Asema Hali ya hewa isiwe kisingizio cha kuchelewesha
miradi ya umeme vijijini.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewataka
wakandarasi wanaosambaza umeme vijijini kutochelewesha utekelezaji wa miradi
hiyo kwa kisingizo cha mabadiliko ya hali ya hewa kama
vile uwepo wa mvua.
Aliyasema hayo wilayani Makete mkoani Njombe
wakati alipokuwa akikagua kazi ya usambazaji umeme vijijini inayotekelezwa
kupitia mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu (REA III) mzunguko wa kwanza.
“ Kabla ya Serikali kuwakabidhi kazi hii ya
usambazaji umeme vijijini, mlishafanya upembuzi wa maeneo mnayoenda kufanyia
kazi na mnayafahamu vizuri, hivyo basi, iwe Jua au mvua, tunataka kuona kazi
hii inaendelea kutekelezwa ili wananchi wengi wapate huduma ya umeme,” alisema
Mgalu
Aliongeza kuwa, wakandarasi hao wanapaswa kuwa na
mipango mbalimbali ya utekelezaji wa kazi kulingana na hali ya hewa ya maeneo
wanayofanyia kazi ili kuweza kusambaza umeme katika vijiji vyote walivyopangiwa
na Serikali ifikapo Juni 2019.
Awali, Mkuu Wilaya ya Makete, Veronica Kessy,
alimweleza Naibu Waziri kuwa, jumla ya vijiji 29 vimepangwa kuunganishiwa umeme
kupitia mradi wa REA III mzunguko wa kwanza ambapo mkandarasi anaendelea na
kazi ya usambazaji umeme vijijini, ingawa uongozi wa Wilaya hiyo umekuwa na
wasiwasi na kasi yake katika usambazaji umeme.
Kuhusu hali ya upatikanaji umeme, alisema kuwa
Wilaya hiyo inapata umeme kutokea mkoani Mbeya lakini laini hiyo ni ndefu na
inapelekea changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara hivyo aliomba Wilaya
hiyo ipate laini nyingine ya umeme kutokea mkoani Njombe.
Kuhusu suala hilo, Naibu Waziri wa Nishati, Subira
Mgalu, alisema kuwa, Serikali ilishaona changamoto hiyo ya umeme wilayani
Makete na kueleza kuwa Wilaya hiyo ipo katika mpango wa kupelekewa umeme
kupitia mradi wa Makambako- Songea ambao umekamilika.
Akiwa wilayani humo, NaibuWaziri aliwasha umeme
katika kijiji cha Bulongwa na kukagua miundombinu ya umeme katika Kijiji cha
Usagatikwa na Usungilo ambapo alimsisittiza mkandarasi kuongeza kasi ya
kusambaza umeme.
Wilaya ya Makete ina Vijiji 96 ambapo vijiji 29
tayari vimeshasambaziwa umeme, vijiji 29 vinasambaziwa umeme kupitia REA III
mzunguko wa kwanza na Vijiji 38 vinavyosalia vitasambaziwa umeme kupitia mradi
wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu unaotarajiwa kuanza Julai
mwakani.
No comments:
Post a Comment