Thursday, December 27, 2018

WAZAZI KIBITI KUPAMBANA NA MAADILI

Na Omary Mngindo, Kibiti

JUMUIA ya Wazazi wilaya ya Kibiti Mkoa wa Pwani, imedhamilia kupambana na vitendo vya mmomonyoko wa maadili wilayani humo, vinavyoendelea kushika kasi kila kukicha.

Mwenyekiti wa Jumuia hiyo Nurdin Ugama ameyasema hayo hivi karibuni, akizungumza kwenye Kongamano lililoandaliwa na Jumuia hiyo, mbele ya mgeni rasmi Mwenyekiti wa Wazazi Mkoa Jackson Josian, Katibu Juma Gama, Mbunge Ally Ungando na Maofisa kutoka Polisi, Magereza, Walimu na TAKUKURU lililofanyika shule ya sekondari Kinyanya.

Ugama alisema kwamba, katika wilaya hiyo kuna baadhi ya vijana wanajihusisha na vitendo vinavyokinzana na sheria na taratibu, ambao hufanya fujo sanjali na kupora watu hususani wanaopita kwenye mabasi katika kituo Kikuu kilichopo Kibiti mjini.

"Kuanzia leo Jumuia ya Wazazi wilaya ya Kibiti tumekubaliana kupambana na vijana wanaojihusisha na vitendo vya mmomonyoko wa maadili, hali ikiachwa inaweza kupotosha wengine wenye maadili mema, pia tunaonya ngoma ya Kiduku," alisema Ugama.

Sanjali na hilo pia wamepiga marufuku uvaaji wa nguo fupi kwa wasichana, sanjali na kuwakemea wamiliki wa baa ambazo wasichana wanageuza maeneo ya kufanyia vitendo vya ngono, huku akiliomba jeshi la Polisi kuungana katika kukomesha vitendo hivyo.

Akizungumza kwenye kongamano hilo, Jackson alisema kuwa Jumuia inaungana na Rais Dkt. John Magufuli katika kufayanyiakazi maagizo au ushauri wote alioutoa kwa Jumuia kuhakikisha inadhibiti vitendo vinavyoendelea ambavyo havina maadili.

Jackson alisema kwamba Jumuia haitamwangusha Rais na kuwa watapambana na vitendo viovu kwani kinyume chake ni kukinzana na agizo la Serikali lililotolewa na Rais Magufuli, huku akiwataka viongozi wa vyama na serikali mkoani humo kuungana ili kukomesha vitendo viovu.

"Niwapongeze Jumuia ya Wazazi wilaya ya Rufiji kwa Kongamano hili zuri, niwakumbushe viongozi kwamba tuna ajukumu kubwa la kusimamia maadili kwa jamii kama tulivyopewa ba Rais Dkt. John Magufuli," alimalizia Jackson.

No comments:

Post a Comment