Na. Immaculate Makilika – MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amegawa
vitambulisho kwa wajasiriamali nchi nzima wenye mitaji isiyozidi shilingi
milioni nne kwa lengo la kuwasaidia kufanya biashara zao kwa uhakika sambamba
na kutambulika katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Akizungumza mapema leo jijini Dar es salaam,
katika kikao kazi na viongozi wa TRA, Rais Magufuli aligawa jumla ya
vitambulisho 25,000 kwa kila Mkuu wa Mkoa, na kusema kuwa vitambulisho hivyo
vimelengwa kutolewa kwa wajasiriamali wote nchi nzima wenye mitaji isiyozidi
shilingi milioni nne ili viwasaidie kufanya shughuli zao mahali popote nchini,
ikiwa ni pamoja na kutambulika TRA.
Ambapo Rais Magufuli alisema kuwa vitambulisho
hivyo vinagawiwa bure, isipokuwa kila mjasiriamali atatozwa gharama ya
shilingi 20,000/= ikiwa ni sehemu ya gharama ya uandaaji wa kitambulisho
husika.
“Kitambulisho hiki nimetoa mimi bure, sioni kama
kuna mtu atakayekuja kuwasumbua, na kila Mkuu wa Mkoa atapata vitambulisho
25,000, ambapo atashirikiana na Wakuu wa wilaya ili kugawa vitambulisho hivyo
kwa wajasiriamali walioko katika mkoa wake”
Halikadhalika, Rais Magufuli aliwataka
wajasiriamali hao kuwa waaminifu, na kutokubali kufanya biashara za
wafanyabiashara wakubwa wenye mitaji yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni
nne.
Sambamba na hilo, Rais Magufuli alisisitiza
watanzania kulipa kodi kwa kuwa kodi ndio msingi wa maendeleo kwa taifa lolote
lile duniani, huku akiwataka TRA kupunguza viwango vikubwa vya kodi ambavyo
wananchi wamekuwa wakivilalamikia.
Kwa upande wake, Gavana wa Benki Kuu, Profesa
Florence Luoga alisema kuwa Benki hiyo imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali
ikiwemo kudhibiti matumizi haramu ya fedha, kuhakikisha kuwa thamani ya
fedha haiyumbi na kudhibiti matumizi ya dola kwa kufungia maduka ya
kubadilishia fedha ambayo hayakuwa na leseni.
Profesa Luoga alisema kuwa BOT iligunduwa
kuwepo kwa maduka ya kubadilishia fedha 1,000 badala ya maduka 300 yaliyokuwepo
awali na ambayo hayakuwa na leseni.
“Tunajadiliana na Waziri wa Fedha ili kuwezesha
wananchi au wafanyabiashara kulipia bidhaa kwa kutumia benki” alisema
Profesa Luoga
Profesa Luoga aliongeza kuwa kwa sasa hivi
hali ya fedha ni nzuri na hivyo Serikali ina fedha za kutosha kufanya matumizi
mbalimbali kwa kipindi cha miezi mitano ijayo na kuwataka wananchi wasiwe na
hofu.
Aidha, aliongeza kuwa kabla ya mwezi Desemba
kuisha , BOT itakuwa imeshatengeneza kanuni za kuwalinda watumiaji wa mabenki.
Naye, Kamishna wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Charles
Kichere, alisema kuwa katika kipindi cha miaka ya Serikali ya Awamu ya Tano,
TRA imefanikiwa kukusanya mapato ya jumla ya shilingi trilioni 42.9
Ambapo, katika kipindi cha robo mwaka wa fedha
2018/2019, Serikali kupitia TRA imekusanya kodi jumla ya shilingi trilioni 3.8.
Aidha, Kichere alisema kuwa licha ya changamoto
mbalimbali zinazoikabili Mamlaka hiyo, wameweza kusajili jumla ya
wafanyabiashara wadogo yaani wamachinga 97,256 huku takribani asilimia 80
ya wafanyabiashara wanatumia mashine za EFD
No comments:
Post a Comment