Sunday, December 30, 2018

MLAWA ATOA WITO KWA WAZAZI BAGAMOYO.

  Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wilaya ya Bagamoyo, Aboubakari Mlawa, akizungumza wakati wa kufunga semina ya siku mbili ya watendaji wajumuiya hiyo na makatibu Elimu, Malezi na Mazingira wa kata iliyofanyika Nianjema Bagamoyo, kulia ni Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bagamoyo, Abduli Sharifu na kushoto ni Katibu wa Jumuiya ya wazazi Mkoa wa Pwani, Juma Gama.
..............................

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wilaya ya Bagamoyo, Aboubakari Mlawa amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanawaandikisha watoto wenye umri wa kuanza shule ya msingi ili wapate haki yao ya kupata elimu huku wale wanaotakiwa kujiunga na kidato cha kwanza wapelekwe kwenye shule walizopangiwa haraka iwezekanvyo.

Mlawa ameyasema hayo leo Desemba 30, 2018 wakati wa kufunga semina elekezi ya siku mbili kwa watendaji wa Jumuiya ya wazazi, kata pamoja na makatibu Elimu na Malezi wa kata iliyofanyika kata ya Nianjema Halmashauri ya Bagamoyo.

Alisema Jumuiya ya wazazi pamoja na majukumu mengine ni pamoja na kusimamia Mazingira na Malezi pamoja na maadili kwa watoto hivyo ni lazima jumuiya ihakikisha inasimamia vyema majukumu hayo na kuwahimiza wazazi na walezi kutekeleza hilo.

Aliongeza kwa kusema kuwa licha ya kuwa wilaya ya Bagamoyo ni wilaya inayoongoza kitaaluma katika mkoa wa Pwani, lakini pia ndio wilaya ambayo watoto wengi hawaandikshwi kuanza darasa la kwanza na kuendelea na kidato cha kwanza.

Aidha, ametumia fursa hiyo kusisitiza umoja na mshikamano ndani ya jumuiya kuanzia ngazi ya kata mpaka wilaya kwani hiyo ndio siri ya mafanikio yanayopatikana ndani ya jumuiya ya wazazi.

Alisema jumuiya hiyo wilaya iko imara na kwamba haiwezi kutetereka kwakuwa inafanya kazi kama timu moja na hivyo inaweza kupambana na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza kwaajili ya kukwamisha maendeleo.

Mwenyekiti huyo wa jumuia ya wazazi aliwaataka washiriki wa semina hiyo kutumia mafunzo hayo kama njia ya kuongeza uwajibikaji kwa ufanisi zaidi na kuongeza wigo wa wanachama ndani ya jumuia na chama kwa ujumla.

Alisema jumuiya ya wazazi ikitekeleza majukumu yake ipasavyo ndio njia pekee ya kuipatia ushindi CCM katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019 na hata ule wa Rais, madiwani na wabunge 2020.

Aliendelea kusema kuwa,  jumuiya hiyo inatekeleza majukumu yake kwa weledi katika kusimamia maadili kila mmoja kwenye eneo lake anapaswa kuhakikisha anapinga vitendo vya rushwa ili kila hatua inayofikiwa katika chaguzi mbalimbali ifikiwe kwa haki na uadilifu.

Kwa upande wake Katibu wa Jumuiya ya wazazi Mkoa wa Pwani Juma Gama ametoa wito kwa wana jumuiya kuinua uchumi wa mmoja mmoja, na jumuiya kwa ujumla kwa kuanzisha miradi mbalimbali ikiwemo ya ufugaji wa nyuki ili kujiletea maendeleo.

Alisema kiongozi atakapojiimarisha kiuchumi ataweza kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kujenga uaminifu katika jamii kwakuwa hatapita kuomba omba.

Alisema kama jumuiya ya wazazi inapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika kujiinua kiuchumi ili utekelezaji wa majukumu ya jumuiya na chama uende kwa ufanisi na sio kwa utapeli.

Aidha, aliwaonya wale wote waliochaguliwa ndani ya jumuiya na wanashindwa kutekeleza majukumu yao ni vyema sasa sheria ikachukua mkondo wake kwa kumsimamisha ili nafasi yake izibwe na mtu mwingine.

Alisema uongozi ni uwajibikaji hivyo yule ambae hawezi kuwajibika anastahili kuwekwa pembeni ili watu wenye nia ya dhati na jumuiya hiyo waweze kusonga mbele.

Washiriki wa semina hiyo wamesema wamefaidika na kile walichofundishwa na kwamba wataleta mabadiliko kwenye maeneo yao.

Katika semina hiyo ambayo imeandaliwa na Jumuiya ya Wazazi wilaya ya Bagamoyo na kukusanya washiriki kutoka kata zote za wilaya hiyo wamejifunza mipaka ya uongozi, uandaaji wa mihutasari, Barua, Taarifa na kazi pamoja na mambo mbalimbali yanayohusu itifaki ndani ya Chama Cha Mapinduzi.
 
Muwezeshaji Hassan Tambaza akitoa mafunzo kwa washiriki
 
Muwezeshaji Mwinyi Sangaraza akitoa mafunzo kwa washiriki

 Katibu wa Jumuiya ya wazazi wilaya ya Bagamoyo, Aeshi akizungumza na washiriki katika semina hiyo.

Washiriki wakifuatilia mada zilizowasilishwa katika semina hiyo
 
Washiriki wakifuatilia mada zilizowasilishwa katika semina hiyo
   Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wilaya ya Bagamoyo, Aboubakari Mlawa, (kulia) na Katibu wa Jumuiya ya wazazi Mkoa wa Pwani, Juma Gama (kushoto) wakifuatilia semina hiyo.

No comments:

Post a Comment