Monday, December 31, 2018

MKURUGENZI WA TIBA ATOA TAARIFA KWENDA KWA WAMILIKI WA MAABARA BINAFSI ZA AFYA KUHUSU UTEKELEZAJI WA SHERIA YA UMILIKI WA MAABARA BINAFSI ZA AFYA.

Mkurugenzi wa Tiba, Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima akisisitiza jambo katika mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa sheria ya umiliki wa maabara binafsi za Afya.
.................................................


Dkt. Dorothy Gwajima, Mkurugenzi wa Tiba wa WAMJW ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Maabara Binafsi za Afya (Private Health Laboratory Board) (PHLB). amewatakia heri ya mwaka mpya 2019 na hongera wamiliki wa maabara binafsi za afya kwa kazi kubwa waliyofanya mwaka 2018 ya kushirikiana bega kwa bega na sekta ya afya katika kuhakikisha taarifa sahihi zinawafikia wananchi na wadau wote kokote waliko.

Katika kufikisha salaam zangu kwa wamiliki wa maabara binafsi, amewashukuru wamiliki hawa kwa kuchagua kuwekeza katika sekta ya afya nchini Tanzania, na kuwapongeza wale wote waliowekeza huku wakihakikisha wanafuata taratibu zote za kisheria za uwekezaji huo.

Aidha, amewakumbusha wamiliki wa maabara binafsi kuwa, umiliki huu unasimamiwa na sheria namba 10 ya mwaka 1997 inayowataka wamiliki wote kusajiliwa na kutambuliwa na PHLB kisheria. Hii ni hata kama maabara husika inajitegemea au iko ndani ya kituo cha kutolea huduma za tiba cha aina yoyote cha ngazi yoyote ile, maabara husika inatakiwa itimize matakwa ya kisheria.

Amesema  kufikia Septemba, 2018 PHLB ilikuwa inazitambua jumla maabara 641 zinazojitegemea na 719 zilizoshikizwa kwenye vituo vya tiba vya watu binafsi vya ngazi mbalimbali.

Katika utekelezaji wa majukumu yake, Bodi imeendelea kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa shughuli za maabara binafsi kama sheria inavyotaka, na kupitia utekelezaji huo imebaini wako baadhi ya wamiliki ambao, hawatimizi matakwa ya kisheria.


Kutotekeleza matakwa ya kisheria siyo tu kunaifanya maabara husika kuwa mbali na macho ya Bodi katika kuhakikisha usimamizi wa ubora wa huduma, bali kunamfanya mmiliki husika kukwepa wajibu wake wa msingi kwa serikali ikiwemo kulipa tozo na ada stahiki zitokanazo na biashara anayofanya na hii ni kukwamisha juhudi za Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo kulingana na mipango yake. Hili halikubaliki hata kidogo.

 Kanuni za kumiliki maabara binafsi zinataka mmiliki kutekeleza mambo makubwa yafuatayo;-

1. Kufuata utaratibu wa kusajiliwa (kwa maabara zinazojitegemea) na kufuata utaratibu wa kujiandikisha na kutambuliwa na Bodi husika kwa maabara ambazo zimesajiliwa pamoja na vituo vya tiba (zilizoshikizwa).
2. Kulipa ada stahiki kila mwaka ambazo ni ada ya uhakiki wa ubora wa huduma na ingine ni ada ya ukaguzi.


Kutokana na baadhi ya wamiliki wa maabara binafsi hususan zilizoshikizwa kutofuata maadili ya uwajibikaji kisheria, bodi imebaini kuwa, kufikia Septemba 2018, kati ya vituo vya tiba 1731 vya watu binafsi vyenye maabara ndani ni maabara 1012 (58%) tu ndiyo zilikuwa zimetimiza wajibu wake wa kujiandikisha kwenye Bodi ya Usimamizi wa Maabara Binafsi na kutekeleza matakwa yote ya kisheria kama nilivyoeleza hapo awali.

Ni kweli kwamba, vituo hivi vya maabara binafsi viko ndani ya vituo vya tiba ambavyo, vinasimamiwa na Sheria ya Usajili wa Vituo Binafsi (PHAB) lakini, hili haliondoi utekelezaji wa sheria ya PHLB yenye dhamana ya kusimamia maabara binafsi. Wizara inakubalina na hoja kuwa, vema sheria hizi zikajumuishwa, na tayari imeanza kufanyia kazi na wadau wote wanafahamu na wameshiriki hivyo, hii haiwezi ikawa ndiyo sababu ya kutowajibika kutekeleza sheria halali ambazo bado ziko hai.

Wizara kupitia Bodi husika imeendelea kuelimisha na kufafanua juu ya mamlaka tofauti za sheria hizi mbili, lakini bado baadhi ya wamiliki wa maabara binafsi wamekuwa wakikwepa tu kuwajibika kwa makusudi.

Aidha, leo hii, watendaji wa sekretarieti ya bodi ya PHLB kwa kushirikiana na sekretarieti ya PHAB na viongozi wa sekta ya afya ngazi zote wakiwemo OR TAMISEMI, Ofisi za Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya mbalimbali, tumehitimisha ziara ya kufuatilia utekelezaji wa shughuli za maabara binafsi za afya katika mikoa mbalimbali ukiwemo mkoa wa Dar es Salaam.

Kupitia ziara hii, tumechambua na kubaini kuwa, wamiliki wengi wasiotekeleza sheria ya umiliki wa maabara binafsi wanatokea miongoni mwa wanaomiliki maabara zilizoshikizwa yaani, zilizomo ndani ya vituo vya tiba ngazi mbalimbali. Aidha, katika kundi hili, wapo watu ambao, kimsingi huwezi kuwatarajia kutokana na elimu zao, kazi zao na Imani zao kwa jamii inayowazunguka (wao wanajijua). Hii haivumiliki kabisa.

Kwa kuwa nilikuwa mstari wa mbele kuwafikia wale wamiliki wa maabara binafsi walioripotiwa kuwa eti wameshindikana, nimewafikia baadhi yao na kusikiliza hoja zao na kubaini kuwa, hazina mashiko kabisa. Eti, hoja yao ya msingi ni kuwa, wanapolipa kusajili kituo cha tiba huwa wanadhani kuwa, tayari na maabara imejumuishwa humo.

 Utetezi huu siyo wa kweli kwa kuwa, sheria ya kusimamia umiliki wa vituo binafsi vya tiba iko wazi na ina bodi yake na hii ya kusimamia umiliki wa maabara binafsi nayo iko wazi na ina bodi yake na siku zote wamekuwa wakielimishwa na mimi nimeshiriki mara nyingi kutoa elimu hiyo.

Nimeona leo nirudie tena kufafanua kuwa, bodi ya usajili wa vituo vya Tiba inajukumu lake na haiingiliani kabisa na sheria ya bodi ya usimamizi wa kumiliki maabara binafsi.

Kwa kuwa wako wamiliki wa maabara binafsi ambao, wameamua kuamini kwenye kufuatiliwa kila siku, sasa ufuatiliaji na uelimishaji uliokwisha fanyika awali unatosha, wakati wa kuelewa somo umepita sasa ni saa ya KAZI TU !. Imefika zamu ya wamiliki wa maabara binafsi waliokuwa hawajatekeleza wajibu wao wa kumiliki maabara hizo kisheria kuchukua hatua mara moja za kwenda kutimiza wajibu wao bila shurti tena pasipo kuendelea kuisababishia Serikali gharama za ziada za kuwafuatilia. 


Hivyo, ifikapo tarehe 15/1/2019 ambaye hajatimiza wajibu wake ni kwamba, atafungiwa bila taarifa ya ziada na kushtakiwa. Iwapo kuna ambaye anayejiandaa kutotimiza matakwa hayo, bora atumie muda huu kufunga ofisi yake kabisa ili kuepuka usumbufu usio wa lazima. Hata hivyo, kufunga ofisi hakutamuepusha mvunja sheria yeyote yule kuwajibika kwa uvunjifu wa sheria alioufanya awali.

Naomba ifahamike kuwa, kutimiza wajibu wa matakwa ya kisheria kwa wamiliki husika wa mabaara binafsi ni pamoja na;-

1. Kila mmiliki kuhakikisha amekidhi vigezo vyote vya kumiliki maabara binafsi kama ambavyo amekuwa akielekezwa na wataalamu walioko kila halmashauri na mikoa husika, pamoja na

 
2. Kuhakikisha amelipa ada na tozo stahiki zikiwemo malimbikizo ya nyuma na faini zote stahiki.

 
3. Amepata risiti halali za malipo hayo

 
4. Anaendelea kulipa tozo stahiki kila mwaka ili, kuwezesha bodi husika kutimiza wajibu wake wa kufanya uhakiki wa ubora wa huduma kwa kila kituo kila mwaka na kufanya ukaguzi maalumu wa vituo husika kama vinaendelea kuwa katika viwango stahiki kama siku vilipopewa kibali cha kutoa huduma husika.


Kwa kuwa tumebaini kuwa, wasiofuata sheria wanatoa huduma bubu mita chache tu toka serikali za mitaa, Bodi imeendelea kuimarisha ushirikiano wake na vyombo vyote vya Serikali ngazi zote kuanzia OR TAMISEMI na ngazi zake zote za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na sasa, Bodi inaandaa orodha ya maabara binafsi nchi nzima na itaweka katika gazeti la Serikali na vyombo vya habari na itasambaza kwa wadau wote.

Hivyo, yeyote ambaye hayumo katika orodha hiyo asithubutu kutoa huduma hizo maana, mamlaka za Serikali za mitaa zitambaini na taarifa zitafika mahali sahihi mara moja na hatua kali zitachukuliwa.
Aidha, natoa wito kwa mamlaka zote za Serikali ngazi zote tuendelee kupeana taarifa kwa haraka zaidi na kujipanga vema zaidi katika kuhakikisha hakuna mvunja sheria anathubutu kutoa huduma za kijamii bila kibali.


Ni matumaini yangu kuwa mtatumia umahiri wenu katika kuhakikisha ujumbe huu unawafikia wadau wote kwa usahihi. Aidha, nina Imani kuwa, wadau husika sasa wataacha utetezi dhaifu na watatimiza wajibu wao mara moja.

Mwisho, naomba kuwakumbusha wadau wote sekta ya afya kuwa, katika kujenga taifa letu, ni budi kila mmoja atimize wajibu wake ili, tuongeze kasi, kwa kuwa hakuna mtazamaji bali wote tuna majukumu na wajibu kamili.

Kaimu Msajili wa Bodi ya Maabara Binafsi za Afya akijibu maswali ya Waandishi wa habari wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari uliohusu utekelezaji wa sheria ya umiliki wa maabara binafsi za Afya.

Wajumbe wa Sekretariet ya Maabara binafsi pamoja na kamati ya Afya ya msingi za manispaa za jiji la Dar es salaam wakifuatilia maelekezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Tiba, Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima kuhusu utekelezaji wa sheria ya umiliki wa maabara binafsi za Afya katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya jijini Dar es salaam.

No comments:

Post a Comment