Thursday, December 27, 2018

DKT JAKAYA KIKWETE AKAGUA MIRADI YA MAENDELEO KATA YA MSOGA

 Rais mstaafu wa awamu ya nne Dkt Jakaya Mrisho Kiwete hivi karibuni amekagua baadhi ya miradi ya maendeleo kwa sekta za afya na elimu na kubaini baadhi ya changamoto zinazoikabili kata ya Msoga katika sekta husika. Katika ziara hiyo Mheshimiwa Kikwete amekagua ujenzi wa miundombinu katika shule ya sekondari Mboga na kuona ujenzi wa mabweni ya shule hiyo ambapo yeye ni mlezi wa shule hiyo.


Katika ziara hiyo Kikwete aliwataka wanajamii kutambua umuhimu wa kuboresha miundombinu ya elimu katika utoaji wa elimu wenye tija kwa maana ya kuhakikisha shule zinakuwa na vyanzo vya maji vya uhakika,madarasa ya kutosha,na mabweni yanayokidhi idadi ya wanafunzi sanjari na uwepo wa nishati ya umeme mashuleni.


Aidha Mzee Kikwete aliutaka uongozi wa halmashauri ya Chalinze kushirikiana kwa ukaribu na wadau mbalimbali wa maendeleo wanaoonyesha nia ya kusaidia katika sekta za afya na elimu kwa kuweka mazingira mazuri sanjari na kuandika maandiko yenye kuwavutia kusaidia kutokana na maandishi yenye mashiko yatakayowamotisha kulingana na uhitaji wa wananchi katika huduma hizo.


Katika ziara hiyo Kikwete ametembelea hospitali ya wilaya ya Chalinze ya Msoga na kuona ujenzi unaoendelea wa jengo la upasuaji ambalo lipo katika hatua za ukamilishaji,na muda si mrefu litaanza kutoa huduma kwa wagonjwa katika halmashauri ya Chalinze,mwisho Mzee Kikwete aliwataka watumishi wa umma kufanya kazi kwa uadilifu kwa maana ya kuwahudumia wananchi na watanzania kwa ujumla pasipo kinyongo cha aina yoyote.
  
Rais mstaafu wa awamu ya nne Dkt Jakaya Mrisho Kiwete akizungumza na viongozi wa Halmashauri ya Chalinze wakiongozwa na Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Kawawa.

No comments:

Post a Comment