Na
Omary Mngindo, Fukayosi
BUNGE
wa Jimbo la Bagamoyo Mkoa wa Pwani Dkt. Shukuru Kawambwa, amekubali kutoa gari
yake inayotumika kwa kazi za kiofisi, ili itumike kwa doria kwa wakazi waishio
kwenye Vitongoji vinavyopakana na Hifadhi ya Mbuga ya Saadani wilayani humo.
Hatua
hiyo imetokana na kuwepo kwa adha kubwa ya Tembo, ambao mara kadhaa wamekuwa
wakiingia kwenye mashamba ya wakulima hao na hufanya uharibifu mkubwa wa mazao
ya wananchi hao.
Dkt.
Kawambwa ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki katika Kitongoji cha Segwa, wakati
wa mkutano uliohusisha Maofisa wa Idara ya Misitu kutoka Kanda ya Mashariki
Makao Makuu jijini Dar es Salaam, waliofika kusikiliza changamoto zinazowakabili
wananchi hao.
Ahadi
ya Kawambwa imefuatia wazo jema lililotolewa na Abraham Jullu Ofisa Wanyamapori
Kikosi dhidi ya ujangili Kanda ya Mashariki kutoka Makao Makuu jijini Dar es
Salaam, ambaye alianza kuwapa pole wakazi hao kwa adha hiyo na kusema kuwa, kuna
Chuo Maalumu kinachotoa mafunzo kwa ajili ya wananchi kuwa na elimu ya
kudhibiti wanyama hao.
Kabla ya kauli ya mbunge huyo, Jullu alisema kuwa tatizo la Tembo lipo maeneo mengi hapa nchini, hivyo kutokana na changamoto hiyo kuwa kubwa, wana mpango wa kuwapatia elimu wananchi ya kukabiliana na wanyama hao, wakati askari wao wakiwa wanakwenda maeneo husika kwa msaada zaidi.
"Kama
mtakuwa tayari ofisi yetu itawapatia mafunzo ya muda mfupi yatakayosaidia
kuwapatia elimu ya kudhibiti wanyama hao, sisi tupo wachache eneo
tunalolifanyiakazi ni kubwa, hivyo wakati mnaathiriwa na Tembo mpaka tutoke Dar
es Salaam kuja huku athari inaweza ikawa kubwa zaidi," alisema Jullu.
Jullu
aliyeambatana na Maofisa wenzake Samsoni Saye na Hemed Matiko, pia
wamewahakikishia wakulima hao kwamba wapo nje ya Hifadhi ya Saadani, huku
akiwaambia kuwa wakipokea wazo hilo
watafika katikati ya wiki hii kwa ajili ya kuanza mafunzo hayo.
"Katika
kufanikisha hili changamoto itakuwa moja, ofisi yetu haina gari za kutosha,
zoezi tunakotaka kulifanya linahusika kutembelea maeneo ambayo Tembo huwa
anaonekana au kupita, kwa hiyo hatuwezi kutembea kwa miguu lazima ipatikane
gari," alisema Jullu.
Kikao
hicho kilichokuwa chini ya Mwenyekiti wa Kitongoji cha Segwa Abdi Amani na wa
Kijiji Shaabani Mkumbi,
Mtendaji
wa Kijiji Zahra Swalehe na Maofisa kutoka Bagamoyo, ndipo Dkt. Kawambwa akasema
kuwa gari yake inayotumika kwa shughuli za kiofisi itakuwa tayari kwa ajili ya
zoezi hilo.
"Gari
yangu ya ofisi ipo itakuja kwa ajili ya zoezi hilo la kuhakikisha mafunzo
yanafanyika, ili wananchi wetu waweze kupata elimu ya namna gani ya kuwakabili
wanyama hao wanaoharibu mazao yetu," alisema Dkt. Kawambwa.
Mwenyekiti
wa Kitongoji hicho Amani alisema kuwa walivamiwa na tembo tarehe 21 mwezi wa 8,
wakarudi tena tarehe 18 wakarejea tena tarehe 20, yena 23 na kwamba tarehe 10
mwezi wa 9 wakarudi kwa mara nyingine wakiwa wawili.
Akitoa
neno la shukrani, Mkumbi alianza kwa kumpongeza Dkt. Kawambwa kwa kuguswa na
changamoto hiyo, ambayo aliiwasilisha kwa Waziri husika, kisha kupatikana kwa
Maofisa hao kufika na kutoa elimu hiyo.
No comments:
Post a Comment