Monday, December 31, 2018

SHARIFU AWATAKA VIONGOZI WA CCM BAGAMOYO WASHIRIKIANE

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bagamoyo Abduli Sharifu akizungumza katika semina ya siku mbili iliyoandaliwa na Jumuiya ya wazazi wilaya ya Bagamoyo ambayo imelenga kuwajengea uwezo watendaji wa CCM kata na makatibu wa Elima na Malezi.
...................................

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bagamoyo Abduli Sharifu amewataka wanachama wa CCM wilayani humo kuwa na ushirikiano katika kutekeleza majukumu yao ili kukiletea maendeleo chama hicho.

Akizungumza katika semina ya siku mbili iliyoandaliwa na Jumuiya ya wazazi wilaya ya Bagamoyo ambayo imelenga kuwajengea uwezo watendaji wa CCM kata na makatibu wa Elimu na Malezi, Mwenyekiti Sharifu amesema siri pekee ya mafanikio ndani ya Chama ni ushirikiano katika kutekeleza majukumu.

Sharifu ameongeza kwa kusema kuwa,  Mwenyekiti wa CCM Taifa Dkt. John Magufuli anahimiza viongozi kujituma na kuzingatia maadili ya uongozi hivyo ni vyema kila kiongozi atekeleze wajibu wake katika nafasi yake aliyo nayo.

Aliwataka wanajumiya hao ambao wamepata semina ya uongozi na maadili kuyafanyia kazi yale waliyofundishwa katika semina hiyo ili kuleta maendeleo ndani ya jumuiya ya wazazi na chama kwa ujumla.

Alisisitiza kuwa, CCM wilaya ya Bagamoyo haitamvumilia kiongozi yeyote mzembe asietimiza wajibu na kwamba hatua zitachukuliwa dhidi ya viongozi wenye kuzembea kwenye nafasi zao.

Mwenyekiti huyo wa CCM wilaya ambe awali aliwahi kuwa Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi wilaya, amempongeza Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi wilaya ya Bagamoyo Aboubakari Mlawa kwa kusimamia vizuri jumuiya hiyo na kuleta mabadiliko mbalimbali ya kimaendeleo.

Aidha, ametoa wito kwa jumuiya zote ndani ya chama kuhakikisha kuwa wanashirikiana na kuacha makundi katika kipindi cha utendaji kazi.

Alisema imezoeleka kuwa na makundi katika vipindi vya uchaaguzi lakini mara chaguzi zinapoisha ni vyema wanachama wote wakawa kitu kimoja ili kushirikiana kukijenga chama.

Alitumia nafasi hiyo kumtambulisha rasmi Katibu mpya wa CCM wilaya ya Bagamoyo, Salum Mtelela ambae anachukua nafasi ya Kombo Kamote aliyestaafu kwa mujibu wa sheria.

Mwenyekiti huyo wa CCM wilaya, alimtaka Katibu anaeanza kazi katika wilaya hiyo kufanya kazi zake kwaa kuzingatia katiba ya CCM, Kanuni, Busara na miongozo mbalimbali iliyotolewa kwa mujibu wa sheria bila ya kumuogopa mtu yeyote.

Alisema Chama Cha Mapinduzi kina Dira inayowaongoza watendaji wote katika kutekeleza majukumu yao hivyo atakaekwenda kinyume katibu ya chama itamuhukumu.

Kwa upande wake Katibu wa CCM wilaya ya Bagamoyo, Salum  Mtelela amesema anashukuru kwa mapokezi aliyoyapata na kwamba ameahidi kushirikiana na viongozi mbalimbali kwa lengo la kuimarisha chama ndani ya wilaya.

Amewataka viongozi na wanachama kwa ujumla kumpa ushirikiano ili CCM iendelee kuchukua ushindi katika chaguzi mbalimbali zinazokuja.
 
Katibu wa CCM wilaya ya Bagamoyo, Salum Khalfani Mtelela akizungumza katika semina hiyo.

Kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi wilaya ya Bagamoyo, Aboubakari Mlawa, Katibu wa Jumuiya ya wazazi Mkoa wa Pwani, Juma Gama, Mwenyekiti wa CCM tawi la Tandika Bagamoyo, Katibu Mwenezi wilaya ya Bagamoyo, Francis Bolizozo, Mjumbe wa kamati ya utekelezaji jumuiya ya wazazi wilaya ya Bagamoyo, Mariamu Hassan.  


No comments:

Post a Comment