Naibu waziri wa Nishati,
Subira Khamisi Mgalu akipokelewa na viongozi wa kata na kijiji cha Pongwe Kiona.
Naibu waziri wa Nishati, Subira Khamisi Mgalu akizungumza na wananchi wa kijiji cha Pongwe Kiona.
.....................................
Naibu waziri wa Nishati,
Subira Khamisi Mgalu amewapa faraja wananchi wa Kijiji cha Pongwe Kiona
kilichopo kata ya Kimange Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo.
Wananchi wa Pongwe Kiona
wamepata faraja hiyo baada ya kumuona naibu waziri kuwasili katika kijiji hicho
ambacho hakina historia yakufikiwa na kiongozi mkubwa wa wizara.
Akifungua mkutano mbele ya
Naibu waziri wa Nishati, Mwenyekiti wa Kijiji cha Pongwe Kiona alisema mara ya
mwisho kijiji hicho kilitembelewa na waziri wa mambo ya ndani mwaka 1960 na
kwamba toka wakati huo mpaka sasa hajawahi kufika waziri wala naibu waziri.
Aliendelea kusema kuwa,
kwa ujio wa Naibu waziri wa Nishati, Subira Mgalu wananchi wa kijiji cha Pongwe
Kiona wamepata faraja kubwa ya kuona serikali inawajali, inawathamini na
kuamini kuwa matatizo yao
yatasikilizwa.
Naibu waziri wa Nishati,
Subira Khamisi Mgalu, amefika katika kijiji hicho kuangalia changamoto
inayowakabili wananchi wa kijiji hicho kuhusu nishati ya umeme ambapo amewahakikishia
kuwa, kazi ya kufikisha umeme katika kijiji hicho itaanza Tarehe 01 mwezi Julai
2019.
Alisema katika kipindi
hicho vijiji vyote vya kata ya Kimange ambavyo vipo katika mpango wa usambazaji
umeme vijijini (REA) awamu ya tatu vitafikiwa na kupatiwa umeme.
Aliongeza kwa kusema kuwa
serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli inaendelea na mpango
wake wa kufikisha umeme vijijini hivyo wananchi waondoe hofu kila kijiji
kitapata umeme.
Alifafanua kuwa Tanzania
ina vijiji 12, 268 ambapo wakati serikali ya awamu ya tano inaingia madarakani
imekuta vijiji 8,783 havina umeme na kwamba utekelezaji umeanza na vijiji 3,559
na baadae kumalizia vijiji vilivyobaki ili umeme upatikane kijiji hadi kijiji.
Aidha, Naibu waziri huyo
wa Nishati amewataka wananchi wanaosubiri miradi kutekelezwa kwenye vijiji vyao
kufanya maandalizi ya kuupokea umeme ili miradi itakapoanza iswachukue muda
mrefu wawe wamepata umeme kwa gharama nafuu ya 27,000 tu.
Kufuatia hali hiyo
wananchi wa kijiji cha Kimange wamempongeza Naibu waziri huyo kwa kazi kubwa
anayofanya ya kuleta mabadiliko katika sekta ya umeme.
Aidha, wamemzawadia mbuzi
kwa furaha ya kufikiwa na Naibu waziri katika kijiji hicho toka miaka hamsini
iliyopita.
Awali, akimkaribisha Naibu
waziri, Diwani wa kata ya Kimange Hussein Hading'oka alisema vijiji vya kata ya
Kimange vinakabiliwa na changamoto ya kukosa umeme na kufanya mazingira ya
utendaji kazi kuwa magumu hasa katika Zahanati wakati wa kujifungua kinamama
nyakati za usiku.
Alimuomba Naibu waziri wa
Nishati kuangalia uwezekano wa kuondolea adha ya kukosa umeme wananchi wa
vijiji vya kata ya Kimange.
Meneja wa TANESCO Chalinze
Zakaria Masalu akitoa ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa Mradi wa umeme katika vijiji
vya Pongwe Kiona na Pongwe Mnazi.
Naibu waziri wa Nishati,
Subira Khamisi Mgalu akipokea zawadi ya Mbuzi kutoka kwa wazee wa Pongwe Kiona baada ya furaha yao ya kumuona Naibu waziri katika kijiji hicho baada ya kipindi cha miaka 58 kupita.
No comments:
Post a Comment