Mjumbe
wa Halmashauri Kuu ya BAKWATA Mkoa wa Mwanza Nurdin Mbaji akishiriki kuchagia
damu kwenye maaadhimish ya miaka 50 ya baraza hilo.
Kaimu
Sheikh wa Mkoa wa Mwanza Alhaji Sheikh Hasani Musa Kabeke akizungumza na
waumini wa dini ya Kiislamu wakati wa kuchangia damu kwenye maadhimisho ya
miaka 50 ya BAKWATA yaliyofanyika kimkoa jijini Mwanza juzi.
.................................................
NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA.
WAUMINI wa Dini ya Kiislamu wameadhimisha miaka 50
tangu kuanzishwa kwa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kwa kuchangia
damu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure.
Akizungumza kwenye maadhimisho hayo na wakati wa
uchangiaji damu Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Mwanza Alhaji Hassan Musa Kabeke
alisema Waislamu waone fahari kujitolea kuchangia damu ili kuokoa maisha ya
watu wenye mahitaji ya damu.
Alisema takwimu zinaonyesha waathirika na wahitaji
wakubwa ni watoto chini ya miaka mitano,akina mama wajawazito wanaojifungua na
majeruhi wa ajali mbalimbali zikiwemo za pikipiki maarufu bodaboda.
Alieleza kuwa ajali zina mchango mkubwa wa
mahitaji ya damu na kuwataka watumiaji wa vyombo vya moto hasa pikipiki kutii
sheria ili kupunguza ajali, vifo na majeruhi kwani jamii inataka kuona Mwanza
na Tanzania
salama isiyo na ajali.
“Tuliamua kuadhimisha siku hii kwa kuangalia wenye
mahitaji na jambo linalotuunganisha ni damu.Wenye mahitaji makubwa wa damu ni
akina mama wanaojifungua , watoto wadogo na majeruhi na tunasaidiana katika
kumcha Mungu kwa kufanya mema badala ya dhambi,” alisema
Kaimu sheikhe huyo aliwataka waislamu wa taasisi
zote kujipanga na kufanya kazi ya kuhudumia jamii na waone umuhimu wa kujitolea
kwa Mungu na umma wa waislamu wenyewe na hivyo kushiriki kujitolea
damu ni kutoa nafsi na mwili kuwasaidia wengine wenye mahitaji ya damu.
Aidha, Sheikh Kabeke alimpongeza Mufti wa Tanzania
Abubakar Zuberi Bin Ali kwa kuasisi maadhimisho ya kuzaliwa kwa BAKWATA
ili kujitathmini na kujipima kama malengo yake yametimia au la, ingawa pia
watangulizi wake walifanya mambo mazuri.
Alieleza zaidi kuwa wapo watu wanapotosha
kwa kueneza maneno yasiyo sahihi kuwa BAKWATA ilinzishwa na Mwl Nyerere kwa
maslahi ya Ukristo na kuonya wanaofanya hivyo wanawavunjia heshima masheikh
waliokiasisi chombo hicho cha Waislamu.
“Jambo hili linapoachwa kuzungumzwa
linapotea.Masheikh hao walikutana Iringa kujadili na kuanzishwa kwa BAKWATA
lakini leo watu wanapotosha ukweli huo.Sheikh Amin Abdallah aliombwa awe Mufti
wa kwanza, lakini alikuwa mtu wa kujishusha na sababu ya uzee na busara
alimpendekeza Hemed Bin Jumaa Bin Hemed awe Mufti wa Tanzania,”alifafanua
sheikh Kabeke.
Pia alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais John
Magufuli kwa kuadhimisha miaka 57 ya Uhuru na kwamba uamuzi wake wa kuzuia
fedha za sherehe za Uhuru na kuelekeza zitumike kwa shughuli za maendeleo kwa
manufaa na maslahi ya Watanzani wote ni jambo la fahari.
“Rais Magufuli kazi yake inaonekana na jinsi
anavyosimamia rasilimali za nchi na nidhamu serikalini hakuna Mtanzania
asiyejua maana nchi ilifikia pabaya.Fedha za sherehe za Uhuru hapa Mwanza
zimejenga barabara hivyo hatuna budi kumpongeza,lakini pia wazee wetu wa
Kiislamu,”alisema
Naye mgeni rasmi Mratibu wa Mabalozi wa Usalama
Barabarani Kanda ya Ziwa Abel Ntahorutoba aliziasa taasisi za dini mbalimbali
kujenga utamaduni wa kuchangia damu ili kuokoa maisha ya watua huku
akikemea tabia ya waendesha pikipiki kuvunja sheria badala utii bila shuruti.
Alisema mabalozi wa usalama barabarani wataendelea
kuwaelimisha watumiaji wa barabara, abiria na madereva wa vyombo vya moto ili
kuwafanya Watanzania kuziishi sheria na kuzitii ili kuwa na Tanzania salama
isiyo na ajali.
“Tuwe na akiba ya damu na ni muhimu tukajenga
tabia ya kuchangia damu, hivyoa kwenye nyumba za ibada tuwaeleze waumini wetu
kuwa damu hainunuliwi na hakuna anayefahamu thamani yake.Lakini pia tuziogope
ajali ambazo zinauawa kuliko UKIMWI,”alisema Ntahorutoba.
Kwa upande wake Katibu wa Hospitali ya Sekou Toure
Leah Lint aliwapongeza waumini hao wa dini ya Kiislamu kwa mchango wao wa damu
kwani wameokoa maisha ya watu wengi na kushauri taasisi zingine ziige kitendo
hicho ambacho kinawafairiji pia wagonjwa.
“Wagonjwa wamefarijika kwa damu hiyo,hivyo kitendo hiki kikasambae
kwa Watanzania wengine ili nao waige mazuri mnayofanya kwa kuwa uchangiaji huu
una maslahi mapana kwa jamii,”alisema Lint.
Afisa
Eimu wa Dini ya Kiislamu Abdi Musa pamoja na waumini wa dini hiyo wakichangia
damu kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure juzi.
Katibu
Muhtasi wa BAKWATA Mkoa wa Mwanza aliyehamika kwa jina moja la Sikitu
akichangia damu siku ya maadhimisho ya miaka 50 ya BAKWATA mkoani hapa. Wa
kwanza kulia ni Katibu wa JUWAKITA Dotto Mangu.
Kaimu
Sheikh wa Mkoa wa Mwanza na Mratibu wa Mabalozi wa Usalama Barabarani Abel
Ntahorutoba (kushoto) wakichangia damu kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Mwanza, Sekou Toure.
Mgeni
rasmi wa zoezi la kuchangia damu kwa waumini wa dini ya kiislamu jijini Mwanza,
Mratibu wa Mabalozi wa Usalama Barabarani Kanda ya Ziwa Abel Ntahorutoba
akizungumza kwenye zoezi hilo
wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya BAKWATA.
No comments:
Post a Comment