MKUU wa wilaya ya Kibaha,
Assumpter Mshama.
.........................................
NA MWAMVUA MWINYI,
KIBAHA
MKUU wa wilaya ya Kibaha,
Assumpter Mshama amesema ataandika ombi la kufuta hati ya shamba la mmiliki
Siemens, lililopo kata ya Pangani, kutokana na kuwa pori na kugeuzwa jalala la kutupwa miili ya
marehemu pamoja na kutumika kwa uhalifu.
Hatua hiyo inakwenda
pamoja na kuwakabidhi wananchi kulitumia kwa masharti ya kulima mazao ya muda
mfupi wakati serikali ikiendelea na taratibu za kupima viwanja na kuuza kwa
gharama nafuu.
Akitoa maamuzi hayo wakati
alipokuwa akizungumza na wananchi wa kata hiyo, Assumpter alisema ifikie mwisho
kujaza viwanja na mashamba pori
wilayani hapo.
Assumpter alitoa rai kwa
wamiliki wenye mashamba na viwanja pori kuanza
kuyaendeleza na kama watakaidi wananchi
wakiyavamia ataruhusu wagawiane maeneo.
“Hii ni salamu tuu,
mwenzio akinyolewa wewe anza kutia maji, wananchi wamechoshwa kulinda maeneo ya
watu, kama mmeyashindwa yaacheni”alifafanua
Assumpter.
Awali diwani wa kata ya
Pangani, Agustino Mdachi aliomba serikali ,kuangalia namna ya kufuta umiliki wa
mashamba ambayo hayaendelezwi na kusababisha kutumika vificho vya wahalifu .
Alisema, kwa kipindi cha
miezi sita miili zaidi ya kumi zimeokotwa kwenye mtaa huo ambapo kati yao wengine walinusurika
kifo na kuokolewa na wengine wakiwa wamefariki dunia.
Nae mwenyekiti wa mtaa wa
Pangani Jitihada Ndiali alisema maeneo hayo yamegeuzwa dampo au sehemu ya
kutupia maiti pia madereva bodaboda kuporwa pikipiki zao kisha kutupwa .
Kwa upande wa wananchi
akiwemo Lillian Godfrey alimpongeza mkuu wa wilaya kwa maamuzi yake.
Alisema, wamekubali kulima
mazao ya muda kama mihogo, mbaazi, maharage na mbogamboga hadi hapo serikali
itakapofanya maamuzi ya moja kwa moja.
No comments:
Post a Comment