Sunday, December 30, 2018

CHAHUA WAKUMBUKA HOFU YA RIDHIWANI KIKWETE KUHUSU MAJI

Wakazi wa kitongoji cha Chahua, kata ya Bwilingu Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wao mara baada ya zoezi la usafi la kila mwisho wa mwezi ambapo wakazi hao walijumuika kwenye Zahanati yao kwaajili zoezi hilo, Picha na Omary Mngindo.
 ..............................................................


Na Omary Mngindo, Chahua 


MWENYEKITI wa Kitongoji cha Chahua, Kata ya Bwilingu Halmashauri ya Chalinze mkoani Pwani Rashid Maisha, amekumbuka hofu iliyooneshwa na Mbunge wao Ridhiwani Kikwete, aliyeionesha wakati ikitolewa ahadi ya upatikanaji wa maji jimboni humo, ifikapo Des 31 mwaka huu.

Maisha ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki, akizungumza na mwandishi wa habari hizi muda mfupi mara baada ya kumalizika kwa zoezi la usafi wa mwishoni mwa mwezi, ambapo wakazi hao walijumuika kwenye jengo la Zahanati kwa ajili ya zoezi hilo.

Alisema kwamba, kwenye mkutano uliofanyika hivi karibuni mbele ya Makamu wa Rais Mama Samoa Suluu Hassani katika viwanja vya Polisi Bwilingu, Mtendaji Mkuu wa DAWASA lipotoa ahadi ya kupatikana kwa maji Des 31, Ridhiwani alionesha hofu ya kukamilika kwake, huku akimuomba Mtendaji huyo wafanye ziara ya kukagua namna ya utekelezwaji wa mradi unavyokwenda.

Alisema kwamba mradi huo mpaka sasa hauna matumaini ya kukamilika hivi karibu, ambapo wananchi wakiendelea kutaabika kupata huduma hiyo, huku matumaini ya kumalizika kwa adha hiyo yakigonga mwamba.

"Wakati Mbunge wetu Ridhiwani Kikwete akionesha hofu ya kukamilika kwa mradi, wengi wetu hatukumuelewa hiyo imetokana na ahadi hiyo kutolewa mbele ya Makamu wa Rais Mama Samia, lakini leo tumeamini, hofu yake imekuwa na mashiko, mradi hauna dalili za kukamilika leo wala kesho," alisema Maisha.

Kwa upande wao wakazi wakazi Mwanahamisi Lomano na Mariana Mtamani walielezea adha ya maji wanayokabiliana nayo huku wakisema kwamba mara ya mwisho kupata huduma hiyo ilikuwa mwezi wa Novemba na kuwa mpaka sasa hawana maji.

"Mpaka leo tuna mwezi mmoja hakuna maji, wananchi tunaendelea kuteseka kwa kutafuta maji kwenye malambo yasiyo safi na salama, hii kero si huku Chahua tu hata kwa wenzetu wa Chalinze pia wanakabiliwa na adha kama hii," alisema Lomano.

Mtamani aliiomba Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Chalinze (CHALIWASA) kuhakikisha wanaboresha upatikanaji wa huduma hiyo, ili wananchi waondokane na adha hiyo ya miaka kwa miaka.

No comments:

Post a Comment