhi ili wayatumie kipindi cha kiangazi.
Kadhalika, Waziri Mkuu aliwataka watafute mashine
nyingine zitakazotosha kumwagilia shamba hilo
wakati wa kiangazi ili miwa isiharibike na iendelee kuwa ya kijani wakati wote.
Nae, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,
Bunge, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenistar Mhagama, alisema shamba la Mkulazi II
ni miongoni mwa mashamba mawili yanayomiilikiwa na wabia wawili yaani NSSF na
Jeshi la Magereza.
Alisema walikubaliana wao na Magereza wafanye kazi
kwa kuongozwa na uzalendo, maadili ya utendaji wa kazi, uaminifu ili mwisho wa
siku mradi huo uwe na tija na uweze kuwafikisha katika malengo yaliyokusudiwa.
Alisema wanaamini fedha zilizowekezwa kwenye mradi
huo ambazo ni za wanachama zinatakiwa zirudishe faida kwa wanachama wenyewe na
kujenga uchumi wa Taifa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, Omari
Mgumba, alimshukuru Rais Dkt. John Magufuli kwa dhamira yake ya dhati ya
kuhakikisha tatizo la upatikanaji wa sukari nchini linakuwa historia.
Alisema mbali ya shamba hilo la Mkulazi II pia
kuna lingine la Mkulazi I ambalo ni kubwa zaidi, hivyo alishauri liendelezwe
ili limalize tatizo la sukari nchini. Waziri Mkuu alimtaka ashughulikie shamba hilo kwa kuwa lipo Wizara
ya Kilimo.
No comments:
Post a Comment