Monday, December 3, 2018

ABDULLAH AID, YAGAWA MSAADA WA VIFAA VYA MILIONI 50 VINGUNGUTI JIJINI DAR ES SALAAM.

 Mbunge wa jimbo la Ilala jijini Dar es Salaam, Mussa Azzan Zungu (kushoto) Mwenyekiti wa Taasisi ya Adullah Aid Tanzania, Aref Yusuf (wa pili kushoto) Naibu Meya Manispaa ya Ilala, Omari Kumbi la moto (wa tatu kushoto, kwa pamoja wakimkabidhi Cherehani mmoja wa wanufaika wa msaada huo katika hafla iliyofanyika Ofisi za Abdullaah Aid Tanzania zilizopo Kiwalani Jijini Dar es Salaam, Desemba 2, 2018.
 
Mwenyekiti wa Taasisi ya  Adullah Aid Tanzania, Aref Yusuf akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukabidhi msaada huo kwa walengwa.
.........................................

Taasisi ya Abdullah Aid kwa kushirikiana na AL-IMDAAD FOUNDATION UK. ya nchini Uingereza imegawa vitu mbalimbali jijini Dar es Salaam ikiwa ni msaada kwa watu wenye uhitaji kwaajili ya kujikimu kimaisha.

Akizungumza na waandsihi wa Habari wakati wa kugawa vitu hivyo, Mwenyekiti wa Abdullah Aid Tanzania, Sheikh Aref Yusuf Abdurrahmaan amesema wamefikia uamuzi wa kutoa msaada wa vitu hivyo ili kusaidia watu wa hali za chini ambao sio rahisi kwao kupata vitu hivyo.

Sheikh Aref alisema vitu hivyo vilivyogaiwa kwa wahitaji ni pamoja na Mashine za  Popcorn 79, Baisakeli za walemavu 6, Pikipiki aina ya TVS 1, Bajaji aina TVS 1, Mashine za Cherehani 28, Mashine ya kumwagilia maji shambani 1, na Gari moja aina Cary, vyote vikiwa na thamani zaidi ya shilingi milioni 50 ambavyo vimetolewa msaada kwa ushirikiano kati ya Taasisi ya Abdullah Aid Tanzania na Uingereza na Taasisi ya AL-IMDAAD FOUNDATION UK. ya nchini Uingereza.

Alisema wametoa msaada ambao utawanufaisha walengwa kwa muda mrefu ukilinganisha na fedha ambazo wakitumia zinaisha kwa muda mfupi bila ya kuwa na kumbukumbu.

Akitolea mfano, Sheikh Aref alisema vitu kama Cherehani, Mashine za Popcorn, Gari, Bajaji na pikipiki  vikitumika vizuri itakuwa sababu ya kujiongezea  kipato na kuweza kumudu gharama za maisha kwa mahitaji ya kila siku.

Aliongeza kuwa, utoaji wa vitu hivyo umetokana  na Mwenye kuwawezesha kufanya hivyo na kuongeza kuwa kadiri Mwenyezimungu atakavyowawezesha ndivyo watakavyoweza kufanikisha mahitaji mbalimbali kwa watu wenye uhitaji.

Aidha, ameishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wake Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutambua na kuthamini misaada mbalimbali inayotolewa na Taasisi hiyo hapa nchini huku akimpongeza mgeni rasmi katika hafla hiyo Mbunge wa Jimbo la Ilala Musa Azan Zungu kwa kukubali kufika katika ugawaji wa vitu hivyo.

Akizungumzia utaratibu unaotumika na Abdullah Aid katika kugawa misaada, Sheikh  Aref alisema Taasisi hiyo haibagui katika ugawaji wa misaada, bali inaangalia vitu walivyonavyo kwa wkati huo na kuhakikisha vinawafikia walengwa wenye uhitaji bila ya kujali dini zao.

Aliongeza kwa kusema kuwa, hiyo si mara ya kwanza kwa Taasisi hiyo kugawa misaada kwani imeshawahi kutoa misaada kwa waathirika wa mafuriko ambayo iliwafikia watanzania wote waliofikwa na madhara hayo bila ya kujali dini zao, rangi wala kabila.

Alifafanua kuwa, katika misaada inayotolewa kwa kuzingatia sheria ya uislamu ipo ile inayotolewa kama sadaka ambayo  hupewa mtu yeyote mwenye uhitaji hata kama sio muislamu, ama katika misaada inayotolewa kutokana na fungu la Zaka hii anaestahili kupwa ni muislamu tu kama maelekezo ya uislamu yanavyotaka ambapo katika hao waislamu pia wameainishwa makundi manane yanayostahili kupewa zaka.

Alisema jamii ya watanzania ina mahitaji ya vitu mbalimbali kutokana na Mwenyezimungu alivyoweka mgawanyo wa riziki hivyo wenye wanaostahili kusaidiwa wanapaswa kusaidiwa ili wapate wepesi wa sababu za kupata riziki.

Aliongeza kwa kusema kuwa, mpango huo ni katika kuunga mkono hujudi za serikali ya awamu ya tano ya kuwajali watu wanyonge na kwamba ndani ya uislamu kuna maelekezo maalum ya kusaidia jamii.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Abdullah Aid Uingereza, Shakir Majid amesema anashukuru kwa hatua hiyo waliyofikia ambayo Mwenyemungu amewawezesha kwa kushirikiana na Taasisi ya AL-IMDAAD FOUNDATION UK. ya nchini Uingereza kufanikisha misaada hiyo.

Alisema huo ni muendelezo na kwa uwezo wa Mwenyezimungu wanaweza kuendelea na mpango huo na kuwafikia watu wengi zaidi kupitia makundi yenye uhitaji.

Nae Kiongozi wa AL-IMDAAD FOUNDATION UK. ya nchini Uingereza Abduswamadu Mullah amesema kufatia ushirikiano walio nato na Abdullah Aid wataendelea kutoa misaada kwa Tanzania ili kusaidia watu wasiojiweza.

Alisema huo sio mwisho wa misaada yao kwa watu wasiojiweza Tanzania, bali wataendelea kuyafikia makundi tofauti na kusaidia mahitaji mbali mbali ya kijamii.

Akizungumza katika hafla hiyo, mgeni rasmi Mbunge wa Ilala Musa Azan Zungu alisema anaipongeza Taasisi ya Abdullah Aid kwa msaada huo na kwamba wamefanya kitu kinachohitajika katika jamii.

Alisema misaada kama hiyo ni muhimu kwani itasaidia kuwaongezea wananchi kipato na hatimae kuchangia katika maendeleo yao kwa kuwasomesha watoto wao na kuchangia katika pato la Taifa kwa ujumla.

Awali akimkaribisha Mbunge, Naibu meya wa Manispaa ya Ilala Omari Kumbi la moto alisema Taasisi ya Abdullah Aid ni Taasisi rafiki na manispaa ya Ilala kwakuwa imekuwa na msaada mkubwa katika matukio mbalimbali.

Alitumia nafasi hiyo kumpongeza Aref kwa kuijali manispaa ya Ilala na kufanya juhudi ya kuisadia serikali katika maswala ya kijamii.

Aidha, Naibu meya huyo wa Manispaa ya Ilala ambae ni Diwani wa kata ya Vingunguti alimuomba Mh. Mbunge kufikisha salamau kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli kwamba ndani ya Manispaa ya Ilala yupo mdau wa maendeleo anaejali maisha ya watu wa chini na kuchukua hatua ya kuwasaidia.

Alisema hakuna nguvu iliyotumika kumuomba misaada hiyo bali ni yeye mweneyewe kwa kuguswa kwake na maisha ya watu wa hali ya chini ameweza kutoa misaada hiyo ambayo itawasaidia wananchi wa kawaida katika kujiongezea kipato na kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Waliopata misaada hiyo ni makundi ya kina mama, kina baba, vijana, watu wenye ulemavu na wale wenye mahitaji maalum kwani vifaa hivyo itakuwa sababu ya  kuwawezesha kuinua vipato vyao katika maisha.

Wakizungumza mara baada ya kupokea misaada hiyo wananchi hao waliishukuru Taasisi ya Abdullah Aid kwa kushirikiana na AL-IMDAAD FOUNDATION UK. ya nchini Uingereza kwa misaada hiyo ambayo itawasaidia kujiongezea kipato.

Waliahidi kuitumia vyema misaada hiyo ambapo baadhi yao walisema itawasaidia kupata mahitaji ya kusomesha watoto na mahitaji ya kila siku.

Walitoa wito kwa Taasisi nyingine kuiga mfano Abdullah Aid kujitokeza na kufika mitaa ya watu wa hali ya chini ili kusaidia watu wanyonge kwa mahitaji mbalimbali.
 
 
 Mbunge wa jimbo la Ilala jijini Dar es Salaam, Mussa Azzan Zungu (kushoto) akikabidhi Baiskeli za kutembela walemavu wa migugu, Msaada uliotolewa na Taasisi ya Abdullah Aid kwa kushirikiana na AL-IMDAAD FOUNDATION UK. ya nchini Uingereza.
  Mbunge wa jimbo la Ilala jijini Dar es Salaam, Mussa Azzan Zungu akikabidhi mashine ya cherehani kwa walengwa wa msaada huo.
Mwenyekiti wa Abdullah Aid Uingereza, Shakir Majid (kulia) na
Kiongozi wa AL-IMDAAD FOUNDATION UK. ya nchini Uingereza Abduswamadu Mullah (kushoto) wakimsaidia mama moja miongoni mwa wanufaika wa msaada huo.

Naibu Meya Manispaa ya Ilala, Omari Kumbi la moto akimkabidhi Amiri Kisu funguo ya Gari yake ambayo inaonekana kwa nyuma hapo pichani.

No comments:

Post a Comment