Waziri wa Kilimo, Mhe.
Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akizungumza na Wenyeviti wa Bodi
za Mazao pamoja na Wakurugenzi wa Bodi hizo za Mazao, kwenye ukumbi wa Wakala
wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Jijini Dodoma jana tarehe 29 Disemba
2018
.......................................................
Waziriwa Kilimo, Mhe.
Japhet Hasunga (Mb) amewaagiza Wakurugenzi wa Bodi za Mazao kuanza mara moja zoezi la kuwatambua na kuwasajili
wakulima wa mazao yote nchini lengo likiwa kuwatambua ili kupanga mipango
sahihi yenye kuongeza tija na uzalishaji katika mazao yote.
Ametoa agizo hilo jana tarehe 29 Disemba 2018
wakati akizungumza na Wenyeviti wa Bodi za Mazao pamoja na Wakurugenzi wa Bodi hizo
za Mazao, kwenye ukumbi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Jijini
Dodoma.
Mhe. Hasunga amesema ili kuongeza tija na
uzalishaji katika Sekta ya kilimo na kuandaa mipango madhubuti ya kuendeleza
mazao yote ni vyema kuwatambua Wakulima wote nchini na kuongeza kuwa Wakulima wa
zao la korosho wametoa funzo kubwa kwa Wizara yake kufanya jambo kama
hili katika
mazao mengine hapa nchini.
Itakumbukwa kuwa wiki tatu zilizopita, Waziri Hasunga
alitoa agizo kwa Bodi ya Korosho agizo kuandaa daftali maalumu la kuwatambua
Wakulima wa korosho kote nchi ambapo moja ya taarifa ambazo zitajumuishwa katika daftali hilo ni pamoja na
Jina Kamili la Mkulima,
Mkoa, Wilaya, Kata
na Tarafa anayotoka.
Mambo mengine ni pamoja na Kitongoji, Mtaa au
Jina la Kijijini anapotoka, mahali lilipo shamba pamoja na ukubwa wa shamba
lake.
Waziri Hasunga ameongeza kuwa mipango sahihi ya
kuwaendeleza Wakulima kuanzia kwenye kilimo chenyewe hadi kufikia katika hatua
ya kuvuna, kuhifadhi na kulifikia soko ni vyema kuwa na mfumo maalumu wa
kanzi data (Database) ya kuwafahamu ili kushughulikia mahitaji yao kisasa na kwa haraka zaidi.
Waziri Hasunga alienda mbali na kushauri matumizi
ya TEHAMA na ya Mfumo wa GPS ili kuboresha daftari hilo kwa lengo la
kuboresha uwekaji wa taarifa za Wakulima na
maeneo wanayotoka Wakulima
kwa usahihi zaidi.
“Tumepata changamoto kadhaa wakati wa kuwahakiki
Wakulima wa korosho katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani na Ruvuma na kama Bodi
ya Korosho ingekuwa makini kuandaa daftari la Wakulima zoezi la uhakiki lingekuwa
rahisi, kwa ajili hiyo niliwaagiza Bodi ya Korosho kukamilisha zoezi hili mpaka Mwezi
Machi, 2019 na Bodi za Mazao zilizobaki ukiacha Bodi ya Tumbaku ambao wao tayari
walishafanya hivyo, kukamilisha
Mwezi June, 2019”. Amekaririwa Mhe. Hasunga.
Waziri ameitisha kikao maalumu na Viongozi wa Bodi
za Mazao, Wakala na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo kwa lengo la kuboresha
mikakati na kuongeza ufanisi katika utendaji wa Wizara pamoja na kujitathmini
kabla ya kufikia nusu mwaka wa utekelezaji wa vipaumbele vya bajeti ya Wizara ya mwaka
2018/2019 ili kujipanga kwa
ajili ya utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya kilimo ya mwaka ujao wa
2019/2020.
Bodi za Mazao zilizoshiriki mkutano huo ni
pamoja na Bodi ya Korosho, Bodi ya Pamba, Bodi ya Mkonge, Bodi ya Pareto, Bodi ya
Chai, Bodi ya Kahawa, Bodi ya Tumbaku, Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko na
Bodi ya Sukari.
Wakala zilizoshiriki ni pamoja na Wakala wa
Taifa wa Mbolea (ASA) Wakala
wa Wakulima Wadogo wa Chai (TSHTDA).
Taasisi nyengine za Wizara ya Kilimo zilizoshiriki
ni pamoja na Taasisi ya Udhibiti wa Mbegu (TOSCI), Shirika la Ukaguzi na
Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO), Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu vya Ukanda
wa Kitropiki (TPRI), Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (AGITF), Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula
(NFRA),
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea
(TFRA), Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI), Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Tume ya Taifa ya
Umwagiliaji, Kampuni ya Taifa ya Mbolea (TFC) na Bodi ya Leseni za Maghala.
Katibu Mkuu
wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe akifatilia mkutano
wa Wenyeviti wa Bodi za Mazao pamoja na Wakurugenzi wa Bodi hizo za
Mazao, uliongozwa na Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) kwenye
ukumbi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Jijini Dodoma jana
tarehe 29 Disemba 2018.
Wenyeviti wa Bodi za Mazao pamoja na Wakurugenzi wa Bodi hizo za Mazao, wakifatilia mkutano wa kazi ulioongozwa na Waziri wa Kilimo, Mhe. Japhet Hasunga (Mb) kwenye ukumbi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Jijini Dodoma jana tarehe 29 Disemba 2018.
(Picha
Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
No comments:
Post a Comment