Thursday, December 6, 2018

DC BAGAMOYO AWAONYA WAPITISHA MAGENDO.

  Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Zainbau Kawawa, akizungumza na wafanyabiashara wanaoagiza mafuta ya kupikia kupitia Bandari ya Bagamoyo katika ukumbi wa mikutano ofisi ya Mkuu wa wilaya, kulia ni
Mkuu wa Takukuru wilaya ya Bagamoyo, Raymond Katima na kushoto ni Mkuu wa Polisi wilaya ya Bagamoyo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi-SSP Rajabu Shemndolwa
......................................
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Zainbau Kawawa amewaonya wanaopitisha magendo katika wilaya hiyo kuwa hawako salama.

Zainabu alitoa kauli hiyo alipokutana na wafanyabiashara ya mafuta ya kupikia wanaopitishia bandari ya Bagamoyo.

Katika kikao hicho ambacho kimewashirikisha waagizaji wa mafuta ya kupikia kutoka Zanzibar kupitia Bagamoyo, maafisa wa forodha, Afya, Biashara, TFDA na TRA lengo likiwa kuangalia changamoto zinazowakabili wafanyabiashara waagizaji mafuta ya kupikia, na maafisa wa serikali wanaohusika kukusanya tozo mbalimbali za serikali.

Katika kikao hicho wafanyabishara wa mafuta wamelalamikia kukamatwa na polisi hali inayopelekea kukwamisha biashara zao kwa siku kadhaa licha ya kuwa vibali vyao vimekamilika.

"tunapata tabu na polisi wanatukamata, wanakuja nyumbani na bunduki mpaka sasa mtoto wangu anaogopa kwenda shule kwa hofu ya polisi kwanini hawatukamati wakati tunatoa mizigo wanatufuata nyumbani?"  alisikika akilalamika mmoja wa wafanyabiashara hao aliyejitambulisha kwa jina Shabani Hamsini (chavurugu)

Kufuatia kauli hiyo, Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo aliwataka wafanyabiashara hao kutoa ushirikiano katika kuwafichua wale wote wanaotumia Bandari bubu kupitisha mizigo yao.

Alisema serikali itaendelea kuwasaka wale wote wanaokwepa ushuru na kodi za serikali na kuhakikisha inadhibiti Bandari bubu.

Aliongeza kuwa, ili kuepuka usumbufu wanaotumia Bandari na kulipa ushuru na kodi wanapaswa kuwataja wenzao wanakwepa kulipa kodi za serikali ili washughulikiwe vinginvyo serikali itawakamata wale wote wanawatilia mashaka ili kukagua mizigo yao kama imepitishwa kihalali.

" Labda niwaambie ndugu zangu, hii kadhia ya kukamatwa kamatwa haiwezi kuisha hapa Bagamoyo kama hamtatupa ushirikiano, ushirikiano tunaotaka wale wote wanaotumia Bandari bubu waache, mnafanana nao wengine mlitokea huko na bidhaa ni hizo hizo sasa ili tuikomeshe tabia hii watajeni vinginevyo tutkamata anaehusika na asiyehusika" Alisema Mkuu wa wilaya Bi Zainabu.

Kwa upande wao wafanyabiashara hao wamekiri kuwa awali walikuwa wanatumia Bandari bubu kupitishia bidhaa zao na sasa wameacha wanatumia njia rasmi ya Bandari na kulipa kila kinachohitajika.

Aidha, wametoa rai kwa mamlaka zinazohusika kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara wadogo ili nao waweze kutumia Bandari rasmi kupitishia mizigo yao kihalili.

Walisema ni wazi kuwa mazingira yakiwa mazuri kwa wafanyabiashara hakuna atakaepitia porini kwani porini kuna hatari nyingi ikiwemo kukamatwa na kupoteza mzigo wako.

Mkuu wa wilaya aliwataka wataalamu kutoka TFDA, TPA, TRA na FORODHA, kutoa elimu kwa wafanyabiashara hao ili kila mmoja awezekutumia njia sahihi kwa wakati sahii kuepuka usumbufu.

Alisema kila mmoja ana wajibu wa kukomesha Bandari bubu kwani Bandari bubu sio tu zinapitisha mafuta lakini pia vinaingizwa vitu vya aina mbalimbali ambavyo vingine ni hatari kwa usalama na afya.

Akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa Polisi wilaya ya Bagamoyo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi-SSP Rajabu Shemndolwa, alisema polisi inapotekeleza majukumu yake haina lengo la kumkomoa raia bali inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria na kanuni.

Aliwataka raia wote wilayani humo kutii sheria bila ya shuruti ili kila mmoja afanye shughuli zake kwa amani na utulivu.

Akizungumzia kukamatwa kwa magari yanayobeba bidhaa zinazotoka Bandalini, SSP Shemndolwa alisema hiyo ni katika kuhakiki mzigo uliobebwa umefuata taratibu za kisheria au la.

Aliongeza kwa kusema kuwa Polisi ndio wenye mamlaka ya kisheria kusimamisha gari na kisha ukaguzi wa nyaraka mbalimbali za mzigo utafanywa na idara husika ili kujiridhisha kilichobebwa kama kinafanana na nyaraka zilizooneshwa.

Alisema tayari ameshatoa maelekezo kwa askari polisi juu ya utaratibu wa kukamata magari yaliyobeba mizigo na kusema kuwa polisi watakagua kinachowahusu na maafisa wa idara nyingine za serikali watakagua vinavyowahusu ili kila mmoja atekeleze wajibu wake kwa ufasaha.
 Mkuu wa Polisi wilaya ya Bagamoyo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi-SSP Rajabu Shemndolwa, akizungumza katika kikao hicho.

Wafanyabishara waagizaji wa mafuta ya kupikia kutoka Zanzibar kupitia Bagamoyo,wakiwa katika kikao kilichoitishwa na Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili.
 
Baadhi ya Wafanyabishara waagizaji wa mafuta ya kupikia kutoka Zanzibar kupitia Bagamoyo, wakiwa nje ya Ukumbi baada ya ndani kujaa katika kikao kilichoitishwa na Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili.


 Wa kwanza kulia ni Afisa Mwandamizi wa Kituo cha Forodha Bandari ya Bagamoyo Noeli Makere, na wapili ni Meneja wa Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) Kanda ya Mashariki, Emmanuel Alphonce
 Kutoka kushoto ni Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Forodha Bandari ya Bagamoyo, Raymond Mwanisawa, wa pili ni Meneja wa Mamlaka ya mapato nchini (TRA) wilaya ya Bagamoyo, Farence Mniko wa tatu ni Mkuu wa Polisi wilaya ya Bagamoyo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi-SSP Rajabu Shemndolwa, wa nne ni Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Zainbau Kawawa, na watani ni Mkuu wa Takukuru wilaya ya Bagamoyo, Raymond Katima.

No comments:

Post a Comment