KAMATI ya Marekebisho ya Katiba ya Chama cha Waandishi wa
Habari za Michezo nchini (TASWA), imekamilisha Rasimu ya Kwanza
ya Mapendekezo ya Katiba ya chama hicho na itaanza kutolewa kwa wadau
mbalimbali leo Jumapili Desemba 9, 2018 kwa ajili ya kujadiliwa.
Hatua ya kuandaa rasimu hiyo ya kwanza imefanywa
na Kamati ya Marekebisho ya Katiba ya TASWA kwa kuangalia Katiba za vyama
mbalimbali duniani vinavyohusiana na waandishi wa habari za michezo na pia
kupitia muongozo kutoka Chama cha Kimataifa cha Waandishi wa Habari za Michezo
(AIPS), ambacho TASWA ni mwanachama.
Pia Kamati imechambua Katiba ya sasa ya TASWA na
kupokea maoni kutoka kwa waandishi wa habari za michezo kuhusu maeneo yenye
upungufu kwa nia ya kuiboresha.
Maeneo mbalimbali yamefanyiwa kazi katika rasimu hiyo
baadhi yakiwa ni sifa za mwanachama, wajibu wa mwanachama, muundo wa uongozi,
sifa za viongozi na pia ukomo wa uongozi.
Pia kuna mapendekezo katika rasimu hiyo ya kuanzishwa kamati
mbalimbali kwa nia ya kuisaidia Kamati ya Utendaji.
Kutokana na hali hiyo, Kamati imepanga hatua ya kwanza baada
ya kuitoa rasimu hiyo leo, itapokea maoni binafsi ya wadau kwa njia ya email (katibataswatz@yahoo.com), kisha itakutana na
wahariri wa habari za michezo, waandishi waandamizi na waandishi chipukizi kwa
kadri mtakavyotaarifiwa.
Baada ya kupokea maoni kutoka makundi hayo, Kamati itafanya
mikutano miwili, ambapo wa kwanza utakuwa wa wadau wote kuijadili kwa pamoja na
kisha kwa kushirikiana na Kamati ya Utendaji ya TASWA utafanyika Mkutano Mkuu
wa kuipitisha na kuiwasilisha kwa Msajili tayari kwa Uchaguzi Mkuu haraka
iwezekanavyo.
Ni matumaini ya Kamati ya Katiba kila mdau ataisoma vyema
rasimu hiyo na kutoa mchango wake na mwisho wa kufanya hivyo ni Desemba 12
mwaka huu. Mapendekezo ya Rasimu hiyo nimeambatanisha katika email zenu.
Kamati ya Katiba ya TASWA
imeundwa kutokana na agizo la Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,
Dk. Harrison Mwakyembe aliyeitaka BMT isitishe uchaguzi wa TASWA uliokuwa
umepangwa kufanyika Novemba 25 mwaka huu na badala yake BMT ikutane na viongozi
wa TASWA pamoja na baadhi ya wanahabari wa michezo kuona namna ya kuifanyia
marekebisho Katiba ya TASWA iendane na wakati.
Kamati ya Katiba inayoongozwa na Mwenyeketi wa
zamani wa TASWA, Boniface Wambura ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa
Bodi ya Ligi (TPLB), viongozi wengine ni Katibu wa Kamati Amir Mhando ambaye
pia ni Katibu Mkuu wa TASWA na mwanahabari, Gift Macha ambaye ni Katibu
Msaidizi wa Kamati.
Wajumbe ni Katibu Mkuu wa
zamani wa TASWA, Abdul Mohammed, Mhazini wa zamani wa TASWA, Nasongelya
Kilyinga na wanahabari Thabit Zacharia na Devotha Kihwelu.
No comments:
Post a Comment