Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Tuzo Mshindi wa Kwanza wa Mashindano
ya TEHAMA ya HUAWEI, Emmanuel Chaula wa Chuo Kikuu cha Dar
es salaam katika sherehe za kukabidhi Tuzo hizo kwenye hoteli ya Hayyat Regency
jijini Dar es salaam, Desemba 5, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipokabidhi Tuzo za Mashindano
ya TEHAMA ya HUAWEI kwenye hoteli ya Hayyat Regency jijini Dar es
salaam, Desemba 5, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
............................................
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya
Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imetoa kipaumbele kwenye
matumizi ya TEHAMA ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utendaji
kazi wa shughuli za Serikali za kila siku.
Hivyo, amewataka wananchi kutumia vizuri
teknolojia hiyo ya habari na mawasiliano kwenye shughuli za uzalishaji mali na utoaji
huduma katika sekta mbalimbali kwa lengo la kukuza uchumi na
kuwapunguzia wananchi umaskini pamoja na kuongeza ajira.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Desemba
5, 2018) katika sherehe za utoaji tuzo za mashindano ya TEHAMA ya HUAWEI
yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo ametumia fursa hiyo kuwaonya watu
wote wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii nchini.
“Nawaonya watu wote wanaotumia vibaya mitandao ya
kijamii waache. Ni vema wakatumia mitandao hiyo kwa kuhamasishana mambo mema
zikiwemo shughuli mbalimbali za maendeleo. Na kwa wataokiuka sheria ipo na
inaendelea kufanya kazi.”
Amsema Serikali inaamini kuwa matumizi ya TEHAMA yataongeza
ufanisi katika kuwahudumia ipasavyo wananchi, mfano katika sekta ya elimu
mwalimu mmoja anaweza kufundisha wanafunzi wengi kutoka katika shule tofauti
kwa wakati mmoja.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa “Matumizi ya TEHAMA kwa
kiasi kikubwa yatapunguza gharamaza za uendeshaji kwani yanaweza kufanikisha
mawasiliano binafsi, warsha na maelekezo mbalimbali kuwafikia walengwa bila ya
kusafiri nje ya vituo vyao vya kazi.”
Ametoa mfano Juni 2017 Rais Dkt. Magufuli
alizindua mfumo wa ukusanyaji Mapato ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na
Ushuru wa Bidhaa (Excise Duty) kwa njia ya kielektroniki na kudhihirisha kuwa,
sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano ni muhimili muhimu wa maendeleo
kwenye sekta zote, ikiwemo viwanda, utalii, ujenzi, elimu, afya, kilimo, uvuvi
na ufugaji.
“Kwa kuzingatia hayo, mwezi Juni 2018 wakati wa
maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Serikali ilizindua mifumo tisa ya
TEHAMA, ambayo inalenga kuimarisha utendaji wa Serikali hususan katika
kuwahudumia wananchi kwenye sekta mbalimbali ikiwemo afya, ukusanyaji mapato na
utoaji wa taarifa.”
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea
kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika kutengeneza mifumo ya TEHAMA
ili kutekeleza kwa vitendo azmaya kuwapatia wananchi
maendeleo hususani waishio maeneo ya vijijini huduma bora na kwa wakati.
Amesema kwa sasa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI) inauwezo wa kuona na kubaini makusanyo
yanayoendelea kukusanywa katika halmashauri mbalimbali nchini na kiasi
kinachoingizwa benki kwa kupitia TEHAMA.
Pia, Waziri Mkuu amsema Serikali imeendelea
kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwenye taasisi zake ili kufanikisha
azma ya kutumia Serikali mtandao, zoezi ambalo linakwenda sambamba na
kuunganisha baadhi ya shule za msingi, shule za Sekondari, Ofisi za Wakuu wa
Wilaya, Polisi, Hospitali za Wilaya, Vyuo Vikuu na Vituo vya Posta.
Wakati huo huo,Waziri Mkuu ameipongeza kampuni ya
HUAWEI kwa uzinduzi wa program yao
ya Seed
of the Futureambayo inalengo la kuwajengea uwezo wa TEHAMA wanafunzi
mbalimbali nchini katika hatua za awali kabisa.
Amesema iwapo TEHAMA itatumika vizuri itatoa fursa
kwa watu wote kupata elimu, kuleta usawa katika elimu, kujenga mazingira na
mbinu bora za ufundishaji na kujifunza, kuongeza weledi wa walimu, kuimarisha
usimamizi wa masuala ya elimu, uongozi na utawala.
Mashindano hayo ya TEHAMA ya HUAWEI yaliasisiwa
mwaka 2015 na baadaye mwaka 2016 yakazinduliwa huko Afrika Kusini, ambapo hadi
kufikia mwaka 2017 tayari wanafunzi wapatao 40,000 wameshiriki mashindano
hayo.
Kwa upande wa Tanzania, yamezinduliwa mwaka huu,
ambapo wanafunzi 500 walishiriki na baadaye kubaki 50,
ambapo waliokabidhiwa tuzo ni saba na watatu kati yao na mkufunzi
mmoja wamepata fursa ya kushiriki hatua inayofuata ya mashindano hayo nchini
Afrika Kusini.
Sherehe hizo zimehudhuliwa na Balozi wa China
nchini Tanzania, Balozi Wang Ke, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,
Profesa Joyce Ndalichako, Naibu Wazri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
Mhandisi Atashasta Nditiye, Mkurugenzi Mtendaji wa HUAWEI Tanzania Frank Zhou
na wawakilishi mbalimbali wa taasisi za Umoja wa Mataifa nchini.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Balozi wa China Nchini, Mhe. Wang Ke
wakati alipowasili kwenye Hoteli ya Hayyat Regency jijini Dar es salaam, Kutoa
Tuzo za Mashindano ya TEHAMA ya HUAWEI, Desemba 5, 2018. Wapili
kushoto ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Profesa Joyce
Ndalichako na kulia ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na viongozi walioshiriki
katika sherehe za Utoaji Tuzo za Mashindano ya TEHAMA ya HUAWEI
kwenye hoteli ya Hayyat Regency jijini Dar es salaam, Desemba 5, 2018. Kutoka
kushoto ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi, Atashasta
Nditiye, Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Profesa Joyce Ndalichako,
Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya HUAWEI nchini, Frank Zhou
na Balozi wa China nchini, Mhe. Wang Ke. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu)
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa na Viongozi wa Kitaifa na Kimataifa wakiwa katika picha
ya pamoja na washindi wa Mashindano ya TEHAMA ya HUAWEI baada ya
kuwakabidhi tuzo za ushindi washindi hao kwenye hoteli ya Hayyat Regency jijini
Dar es salaam, Desemba 5, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
No comments:
Post a Comment