Sunday, December 2, 2018

DC BAGAMOYO AAGIZA KUKAMATWA MHASIBU MKUU NA WASAIDIZI WAKE WATATU HALMASHAURI YA CHALINZE KWA UBADHILIFU WA FEDHA.

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Bi Zainabu Kawawa ameagiza watumishi wa idara ya fedha katika halmashauri ya wilaya ya Chalinze wanaoshughulika na ukusanyaji mapato wakamatwe na kupisha uchunguzi kufuatia hali ya ukusanyaji mapato katika halmashauri hiyo kuwa chini ya kiwango tarajiwa, agizo hili amelitoa leo katika kikao alipokuwa akizungumza na watumishi wa halmashauri hiyo.

Watumishi alioagiza wapishe uchunguzi ni Mweka Hazina wa halmashauri Bwana David Rubibira, na wahasibu watatu ambao ni Waziri Ally, Jumanne Sanga na Maneno Kwambwa

Mheshimiwa Kawawa alisikitishwa na ukusanyaji mapato katika halmashauri ya Chalinze kuwa chini ya malengo na kudai kuwa kuna mianya ya ubadhirifu wa mapato kwani mapato ya halmashauri yakikusanywa kwa umakini yanafikia milioni 920 kwa mwezi kwa chanzo cha madini ya kokoto nje ya vyanzo vingine kwa maana ya milioni 33 kwa siku.

Hivyo kutokana na makisio hayo Mkuu wa wilaya hana imani na mapato yanayokusanywa katika halmashauri hiyo ambayo ni wastani wa milioni 550 hadi 659 kwa mwezi.

Aidha baada ya kikao hicho Mheshimiwa kawawa alimtaka Mkuu wa polisi Chalinze kuwaweka chini ya ulinzi na kuwachukua kwa ajili ya uchunguzi na baada ya uchunguzi kukamilika hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao kwa kusababisha upotevu wa mapato.

"Nimekuwa nikifuatilia ukusanyaji mapato kuna mianya mingi ya utoroshaji mapato, tusitafutane wala kujaribiana kwa kuvujisha mapato tumepoteza Mapato sana kwenye makrasha kwa siku tuna uwezo wa kukusanya milioni 33 ,kwa mwezi tuna uwezo wa kukusanya zaidi ya milioni 900, badala ya kufuatilia na kukagua mnakaa tu ofisini katika hili hatuwezi kuvumiliana hata kidogo,Mkurugenzi nakuagiza watumishi wanaohusika na mapato wakae pembeni kwa hatua zaidi kuanzia leo na vyombo vya usalama vifanye kazi katika kuchunguza haya." Mheshimiwa Kawawa aliagiza.


No comments:

Post a Comment