Friday, December 21, 2018

ALIYOYASEMA NAIBU WAZIRI WA NISHATI, SUBIRA MGALU KATIKA MAHOJIANO NA KINGS FM RADIO MKOANI NJOMBE LEO TAREHE 21/12/2018

# Ziara yangu mkoani Njombe imelenga kukagua miradi ya umeme vijijini ili itekelezwe kwa kasi na kuweza kuunganisha vijiji 125 vya Mkoa wa Njombe vilivyopangwa kuunganishwa na umeme kupitia mradi wa usambazaji umeme wa awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza unaokamilika Juni, 2019.

# Sijaridhishwa na kasi ya mkandarasi kampuni ya Mufindi katika usambazaji umeme vijijini, hata hivyo tayari nimeshazungumza naye na ameahidi kuongeza kasi.

# Nimekagua yadi ya mkandarasi huyo iliyopo Makambako mkoani Njombe na nimekuta ameleta mita za umeme zaidi ya 4000, transfoma zaidi ya 50 na vifaa vingine vinavyohitajika katika kazi ya usambazaji umeme hivyo tunaamini kasi yake sasa itaongezeka.

# Katika mradi wa Makambako- Songea, jumla ya vijini 121 vinasambaziwa umeme katika Mkoa wa Ruvuma na Njombe huku Njombe ikiwa na Vijiji 55.

# Kati ya Vijiji 121 vilivyopangwa kupelekewa umeme katika mradi wa Makambako- Songea, Vijiji 78 tayari vimeshapata umeme.

# Kuhusu changamoto ya uunguaji wa transfoma mara kwa mara mkoani Njombe na wananchi kukosa umeme kwa muda mrefu, nimeagiza TANESCO kuleta kikosi kazi kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa changamoto hii.

# TANESCO izingatie agizo la Waziri wa Nishati, la kuwa na vifaa vya akiba ili linapotokea tatizo la kifaa kuharibika kuwe na marekebisho ya haraka ili kutowakosesha wananchi umeme kwa muda mrefu.

# Vitengo vya manunuzi vya TANESCO katika Kanda mbalimbali vitathmini utendaji kazi wake hasa katika suala la kuwa wabunifu wakati zinapojitokeza changamoto za wananchi kukosa umeme kwa muda mrefu kwa sababu ya vifaa kuharibika.

# Kazi ya usambazaji umeme ilenge pia vituo vya afya 300 vinavyojengwa nchini na kama maeneo hayo yapo nje ya wigo wa wakandarasi wanaosambaza umeme, wakandarasi wawasilishe andiko serikalini ili kuweza kufanyia kazi suala hilo.

# Mkoa wa Njombe ni mdau mkubwa katika mradi wa Umeme wa Rufiji kwani kuna vyanzo vinavyopeleka maji katika mito inayotiririsha maji katika Mto Rufiji hivyo wananchi wahakikishe kuwa hawafanyi shughuli zitakazoathiri vyanzo hivyo.

# Serikali inaendelea kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali ikiwemo gesi asilia ambapo katika zaidi ya megawati 1500 zinazozalishwa nchini, zaidi ya asilimia 50 ya megawati hizo zinazalishwa kwa kutumia gesi.

# Kazi ya usambazaji gesi majumbani imeanza katika mikoa ya Dar es Salaam na Mtwara na itaendelea katika mikoa mingine nchini.

No comments:

Post a Comment