Friday, December 14, 2018

UPEPO WABOMOA NYUMBA 157 NACHINGWEA.

 Na Hadija Hassan- Lindi

Nyumba {157} yakiwemo majengo ya Serikali zimebomolewa kufuatia upepo mkali ulioambatana na mvua  iliyonyesha juzi ,Wilaya ya Nachingwea, Mkoani Lindi.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Nachingwea Bi, Rukia Muango ambae pia ndio   mkuu wa wilaya hiyo, 

Alisema kuwa mvua hiyo ilianza majira ya saa 10:30-11:30 jioni iliambatana na Upepo mkali ambao ,licha ya kuharibu Nyumba za kuishi wananchi wa kata za Nachingwea, songa mbele na Stesheni, pia umeharibu  na Zahanati ya  Stesheni.

Pia,alifafanua kwa kutaja maeneo yaliyokumbwa na balaa la  upepo huo ni pamoja na kata za Stesheni Nyumba na Zahanati jumla (83), Kata ya Songa Mbele nyumba  (14) na kata ya Nachingwea Nyumba (60) kufanya idadi kufikia' (157).

Mkuu huyo wa wilaya amesema katika tukio hilo hakuna mtu aliyekuwa amepoteza maisha,bali ni watu wanne {bila kutaja majina},waliangukiwa na kuta za nyumba zao,kisha kukimbizwa Hospitali ya wilaya hiyo,wakatibiwa na kuruhusiwa kurejea majumbani mwao.

Hata hivyo Mwango alieleza Kwamba  bado hasara iliyopatikana haijaweza kufahamika mara moja, na kwamba Ofisi yake imewaagiza wataalamu kufanya upembuzi yakinifu ili kubaini idadi yake.



Mwango ametaja sababu zilizochangia kubomolewa kwa nyumba na Jengo la Zahanati,ni ujenzi usiozingatia ubora,ikiwemo kutokuwepo kwa Linta zilizo na ubora na kutumia mbao zisizokuwa na viwango vinavyohitajika.

“Zahanati nayo mbao zilizotumika kuwekea kenchi ni nyembamba mno,hivyo upepo ulipofika ilikuwa rahisi tu kuezua na kuweka kando”Alisema Mwango.

Hata hivyo Mwango Alisema kuwa kutokana na tukio hilo serikali Wilayani humo imeamua kuifunga zahanati ya stesheni mpaka itakapofanyiwa ukarabati

Pia,Mwango aliongeza kuwa watu wote walioathiriwa na upepo huo,karibu wote wamepatiwa hifadhi na baadhi ya Jamaa na majirani zao,huku Ofisi yake ikiandaa taarifa kupeleka Ofisi ya Maafa kuona namna itakavyoweza kusaidia wale watakaobainika kuathirika zaidi na upepo huo.



Aidha, amewataka wananchi wote wilayani Nachingwea wanaotaka kujenga Nyumba za kuishi kuwatumia wataalamu wa majengo waliopo ili kupata maelekezo ya kitaalamu ili kuepuka hasara kama walivyoipata sasa.

Hii ni mara ya pili kwa Mkoa wa Lindi kupata mkasa wa aina hii,kwani wiki iliyopita upepo aina ya Kimbunga ulioambatana na mvua kiasi umepoteza mkazi mmoja wa Kijiji cha Mbuli na kubomoa Nyumba (38) yakiwemo majengo ya taasisi za Serikali na Ghala la kuhifadhia mazao Kata ya Nangano,wilaya ya Liwale.
 

No comments:

Post a Comment