Tuesday, December 11, 2018

MBUNGE WA KIBAHA MJINI ACHANGIA MILIONI MBILI KUBORESHA HUDUMA YA MAJI KWA WANANCHI WA VIZIWAZIWA.

Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka akizungumza na baadhi ya wananchi wa mitaa miwili ya Sagale pamoja na viziwaziwa hawapo pichani wakati wa ziara yake aliyoifanya kwa ajili ya kutembelea miradi mbali mbali ya maendeleo pamoja na kusikiliza kero za wananchi ili kuweza kuzitafutia ufumbuzi. (PICHA NA VICTOR MASANGU)
.......................................................


VICTOR MASANGU,KIBAHA

WAKAZI zaidi ya 2500 kutoka mitaa miwili ya Sagale na Viziwaziwa katika halmashauri ya mji Kibaha mkoani Pwani  kwa sasa  bado wanakabiliwa na changamoto ya  kupata  magonjwa ya mlipuko ikiwemo kuumwa na  matumbo kutokana na ukosefu wa maji safi na salama.

Wakazi hao wanakabiliwa na hali hiyo kwasababu ya kuwalazimu kutumia maji machafu ya visima ambayo  sio salama kwa afya zao kutokana na kuchangia na wanyama mbali mbali pamoja na wadudu.

Hayo yamebanishwa na wananchi wakati wakizungumza katika mahojiano maalumu mara baada ya kutembelewa na  Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka ikiwa ni ziara yake ya kikazi kwa ajili ya kukagua miradi mbali mbali ya maendeleo pamoja na kusikiliza kero za wananchi kwa lengo la kuweza kuzitafutia ufumbuzi.

Baadhi ya wakazi hao akiwemo  Yakimu Musa pamoja na Kili Mussa walisema  kwamba kwa kipindi cha miezi sita  sasa wamekuwa wakiteseka usiku na mchana kwa ajili ya  kutembea umbari mrefu kutafuta maji ya visima ambayo hata hivyo sio salama kabisa kwa matumizi ya binadamu.


Naye Diwani wa kata ya Viziwaziwa Mohamed Masoud alibainisha kwamba hapo awali walikuwa wanapata maji kupitia mradi ujulikanao kwa jina la Savi lakini kutokana na kudaiwa deni la kiasi  cha shilingi milioni 6 walikatiwa huduma ya upatikanaji wa maji hayo na ndipo wananchi wake wakaanza kupata usumbufu mkubwa wa kutembea umbari mrefu kwa ajili ya kutafuta maji.


Katika kuliona  hilo Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka akiwa katika ziara yake ya kukagua maendeleo na kusikiliza kero za wananchi ameahidi kulivalia njuga suala hilo kwa kuwakutanisha viongozi wa mamlaka zinazohusika ambapo pia  amechangia kiasi cha shilingi milioni 2  kwa lengo la kuhakikisha huduma ya maji  inarejeshwa  kwa wananchi katika hali yake ya kawaida ili kuwaondolea adha waliyokuwa wanaipata.

“Kwa kweli mimi kama Mbunge wenu nia yangu ni kuhakikisha tunashirikiana na nyinyi katika kuzitatua changamoto mbali mbali ambazo zinawakabiliwa katika Nyanja tofauti na kikubwa katika mtaa huu wa mikongeni kitu kikubwa ni suala la maji ambalo limetokana na deni ambalo mlikuwa mnadaiwa kwa hiyo mimi nitaendeleo kuchangia zaidi na pia nitawakutanisha wahusika  katika mamlaka zinazohusika kulitafutia ufumbuzi,”alisema Koka.

WANANCHI hao wa mtaa wa Sagale pamoja na mtaa wa viziwaziwa Wilayani Kibaha mnamo mwaka 2013 waliamua kuanzisha mradi maalumu wa kusambaza huduma ya maji  kwa ajili ya kuondokana na kero  hiyo lakini  kutokana na kuibuka kwa changamoto ya kudaiwa deni hilo  mradi huo  uliweza kusimama  mwaka huu na kupelekea  usum ufu mkubwa kwa wakazi hao.
Diwani wa kata ya Viziwaziwa  Mohamed Masoud akifafanua jambo kwa wananchi wakati wa ziara ya Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini katika mitaa ya ya Viziwaziwa na Sagale (PICHA NA VICTOR MASANGU)

No comments:

Post a Comment